• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 3:25 PM
MAUYA OMAUYA: Shujaa Magufuli: Hakika chema kamwe hakidumu

MAUYA OMAUYA: Shujaa Magufuli: Hakika chema kamwe hakidumu

Na MAUYA OMAUYA

Bwana ametoa, Bwana ametwaa…” Maneno haya ya Makamu wa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan juzi, Jumatano usiku yalizima mwanga wa matumaini na kuatua nyoyo za mamilioni ya watu barani Afrika na ughaibuni.

Wasiwasi wa kutojua hali yake Rais Dkt John Pombe Magufuli uligeuka kuwa giza la simanzi ya mauti. Jembe kuu la Chato limevunjika mpini na kusalia mchangani milele. Kifo cha Rais Magufuli ni pigo kuu kwa Tanzania na Afrika.

Rais Magufuli aliwapa Waafrika wengi matumaini na kuwafanya watafaharie bara lao.

Katika jumuiya iliyojaa uozo, ufisadi, utapeli wa kisiasa na uongozi mbaya, Ndugu Magufuli aliwapa wengi sababu ya kutabasamu na ari ya kusadiki kwamba hatimaye Mwafrika atajinasua kutoka kwa minyororo ya uongozi mbaya na hila za ukoloni mamboleo.

Alikuwa na nia na msukumo wa kweli kubadili maisha ya raia wa nchi yake, hasa hohehahe wa kule vijijini na mabandani.

Ikiwa ungwana ni vitendo, Magufuli alikuwa Mwungwana kwelikweli. Kile kingefanyika leo hakusubiri kesho ije! Kila nilipomwona akishirikiana na raia katika kung’arisha jiji, akizoa taka na kuzibua mabomba jijini Dar es Salaam nilipata taswira ya Mwalimu Julius Nyerere au Thomas Sankara wa Burkina Fasso.

Alipenda uhuru wa Waafrika na hakuruhusu makampuni ya kimataifa kutumia nchi yake kama wanda la majaribio au kuruhusu Watanzania kukandamizwa kupitia ajira mbovu mbovu za waajiiri wa kigeni.

Nilipenda zaidi alivyofafanua uwezo wa mataifa ya Afrika kutengana kabisa na mitego ya misaada ya kigeni. Alichukia rushwa na kukataa uzembe serikalini.

Kila alipozungumzia mada ya Afrika kujitegemea, ulihisi msisimko mpya na ari kuu. Katika Magufuli uliona ndoto ya mabingwa wa uhuru na uafrika.

Katika mikakati yake ya uzalishaji na miundomsingi uliona mawaidha ya Kwame Nkrumah, jagina wa Ghana na Afrika.

Katika sisitizo la kukataa ufyonzaji wa mabepari wa kigeni uliona moyo wa mwalimu wake Nyerere. Katika nasaha kwa raia akiwatia shime wajiinue kwa bidii yao, uliona ndoto wa Marcus Garvey.

Hakika, jina lake la utani, Buludoza alilipata kwa sababu ya bidii yake ya mchwa alipokuwa waziri wa barabara. Kwa siku kadhaa, kimya na wingu la usiri vilitanda kote kuhusu hali yake.

Tulisubiri kwa hamu kufahamu kwa nini buludoza ametoweka bila kutuarifu. Tulimtakia kila kheri na kumpigia dua aepukane na kila shari. Tulilolitaka halikuwa. Kumbe Chema Hakidumu!

Ni masikitiko zaidi kwa sababu Dkt Magufuli amefariki wakati mgumu sana. Ameaga dunia kabla hajalainisha msimamo wake kuhusu janga tunalokabiliana nalo la Korona.

Wakosoaji wake watasalia na pambio hilo kwamba Rais Magufuli alikaidi uwepo wa Korona na kuwaweka raia wake katika hatari. Si neno, Mkamilifu ni Mola.

Ukweli ni kwamba ushupavu wake kama rais utasalia katika kilele cha kumbukumbu ya wote waliomfahamu.

 

You can share this post!

Wezi wakata vyuma vya daraja la Makupa

FRANCIS MUTEGI: Suluhu awe mwanga mpya Tanzania...