• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Messi aongoza Barcelona kupepeta Sevilla ligini na kupunguza pengo la alama kati yao na Atletico Madrid

Messi aongoza Barcelona kupepeta Sevilla ligini na kupunguza pengo la alama kati yao na Atletico Madrid

Na MASHIRIKA

LIONEL Messi alifunga bao na kuchangia jingine katika ushindi wa 2-0 uliosajiliwa na Barcelona dhidi ya Sevilla katika Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) mnamo Jumamosi.

Ushindi huo wa Barcelona uliwawezesha kupunguza pengo la alama kati yao na viongozi wa jedwali Atletico Madrid hadi pointi mbili pekee.

Barcelona kwa sasa wanashikilia nafasi ya pili kwa alama 53 japo wamesakata michuano miwili zaidi kuliko Atletico ya kocha Diego Simeone.

Sevilla wanakamata nafasi ya nne kwa alama 48, nne nyuma ya Real Madrid ambao pia wamesakata mechi 24 sawa na wao. Kichapo kilikomesha rekodi nzuri ya kutoshindwa kwa Sevilla katika jumla ya mechi 10 mfululizo za La Liga.

Ousmane Dembele aliwafungia Barcelona bao la kwanza katika dakika ya 29 kabla ya Messi kucheka na nyavu dakika tano kabla ya kipenga cha kuashiria mwisho wa mechi kupulizwa.

Bao la Messi lilikuwa lake la 38 dhidi ya Sevilla, sita zaidi kuliko idadi ya magoli ambayo amefunga mpinzani yeyote mwingine katika La Liga.

Messi kwa sasa amefunga katika mechi nane mfululizo za La Liga ambazo zimemzolea magoli 12, hii ikiwa rekodi yake bora zaidi chini ya kipindi cha miaka miwili iliyopita.

Barcelona na Sevilla watakutana tena mnamo Jumatano ya Machi 3, 2021, kwa mkondo wa pili wa nusu-fainali ya Copa del Rey. Sevilla walishinda mchuano wa mkondo wa kwanza kwa mabao 2-0.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

JAMVI: Kushindwa BBI Baringo ishara Gideon hatoshi mboga

Mbappe afunga mawili na kusaidia PSG kurefusha mkia wa...