• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 8:55 PM
FRANCIS MUTEGI: Suluhu awe mwanga mpya Tanzania ikimwomboleza Magufuli

FRANCIS MUTEGI: Suluhu awe mwanga mpya Tanzania ikimwomboleza Magufuli

Na FRANCIS MUTEGI

NILIPOKEA habari za kifo cha kiongozi shupavu John Joseph Pombe Magufuli kwa masikitiko makubwa. Rambirambi kwa mjane mama wa taifa Janeth Magufuli, na wanawe, pamoja na jamaa, marafiki na Watanzania kwa jumla.

Katika kipindi hiki cha siku 14 za maombolezi, na maagano na mwendazake rais Magufuli, kila mcha Mungu ana sababu ya kuamini kwamba amepokelewa paradiso na jeshi la Malaika kutokana na uadilifu na umakinifu wake kwa kanisa na ukristo.

Isisahaulike kwamba hakuwa tu Mkristo Mkatoliki bali aliwahi kuwa seminari akisomea upadre japo hakuhitimisha somo hilo kuitwa kasisi. Badala yake aligeukia ualimu wa somo la kemia kabla ya kujitosa katika majukwaa ya kisiasa, hadi kuwa rais wa tatu wa Tanzania.

Akiwa rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania kuanzia 2015 hadi mauti, anastahili tuzo ya kufanya kazi na kupigania uadilifu wa viongozi wa serikali Tanzania; na utumizi wake wa rasilimali za nchi kuiendeleza, daima unastahili pongezi na kupigiwa mfano.

Ukweli ni kwamba marehemu Magufuli aliipaisha Tanzania kimaendeleo na kiuchumi. Avuliwe kofia kwa utendaji na uwajibikaji katika matumizi makubwa yasiyo na gharama kubwa kwa umma, kwa kupunguza hasa ufisadi na upotovu wa viongozi wa utawala, ikilinganishwa na nchi nyingine majirani, hususan Kenya.

Hata hivyo, kwa upande mwingine, alikosea sana Tanzania na nchi zetu za Afrika Mashariki, kwa kuzingatia viwango vya ukaidi vilivyoishia kuitenga Tanzania na Afrika nzima. Ila alidinda kabisa kukubali udhaifu huu hata kwa kiwango cha kuilazimisha stesheni moja ya Kenya kuomba radhi kwa wiki nzima, kwa kutumia tago la ‘Ukaidi wa Magufuli’.

Hapana shaka alitumia sera za uchumi zilizoangazia ustawi wa taifa la Tanzania, japo hasa kwa kujiweka kando na majirani zake.

Vile vile, alikosa kuthamini ujirani mwema, ushirikiano na umoja wa kuipa Tanzania nguvu zaidi, alipoonekana kukosa muambata na kaka zake marais wa nchi za Jumuia ya Afrika Mashariki, na kuendeleza zaidi muungano wa Kusini mwa Afrika SADC.

Matarajio ya wengi ni kwamba mrithi wake, ambaye ni rais mtarajiwa Bi Samia Suluhu Hassan, msomi wa vyuo vikuu vya Manchester na New Hampshire, atapaza sauti yake kwa majirani na dunia nzima, kupata kurunzi ya mwanga wa uwazi, utii wa sheria za kimataifa na ujirani mwema wa kushikana mikono na wanaopakana nao, kusudi wazikwee ngazi zote pamoja hususan na wana-EAC.

Kadhalika aanze sera na mikakati ya kusitiri Watanzania wote dhidi ya corona, kwa njia za kitaalamu zinazotumika kote duniani.

Aidha, kama mzaliwa kisiwani Zanzibar, Bi. Suluhu Hassan atahitajika kumteua makamu wake kutoka Tanzania Bara.

Aidha, Mama Suluhu atamulikwa kwa darubini sio tu za Tanzania bali za dunia nzima, kuona iwapo ataondolea mbali makiukaji ya haki za kibinadamu, ukatili unaoelekezewa wakosoaji serikali na upinzani, kadhalika kutokomeza ukandamizaji vyombo vya habari, kama nguzo kuu za kumaliza kile ambacho kinawatenganisha na nchi za Afrika mashariki.

Ahimizwe kuzidisha sera za uchumi na maendeleo endelevu, alizothamini sana mkuu wake mtangulizi, na mwanarika wake John Magufuli (umri sawa wa miaka 61), ila kwa mshikamano haswa na majirani.

Mzee wa kazi Magufuli alikuwa Mkatoliki shupavu anayestahili sifa kwa misimamo thabiti ya Imani katika maweza ya Ukristo, pengine kutokana na asili ya siku zake katika seminari ya upadre.

Hakika anastahili heshima si kejeli kwa mengi mazuri aliyotenda; na ikubalike kwamba ilivyo kwa binadamu yeyote yule, alikuwa na mapungufu na mawili matatu ya kukunjiwa uso, hasa yaliyokosa kufaa mkosoaji wake; na mstakabali wa mrithiye uwe kuyabadilisha na kuyapa ubora ustahilio.

Kwa ufupi tumpumzishe kwa tahadhima, kwani kaenda kwa Muumba wake, na yote ya dunia aliyohusishwa nayo, jaji mkuu ni Mwenyezi Ilhai.

Mola humpenda sana muungwana, muadilifu, mzalendo na muwajibikaji, sifa anazofaa kuvikwa mwendazake kiongozi Pombe Magufuli, hususan alivyohimiza utangulizi Mungu, katika kila jambo.

Tukubali kwamba sawa na mimi na wewe, hakuwa mkamilifu, ndio maana akakosa ujasiri wa kukiri sayansi ni kazi ya Mungu mwenyewe, na wajuzi wa usomi huu, kawapa uwezo mkubwa sana Mungu muumba, ili waendelee kumuumbia na kumtunzia alichokiumba yeye. Wasemavyo wahenga wa zama za babu zetu, mghala muue na chake umpe; na kweli hujafa hujaumbwa!

Mola aiangaze roho yake katika mwanga wa milele kwenye uzima wake, na ailaze roho yake Magufuli mahali pema peponi. Amina.

 

You can share this post!

MAUYA OMAUYA: Shujaa Magufuli: Hakika chema kamwe hakidumu

DOUGLAS MUTUA: Nenda salama Magufuli