• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 3:25 PM
Kimani kuidhinishwa rasmi naibu kocha Bandari

Kimani kuidhinishwa rasmi naibu kocha Bandari

NA ABDULRAHMAN SHERIFF

ANTHONY Kimani ataidhinishwa rasmi kuwa naibu kocha wa Bandari FC Alhamisi ambapo anatarajiwa kuongea na wanahabari katika makao makuu ya klabu hiyo ya Mbaraki Sports Club.

Kimani ambaye alikuwa mkufunzi wa AFC Leopards amesaini mkataba wa kuifanyia kazi Bandari FC kwa msimu mmoja ambapo ataweza kuongeza muda kipindi hicho kikikamilika na akikubaliana na uongozi wa klabu hiyo.

Katika taarifa fupi ya klabu hiyo ya Bandari imesema kuwa wana furaha kutangaza rasmi kuwa Kimani almaarufu Modo ndiye naibu kocha wao kwa kipindi cha msimu mmoja lakini ataweza kuongeza muda yakifikiwa makubaliano yao na mkufunzi huyo.

“Kimani anajiunga nasi kutoka AFC Leopards ambako anatuletea uzoefu mkubwa wa kuwa katika Ligi Kuu ya Kenya huku akituahidi mazuri siku za usoni. Tunaendelea kuangazia uwekezaji wa vijana ambao ndio filosofia ya Kimani na ndio sababu anafaa kuwa kwetu,” ikasema taarifa ya klabu hiyo.

Klabu hiyo ilimkaribisha nyumbani Modo ikiwa na matumaini makubwa kuwa pamoja naye na maofisa wenzake wa benchi la ufundi, timu itafanya vizuri katika ligi na mashindano mengine yote itakayoshiriki.

Modo atakayefanya kazi pamoja na kocha mkuu Andre Cassa Mbungo anatarajia kuwa na kikao chake cha kwanza pamoja na wanahabari hivi leo kuanzia saa tatu asubuhi hapo Mbaraki Sports Club akiwa pamoja na maafisa wengine wa benchi la ufundi.

Miongoni mwa maafisa hao wanaotarajiwa kuwa pamoja naye wakati wa mkutano huo na wanahabari utakaofanyika leo asubuhi ni kocha Mbungo, meneja wa timu Albert Ogari, kocha wa makipa Wilson Obungu, naibu kocha Daniel Lenjo na nahodha Bernard Odhiambo.

Kimani aliyekuwa na Leopards alijiuzulu mwezi mmoja uliopita na kumekuwa na uvumi mkali kuwa anatakiwa na Mbungo kufanya kazi naye kwani wamewahi kuwa pamoja katika klabu hiyo ya Ingwe.

You can share this post!

Sofapaka kuwa na kikosi kamili dhidi ya Bidco United

Msanii ‘Lonely Man’ awaumbua mabinti wapenda...