• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Italia wapepeta Northern Ireland bila jasho jingi katika mechi ya kufuzu kwa Kombe la Dunia

Italia wapepeta Northern Ireland bila jasho jingi katika mechi ya kufuzu kwa Kombe la Dunia

Na MASHIRIKA

ITALIA waliwapepeta Northern Ireland 2-0 mjini Parma mnamo Alhamisi katika mchuano wao wa ufunguzi wa kampeni za kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia za 2022.

Domenico Berardi aliwafungulia Italia ukurasa wa mabao katika dakika ya 14 kabla ya Ciro Immobile kupachika wavuni goli la pili katika dakika ya 38 baada ya kumwacha hoi kipa Bailey Peacock-Farrell.

Ingawa mabao hayo mawili yaliwaamshia Northern Ireland ari ya kurejea mchezoni, juhudi za wavamizi wao Gavin Whyte na Paddy McNair hazikuzaa matunda.

Chini ya kocha Ian Baraclough, Northern Ireland kwa sasa wanajiandaa kuvaana na Bulgaria katika mchuano wao ujao mnamo Machi 31 katika uwanja wa Windsor Park mjini Belfast. Kabla ya mechi hiyo, kocha Baraclough atakuwa amewaongoza vijana wake kupimana nguvu na Amerika mnamo Machi 28.

Tangu aaminiwe kuwa mrithi wa mkufunzi Michael O’Neill mnamo 2020, Baraclough aliyekuwa kocha wa chipukizi wasiozidi umri wa miaka 21 nchini Northern Ireland, bado hajashinda mechi yoyote kati ya tisa zilizopita.

Kibarua dhidi ya Italia hata hivyo kilitarajiwa kuwa vigumu ikizingatiwa kwamba Italia hawajawahi kupoteza mechi yoyote kati ya 23 zilizopita tangu mikoba yao itwaliwe na mkufunzi Roberto Mancini mnamo 2018.

Aidha, mabingwa hao mara nne wa Kombe la Dunia hawajawahi kupoteza mechi yoyote ya kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia nyumbani. Ushindi dhidi ya Northern Ireland mnamo Alhamisi uliendeleza ubabe uliowashuhudia wakishinda mechi zote 10 za kufuzu kwa fainali za Euro 2021.

Kwa kuwa Uswisi walisajili ushindi wa 3-1 dhidi ya Bulgaria katika mchuano mwingine wa Kundi C, ina maana kwamba Northern Ireland kwa sasa wana ulazima wa kucharaza Bulgaria katika mechi ijayo ili kuweka hai matumaini ya kunogesha fainali za Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza tangu 1986.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Ibada yaendelea Chato kabla ya Magufuli kuzikwa baadaye leo

Scotland na Austria nguvu sawa katika mchuano wa kufuzu kwa...