FC Talent inavyokuza talanta za vijana chipukizi

Na JOHN KIMWERE

KLABU ya FC Talent ni miongoni mwa vikosi vinavyotifua vumbi la kufa mtu kwenye juhudi za kuwania ubingwa wa taji la Ligi ya Kaunti msimu huu.

Kocha wa kikosi hiki, Patrick Kegonde anasema ”Tumepania kujitahidi kadiri ya uwezo wetu kukabili wapinzani wetu michezoni nia yetu ikiwa kubahatika kunasa tiketi ya kupandishwa daraja msimu ujao.”

Ofisa huyo anadokeza kuwa wachezaji wake wanatamani sana kushiriki mechi za ligi ya juu muhula ujao. Pia anasema kuwa raundi hii wamejipanda kupambana mwanzo mwisho na wapinzani wao kwani wanahisi wanaweza kupiga hatua michezoni.

”FC Talent sio klabu ya jana ilianzishwa mwaka 2012 lakini ukata umekuwa donda sugu hali iliyozima ndoto yetu kusonga mbele. Mara mbili tulishiriki mechi za ligi ya Wilaya tulipopanda ngazi mwaka 2013,” alisema nahodha wa FC Talent, Godfrey Ekol na kuongeza kuwa mara nyingi wamekuwa wakilemewa kugharamia nauli ya kushiriki mechi za ugenini.

”Bila kuweka katika kaburi la sahau nambuka kuna wakati tulifuzu kupandishwa ngazi lakini tulikosa ufadhili wa kutupiga jeki kushiriki ngarambe ya Kaunti. Hali hiyo ilifanya tutulie na kuendelea kucheza mechi za Ligi ya Kaunti,” alisema. Klabu hiyo imekuwa ikipitia wakati mgumu lakini pia imekuwa ikimaliza kati ya nafasi zisizozidi kumi.

Ingawa tumepitia changamoto nyingi tangia tuanze kushiriki michezo ya shirikisho la soka la Kenya (FKF) tunajivunia kukuza talanta za mchezaji mmoja ndani ya kipindi kisichopungua miaka mitano.

Nahodha huyo anadokeza kuwa msimu huu wana imani ya kufanya kweli na kunasa tiketi ya kufuzu kupandishwa ngazi kushiriki mechi za Nairobi West Regional League (NWRL) msimu huu. Anatoa wito kwa wachezaji wenzake kuwa wasilaze damu dimbani bali wajitahidi zaidi ili kutimiza maazimio yao.

Anasema kuwa wameanza kampeni zao vibaya ambapo wamevuna alama saba kutokana na mechi saba kwa kushinda patashika mbili, kutoka nguvu sawa mara moja na kudondosha michezo miwili.

Nahodha huyo anakiri kuwa kipute hicho kinashuhudia upinzani mkali ambapo wakiteleza tu ni rahisi ndoto yao kuzimwa. Mchezaji huyo anataja baadhi ya wapinzani wao wanatisha kwenye kampeni za kipute hicho kama Imara FC kati ya zingine. Kocha wa klabu hii anatoa wito kwa wahisani wajitokeze na kuungana nao ili kunoa makucha ya wachezaji wanaoibukia.

FC Talent inajumuisha wachezaji kama:Martin Agoi, Godfrey Ekol (nahodha), Sammy Boluma, Brian Ingati, Andrew Musungu, Douglas Oduor, Brian Omoja, Bryant Omwange, Godfrey Amalemba, Nick Kivuli, Justin Shivangi, Curren Ameda, Anderson Juma, Bonventure Ayuya.

 

Habari zinazohusiana na hii