• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 7:55 AM
AKILIMALI: Jinsi unavyoweza kuzalisha mparachichi kutoka kienyeji hadi Hass

AKILIMALI: Jinsi unavyoweza kuzalisha mparachichi kutoka kienyeji hadi Hass

Na MWANGI MUIRURI

KILIMO cha parachichi aina ya Hass kimekuwa kikiwazolea wazalishaji pesa kwa wingi kiasi kwamba wengi wamekuwa wakitupilia kilimo cha kahawa, majani chai na migomba ya ndizi ili kukikumbatia.

Mparachichi mmoja kwa mwaka umekadiriwa kuwa ukitunzwa kwa njia inayofaa, unaweza ukakupa kati ya Sh18,000 na Sh25,000 kwa mwaka.

Miche ya parachichi aina ya Hass inaweza ikanunuliwa kutoka kwa wafanyabiashara wa mauzo ya mimea na pia, unaweza ukajizalishia.

Kwa mujibu wa mtaalamu wa uzalishaji miparachichi katika Kaunti ya Murang’a Bw Mwangi wa Njeri, kujizalishia mimea hii katika shamba lako ndiyo ya uhakika zaidi kupata ubora unaohitajika.

“Shida ya kununua miche hii kutoka kwa wafanyabiashara ni kwamba, wengi wao huwa na ule utundu wa kuwa na mvuto wa kibiashara wala sio ubora wa miche. Ni katika harakati za kujipa uhakika wa ubora ambapo ningekushauri ujizalishie miche ya Hass moja kwa moja katika shamba lako,” asema.

Bw Mwangi anashauri kuwa hatua ya kwanza katika kujipa ubora wa miche ya Hass ni kukusanya mbegu za parachichi ambazo ni za kienyeji.

“Mbegu za kienyeji ndizo mufti zaidi kutumia katika mkakati wa kuzindua awamu ya kuishia kuwa na miche bora ya Hass. Mbegu hizi unafaa uzipande kwa mashimo ambayo yametengana kwa futi nane mraba. Zikishamea, unafaa uipe miche hiyo muda ili angalau iwe na urefu wa futi mbili,” asema.

Hatua ya pili ni kusaka mparachichi wa Hass ulio na ubora wa juu na uvune matawi ambayo utatumia kuzalisha ile mimea yako ya kienyeji. Matawi hayo yanaitwa kwa kingereza “buds” na huchaguliwa kwa ustadi mkuu ambapo cha kuzingatia ni saizi ambayo itaingiana na ile mimea ya kienyeji shambani mwako.

Ukishachagua badi hizo, utahitaji wembe na makaratasi ya plastiki.

Utakata mmea ule wa kienyeji katika kiwango cha urefu wa futi moja na nusu na kisha ukate shina lake kuanzia juu katikati ukielekeza chini ili kuunda nafasi ya kupenyeza badi ile ya Hass.

Bw Mwangi Wa Njeri akuonyesha jinsi unavyofaa kukata shina la mmea wa kienyeji wa mprachichi katika maandalizi ya uuzalisha uwe aina ya Hass. Picha/ Mwangi Muiruri

Awamu ya pili ni kuchonga ile badi ili iingie katika ile nafasi uliounda katika mmea wako wa kienyeji.

Bw Mwangi wa Njeri akuonyesha badi ya Hass iliyochongwa na ambayo iko tayari kupenyezwa iiingie katika shina la ule mmea wa kienyeji. Picha/ Mwangi Muiruri

Katika awamu ya tatu, ukishaingiza ile badi ya Hass katika shina la mmea ule wa kienyeji, utaifunga kwa karatasi ile ya plastiki ili kuiunganisha na kuipa uwezo wa ushikamano.

Bw Mwangi wa Njeri aonyesha jinsi ambavyo ukishaingiza badi ya Hass katika shina la mmea wa kienyeji unafaa kufunga ili ishikamane. Picha/ Mwangi Muiruri

Hayo yakishafanyika, utangoja kwa kipindi cha kati ya wiki tatu na nne ambapo utafuatilia uone kama ile badi ilijipa ushikamano wa uhai na kuchipuza majani, ishara kwamba imekubali kunawiri.

Mizizi yake itakuwa ni ya kienyeji hadi pale ‘upasuaji’ wa ufundi wa kupenyeza badi ulitekelezewa lakini kuanzia hapo ni shina na matawi ya Hass na ambayo hatimaye yatatoa mazao uliyolenga.

Wakati mmea mmoja wa Hass huuzwa kwa kati ya Sh200 na Sh300 kutoka kwa wafanyabiashara wa miche, kujizalishia katika shamba lako hupunguza gharama.

Mbegu unaweza ukaziokota sokoni au kutoka kwa shamba bila kulipia chochote au ununue tu parachichi la kienyeji lililoiva kwa gharama ya Sh10 ili upate mbegu.

Hatimaye, ikishamea, Bw Wa Njeri atakutoza Sh40 kuzalisha kila mmea hivyo basi kujumlisha gharama ya mche mmoja wa Hass kuwa Sh50.

You can share this post!

Watu 26 wafariki kwa corona

Ujerumani yakomoa Iceland 3-0