• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 5:20 PM
Utawala wa Magufuli ulivyoua demokrasia Tanzania

Utawala wa Magufuli ulivyoua demokrasia Tanzania

Na SAMMY WAWERU

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli na aliyefariki Jumatano akiwa na umri wa miaka 61, atakumbukwa kwa msimamo wake mkali katika uongozi.

Katika majukwaa mengi, msimamo wa utawala wake umetajwa kuwa wa kidikteta na uliokandamiza demokrasia ya raia wa nchi hiyo, mashirika ya haki za kibinadamu na pia vyombo vya habari.

Huku akitambulika kwa jina la lakabu kama “Bulldozer”, Rais Magufuli aliiaga dunia kutokana na kile serikali ilisema ni tatizo la moyo baada ya kutoonekana machoni pa umma kwa muda wa wiki kadha bila sababu.

Kukosekana huko, hisia mseto zilizuka, tetesi zikihoji aliambukizwa virusi vya corona.

Alipochukua hatamu ya uongozi miaka mitano-sita iliyopita, aliapa kupambana vilivyo na mafisadi, ila kwa wadadisi wengi alivyochukulia janga la Covid-19 iliibua maswali chungu nzima.

Rais Magufuli na ambaye alikuwa Mkristu, alidai maombi yaliokoa Tanzania dhidi ya corona, akihimiza haja ya maombi badala ya kuvalia barakoa.

Isitoshe, aliamuru kusimamishwa kutolewa kwa takwimu za maambukizi ya janga hili ambalo ni kero la kimataifa, na pia kuonya vyombo vya habari “visithubutu kuzichapisha”.

Mwezi uliopita, Februari 2021, mambo yalizidi unga. Visa vya maambukizi ya corona Tanzania vilipanda, kiasi cha maeneo ya kuabudu, shule, taasisi za umma na mashirika mengine kutoa tahadhari.

Makamu wa Rais wa Zanzibar, Bw Seif Sharif Hamad akafariki kipindi cha janga hili, chama chake kikikiri aliangamizwa na Homa ya virusi vya corona.

Kufuatia msukumo na presha ya wakosoaji wake na pia mataifa ya kigeni, Rais Magufuli aliinua mikono na kusalimu amri, akaungama virusi vipo, kinyume na kauli yake ya awali.

“Ugonjwa huu wa mapafu ulipolipuka mwaka uliopita, tuliibuka washindi kwa sababu tuliweka Mungu mbele na kuweka mikakati mingine. Nina uhakika bado tutashinda tena mara hii,” akasema.

“Huu ugonjwa na mengine ya mapafu yapo, yameua watu wengi katika mataifa mengine. Sote tutafariki aidha kutokana na ugonjwa huu, Malaria au mengineyo. Tumrejelee Mungu, pengine tulikosea mahali,” Rais Magufuli akanukuliwa akieleza.

Ni matamshi yaliyoashiria “kiongozi aliyejawa na hujuma na kupuuza mengi”.

Rais Magufuli alipochaguliwa mara ya kwanza mwaka wa 2015, aliapa kupambana na ufisadi, ila sakata za ufujaji wa mali ya umma zilizidi.

Sikukuu ya maadhimisho ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupata uhuru wa kujitawala, aliifutilia mbali, na mahala pake kuchukuliwa na usafi wa mazingira na barabara za mitaa.

Isitoshe, alipiga mafuruku baadhi ya ziara za kigeni za maafisa wa umma.

Utendakazi wake uligonga vichwa vya vyombo vya habari, kufuatia visa ambapo alitaka kuelezwa hadharani kwa nini baadhi ya watumishi wa umma hawakuwa katika mahala pao pa kazi.

Wengine walishtakiwa na kufungwa jela, kwa kile Rais Magufuli alihoji ni “utepetevu kazini kwa kufika kama wamechelewa afisini”.

Ni utawala wa kimabavu na kidikteta, ambao nchi rafiki za Tanzania zilikosoa kwa kukandamiza demokrasia, katika taifa linalojulikana kuwa tulivu Ukanda wa Afrika Mashariki.

Kuchaguliwa kwake tena Oktoba 2020, kuhudumu awamu ya pili na ya mwisho, kulikosolewa na wapinzani wake na pia waangalizi wa chaguzi.

Aidha, uchaguzi huo ulishuhudia vikosi vya kijeshi Tanzania kuhangaisha vyama vya upinzani na pia kuzima vyombo vya habari vya kigeni na waangalizi.

“Alihujumu na kudhalilisha mengi, kuanzia sheria, haki za kibinadamu…kila kitu,” akasema Aikande Kwayu, mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Tanzania.

Chini ya utawala wake, sheria zilizolenga kuhujumu vyombo vya habari zilipitishwa, wanahabari na watetezi wa haki za kibinadamu kukamatwa kiholela, na pia viongozi wa upinzani kuuawa.

Kuna haya matamshi yaliyoacha wengi vinywa wazi “wasichana wanaopata ujauzito wakiwa shuleni wafurushwe”.

“Chini ya utawala wangu, sitaruhusu msichana yeyote wa shule kushiriki mambo ya watu wazima. Hata kwangu, akipata mimba nitamtimua,” alisema Rais Magufuli, matamshi ambayo yalizua tumbojoto na kukosolewa vikali kuhusu haki za mtoto wa kike.

Serikali yake iliendesha kamatakamata ya wanachama wa LGBT – kikundi kilichofafanuliwa kwa hiari cha wasagaji, mashoga na jinsia mbili, jinsi ilivyofanyika oparesheni hiyo ikikosolewa na makundi na mashirika ya kutetea haki za kibinadamu.

Utawala huo wa kidikteta na unaotafsiriwa kuwa wa kiimla, ulisifiwa na wafuasi wake hasa katika vita dhidi ya mafisadi, mageuzi katika sekta ya madini, ambapo alijadiliana na wanakandarasi wa ughaibuni ili kuona Tanzania inapata mgao wake wa raslimali hiyo.

You can share this post!

Rais Kenyatta atangaza siku 7 za kumwomboleza Magufuli,...

Kifo cha Magufuli chamletea Harmonize dhiki kuu