• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 10:50 AM
Ibada yaendelea Chato kabla ya Magufuli kuzikwa baadaye leo

Ibada yaendelea Chato kabla ya Magufuli kuzikwa baadaye leo

Na SAMMY WAWERU

MWILI wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Joseph Magufuli umewasili katika uwanja wa Magufuli ili kupumzishwa rasmi.

Dkt Magufuli ambaye alikuwa Rais wa awamu ya tano, anazikwa leo Ijumaa nyumbani kwake Wilaya ya Chato, Mkoa wa Geita.

Juma hili, maeneo mbalimbali Tanzania wananchi walipata fursa ya kumuaga kwa kuutazama mwili wake, na pia misafara ya kikosi cha kijeshi kuuzungusha ili aliotawala kumpa heshima za mwisho.

Jeneza lenye mwili wa Rais Magufuli limewasili katika Uwanja wa Magufuli, Chato, likiwa limebebwa na maafisa wakuu wa kijeshi nchini Tanzania.

Ibada ya maziko inaendelea kwa sasa.

Aliyekuwa makamu wake, Mama Samia Suluhu Hassan na ambaye amemrithi, ameongoza Watanzania katika kumuaga.

Atazikwa kwa mujibu wa mila na itikadi za kijeshi, ambapo mizinga itafyatuliwa kumpa heshima za mwisho kama Amiri Jeshi Mkuu.

Dkt Magufuli aliaga dunia Machi 17, 2021, serikali ikitangaza “alifariki kutokana na tatizo la moyo baada ya kuugua kwa muda mrefu”.

Hata hivyo, kwa mujibu wa tetesi ambazo hazikuthibitishwa, wakosoaji wake walidai Dkt Magufuli alifariki kutokana na makali ya virusi vya corona.

Mwaka uliopita, 2020, Rais Magufuli alishangaza ulimwengu alipodai Tanzania “imelishinda janga la Covid-19”.

Mapema 2020 alipiga marufuku kutolewa kwa takwimu za maambukizi ya corona na pia kuchapishwa na vyombo vya habari kupitia sheria za data.

Dkt Magufuli alifariki akiwa na umri wa miaka 61. Amemwacha mjane, Mama Janeth Magufuli na watoto saba na wajukuu wasiopungua 10.

You can share this post!

Salah apongeza Harambee Stars na kupatia Muguna jezi

Italia wapepeta Northern Ireland bila jasho jingi katika...