• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 6:50 AM
Hali tete Barcelona raia wa zamani na watatu wengine wakitiwa nguvuni

Hali tete Barcelona raia wa zamani na watatu wengine wakitiwa nguvuni

Na MASHIRIKA

MAAFISA wa polisi mjini Catalonia wamesema wametia nguvuni watu wanne baada ya kufanya upekuzi katika ofisi za kikosi cha Barcelona kinachoshiriki Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga).

Miongoni mwa watu waliokamatwa ni rais wa zamani wa Barcelona, Josep Maria Bartomeu.

Kinara huyo na wenzake anatarajiwa kuhojiwa kama sehemu ya uchunguzi kuhusu matumizi mabaya ya fedha kambini mwa Barcelona wakati wa uongozi wake.

Miongoni mwa masuala yanayochunguzwa yanahusiana na sakata ya ‘Barcagate’ 2020 ambapo kikosi cha Barcelona kilianza kuvutana na kampuni inayosemekana kuwakosoa vikali wachezaji wa sasa na wa zamani wa klabu hiyo kwenye mitandao ya kijamii.

Uchaguzi wa urais kambini mwa Barcelona unatarajiwa kufanyika mnamo Machi 7, 2021 baada ya Bartomeu kujiuzulu mnamo Oktoba 2020.

Bartomeu aliwahi kuthibitisha kuwa Barcelona ilikatiza rasmi kandarasi yake na kampuni ya I3 Ventures ambayo ilikuwa imepatiwa kazi ya kupepeta sifa za Bartomeu na bodi ya klabu hiyo mitandaoni.

Kwa mujibu wa gazeti la Mundo Deportivo nchini Uhispania, kampuni hiyo ilisimamia akaunti kochokocho za mitandao ya kijamii kwa nia ya kukosoa na kuumbua wanasoka Lionel Messi, Gerard Pique, Xavi Hernandez, Pep Guardiola na Carles Puyol kupitia Facebook na Twitter.

Miongoni mwa masuala yaliyoendelezwa na Ventures ni kueneza uvumi wenye lengo la kuzua hisia kali dhidi ya Messi baada ya fowadi na nahodha huyo raia wa Argentina kuchelewa kutia saini kandarasi mpya uwanjani Camp Nou.

Mambo mengine yaliyoibuliwa ni pingamizi dhidi ya Pique kujihusisha na mashindano ya tenisi ya Davis Cup.

Mnamo Aprili 2020, wanachama sita wa Bodi ya Usimamizi ya Barcelona walijiuzulu na kumweleza Bartomeu kwamba hawakufurahishwa na namna ambavyo kikosi hicho cha La Liga kinavyoendeshwa.

Katika barua iliyoandikwa na kutiwa saini na sita hao, masuala kuhusu jinsi Barcelona itakavyoathirika kifedha kutokana na janga la corona pia yalifichuliwa.

Aidha, wanachama hao walikashifu namna ambavyo sakata ya ‘Barcagate’ ilivyoshughulikiwa.

Isitoshe, vinara hao walitaka Kamati Kuu ya Barcelona kufutilia mbali Bodi nzima iliyokuwepo wakati huo na kuagiza uchaguzi mpya wa urais.

Mbali na Emili Rousaud na Enrique Tombas waliowahi kushikilia wadhifa wa urais wa Barcelona, wanachama wengine wa Bodi waliojizulu hapo jana ni wakurugenzi wanne wakiwemo Silvio Elias, Josep Pont, Jordi Calsamiglia na Maria Teixidor.

Migogoro hiyo ya mara kwa mara miongoni mwa vinara wa klabu na kati yao na wachezaji ni kiini cha Messi kutaka kuondoka ugani Camp Nou baada ya mkataba wake wa sasa na kikosi hicho kutamatika rasmi mwishoni mwa msimu huu. Messi anahusishwa pakubwa na uwezekano wa kutua Manchester City ya Uingereza au Paris Saint-Germain (PSG) ya Ufaransa.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Jeraha kumnyima kigogo Ibrahimovic fursa ya kucheza dhidi...

Everton yapepeta Southampton na kuweka hai matumaini ya...