Polisi waendelea kukamata wanaodai Magufuli anaugua

Na WAANDISHI WETU

POLISI nchini Tanzania wamezidisha msako dhidi ya raia wanaoeneza uvumi kuhusu hali ya afya ya Rais John Pombe Magufuli hasa kupitia mitandao ya kijamii.

Rais huyo ambaye kwa kawaida alikuwa akikagua miradi ya umma na kufanya mikutano ya hadhara mara kwa mara, hajaonekana kwa zaidi ya wiki mbili sasa.

Ingawa maafisa wakuu wa serikali wamesisitiza hali yake ya afya ni shwari, duru nyinginezo zimekuwa zikidai anaugua na serikali inafichia wananchi ukweli.

Jeshi la Polisi jana lilisema watu wanne walikamatwa katika maeneo mbalimbali kwa kueneza habari za uzushi kinyume na sheria ya makosa ya kimtandao.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka jeshi la polisi nchini humo, mtu mmoja alikamatwa mkoani Iringa, mwingine jijini Dar es salaam na wawili wamekamatwa mkoani Kilimanjaro.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Ronald Makona jana alisema, watu hao walikamatwa kwa nyakati tofauti.

Aliwataja waliokamatwa Kilimanjaro kuwa ni Peter Pius Silayo, 30, ambaye ni mkazi wa Tegeta Dar es Salaam, aliyekamatiwa eneo la Kibaoni Tarakea Wilaya ya Rombo na Melchiory Prosper Shayo, 36, mkazi wa Keni, Wilaya ya Rombo.

“Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro limemkamata na kumshikilia Peter Pius Silayo na Melchiory Prosper Shayo kwa kosa la kusambaza taarifa za uzushi kwenye mitandao ya kijamii kinyume na Sheria ya makosa ya Mitandao kuwa viongozi wakuu wa Serikali ni wagonjwa,” akasema.

Hata hivyo, hakufafanua wazi kama habari walizodaiwa kusambaza zilimhusu Magufuli.

Kamanda alisema watuhumiwa watafikishwa mahakamani baada ya uchunguzi kukamilika.

Aidha, Jeshi la Polisi mkoani hapa limetoa wito kwa jamii na wananchi kwa ujumla kuacha kusambaza taarifa ambazo hazina ukweli, na kwamba hatua kali zitachukuliwa kwa wale watakaobainika.

“Hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa mtu yeyote atakaebainika ametoa au amesambaza taarifa za kupotosha umma na kusababisha taharuki kwa jamii,” idara hiyo ya usalama ikasema.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa alisema rais wa nchi hiyo yupo salama na anaendelea na majukumu yake kama kawaida.

Majaliwa alitahadharisha kuwa kumekuwa na upotoshaji mkubwa unaofanyika juu ya afya na alipo Magufuli katika siku za hivi karibuni.

Alizungumza baada ya swala ya Ijumaa katika Msikiti Mkuu wa Mkoa wa Njombe ambapo alikashifu Watanzania wanaoishi nje ya nchi kwa kueneza “uzushi na upotoshaji huo.”

“Tangu juzi mpaka leo asubuhi tunaona watanzania wenzetu wenye husda wanashawishi vyombo vya kimataifa wasema rais wa Tanzania anaumwa, kajifungia, tena hata hawapo Tanzania wapo nje. Sisi tupo ndani lakini tupo kimya. Wanaona fahari kuisema nchi yao vibaya,” akasema Majaliwa.

Chama kikuu cha upinzani nchini humo (Chadema) kiliitaka serikali ya kujitokeza na kueleza alipo Magufuli.

Katika mkutano na wanahabari, Katibu Mkuu wa Chadema John Mnyika alisema kuwa wananchi wana haki ya kupata taarifa rasmi kutoka serikalini kumhusu kiongozi wa nchi yao.

Habari zinazohusiana na hii

SULUHU APATA MPANGO TZ