• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 5:50 AM
JAMVI: Kipute kikali kati ya Rais Kenyatta na Ruto chatarajiwa Juja Mei 18

JAMVI: Kipute kikali kati ya Rais Kenyatta na Ruto chatarajiwa Juja Mei 18

Na MWANGI MUIRURI

UCHAGUZI mdogo wa eneobunge la Juja unatazamiwa kutoa taswira kamili kuhusu ushindani kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Naibu Rais William Ruto katika kumenyania roho ya kisiasa ya Mlima Kenya.

Hii ina maana kuwa kivumbi hiki cha Mei 18 kitakuwa kati ya chama tawala cha Jubilee – kinachokumbwa na misukosuko tele ikiwemo kutimuliwa kwa wandani wa Dkt Ruto kutoka nyadhifa muhimu bungeni – na kile cha United Democratic Alliance (UDA).

Chama cha UDA kinahusishwa na Dkt Ruto.

Kati ya wawaniaji ambao wametangaza nia ya kurithi marehemu Francis Munyua Waititu ‘Wakapee’ ni pamoja na mjane wake Susan Waititu, watoto wao ambao ni Martin Munyua na Michael Munyua na pia aliyekuwa meneja wa hazina ya ustawishaji eneobunge hilo Bw Kennedy Gachuma Ndung’u.

George Koimburi ambaye amekuwa akiwania na kuangukia pua pia ametangaza nia sambamba na aliyekuwa mkuu wa kitengo cha Inooro FM katika kampuni ya Royal Media Services Bw Zulu Thiong’o.

Wakapee aliaga dunia Februari 22 akiwa na umri wa miaka 62 baada ya kupambana na kansa ya ubongo kwa muda.

Kinachosubiriwa cha kuweka kivumbi hiki ladha ni mchujo wa vyama vya kisiasa na kupokezwa hati za uwaniaji na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ndio sasa isemwe “acha katambe.”

Washirika wa Dkt Ruto katika Kaunti ya Kiambu na ambao wanatarajiwa kuongoza ushindani wa kudhibiti siasa za Juja ni Mbunge wa Gatundu Kusini Bw Moses Kuria, mwenzake wa Kikuyu Bw Kimani Ichung’wa, wa Thika Mjini Patrick Wainaina, wa Ruiru Bw Simon King’ara na Seneta maalum Isaac Mwaura.

Bw Kuria na Bw Ichung’wa wamekuwa mwiba sugu katika siasa za Rais Kenyatta kufuatia ufuasi wao sugu kwa Dkt Ruto na ikifahamika kuwa Kiambu pia ndiko nyumbani – kwa kuzaliwa – kwa Rais, kivumbi hiki kinapata utamu wa kipekee.

Mrengo wa Rais unapigwa jeki na aliyekuwa gavana wa kwanza wa Kiambu Bw William Kabogo na wa sasa Dkt James Nyoro na ambao kwa sasa wanapigana mieleka ya kisiasa wakilenga kushindania ugavana 2022.

Ikiwa chama cha Jubilee hakitapata dharura ya kuungana jinsi ilivyokuwa 2013 na 2017, basi ishara zote zinaashiria kuwa mbivu na mbichi itabainika kati ya mirengo hii miwili ya Rais na Dkt Ruto na hatimaye Wakenya wapate ukweli wa mambo kuhusu ni nani atabeba ushawishi katika jumuia ya Mlima Kenya ambayo kwa ujumla inadadisiwa kuwa na kura 8 milioni.

Mjomba wa Rais

Kinachotarajiwa katika kinyang’anyiro hiki kilianza kujipa umbo siku ya mazishi ambapo mjombake Rais akifahamika kama Kapteni Kung’u Muigai alizomewa na waombolezaji alipojaribu kumkinga (Rais) kupokezwa malalamishi na matakwa ya wenyeji.

Bw Kung’u akiongoza ratiba ya mazishi hayo alikuwa amekerwa na hatua ya waliokuwa wakipewa nafasi ya kuhutubu ya kudai kila aina ya huduma akilazimika kuwaagiza “hebu tuache kumlimbikizia mapendekezo mengi Rais wetu ili katika siku zijazo asiogope kututembelea tena.”

Ndipo baadhi ya waombolezaji wakaanza kusonya na kumkebehi nusura wakatize harakati zake za kusimamia ratiba, lakini wakatulia baada ya baadhi ya wabunge kuonekana wakiwanyooshea mkono wa kuwaomba wadumishe amani.

Kumekuwa na tetesi kuwa Rais huwa anapewa ushauri mbovu ambao humtenga na wafuasi wake hasa katika ngome yake muhimu ya Mlima Kenya huku akikosanishwa na waliomfaa kwa hali na mali katika safari yake ya kutimiza ndoto yake ya urais.

Wakapee alihudumu kama meneja wa kilimo cha kahawa katika familia ya Rais kati ya 1994 na 2012 kabla ya kuwania ubunge 2013 na akapewa awamu ya pili 2017.

Ni hafla ambayo Bw Kuria alisusia, kuangazia pengo kuu kati ya Rais na Naibu wake.

Rais alikuwa ameombwa na baadhi ya waliohutubu aingilie kati ili wenyeji wapate hatimiliki za vipande vya ardhi, maji safi ya kunywa, barabara na miundombinu mingine, hali ambayo alipohutubu alisema atarejea Juja na aishughulikie.

Ni hafla ambayo pia Bw Kabogo na Bw Nyoro walipimana nguvu mbele ya Rais Kenyatta.

Walionekana kujipendekeza kwa njia ya wazi kwa wenyeji na kwa Rais na ambapo Bw Muigai alizidisha hisia za kivumbi kati ya wawili hao alipomtaja Bw Kabogo kama Gavana, hali ambayo ilitandaza msisimko mseto miongoni mwa waombolezaji.

Bw Kabogo alishindwa katika uchaguzi mkuu wa 2017 na Bw Ferdinand Waititu ambaye naye aliishia kung’atuliwa mamlakani na Bunge la Kiambu na pia bunge la Seneti baada ya kuibuliwa tuhuma za ufisadi dhidi yake na ndipo naibu wake, Bw Nyoro akatwaa hatamu za uongozi.

Hatua ya Kapteni Muigai kumpendelea Bw Kabogo ilisawiriwa kama msimamo wa Rais kuhusu wapinzani hao wawili.

Bw Kabogo katika siku za hivi karibuni ameonekana kumkaribia rais na amebadilisha ,msimamo wake wa kupinga BBI na kwa sasa ni miongoni mwa wanaopigia debe kwa dhati.

Hali ya kumpendelea Bw Kabogo iliendelezwa mbele na mwanawe marehemu, Michael Munyua ambaye alipopewa nafasi ya kurudisha shukran, alimmiminia sifa gavana huyo wa awali huku akijitenga na kutambua Bw Nyoro na wengine.

“Wakati tulimwandama Bw Kabogo ili awe mwenyekiti wa kamati yetu ya kinyumbani ya mazishi, alikubali na ametufaa sana kwa njia ya haki. Ni rafiki wa kweli na ambaye kujitolea kwake ni kwa kutamanika na Mungu amsaidie,” akasema Bw Munyua; sasa ikibainika kuwa anatarajia kuungwa mkono na gavana huyo wa zamani kurithi mikoba ya marehemu babake kama mbunge.

Bw Kabogo alikuwa awali amejiangazia kuwa wa karibu sana na familia ya mwendazake ambapo alikariri jinsi alivyokuwa akiandamana na mke wa Wakapee hospitalini kumjulia hali.

“Hata akiaga dunia nilikuwa karibu na ambapo nilimgusa kichwa na nikajua ameenda… Nikamvuta mjane kando na nikamfahamisha kuhusu tukio hilo nikimsihi ajiandae kujipa nguvu,” akasema Kabogo.

Bw Kabogo aliongeza kuwa yeye ndiye alisaka idhini ya kuandaa misa katika Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Jomo Kenyatta (JKUAT) huku akimwagiza Naibu Chansela Bi Victoria Ngumi asimame kuthibitisha hayo.

Bw Nyoro aliposimama kuhutubu alishangiliwa na kundi la waombolezaji waliokuwa wamekaa katika sehemu moja ya hema, nao mrengo mwingine ukishangilia Bw Kabogo katika hema tofauti, kuashiria hali kwamba walikuwa wamejipanga kimakusudi.

Gavana Nyoro alimkumbuka mwendazake kama aliyekuwa na sifa za kupenda mtindi kiasi cha kubandikwa jina la majazi la “Wakapee” mkarimu, mwadilifu na mchapa kazi.

“Jina Wakapee linatokana na ukarimu wake wa pombe ambapo alikuwa akisema kwa baa watu wapewe…” Nyoro akadai, msimamo ambao Rais na Spika wa Bunge la Kitaifa Bw Justin Muturi kimafumbo walikubaliana nao.

Rais Kenyatta alisema kuwa marehemu hajashikwa na kashfa yoyote wa wizi wa rasilimali za umma huku mbunge wa Kiambu Mjini Bw Jude Njomo akimpendekeza mjane Susan Njeri kuibuka mbunge.

You can share this post!

Dortmund wadengua Sevilla na kutinga robo-fainali za UEFA...

TAHARIRI: Handisheki bila amani haitoshi