• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 12:30 PM
SHINA LA UHAI: Chanjo: Hatari ya mgando wa damu ipo ila ni kwa watu walio na matatizo tofauti

SHINA LA UHAI: Chanjo: Hatari ya mgando wa damu ipo ila ni kwa watu walio na matatizo tofauti

Na BENSON MATHEKA

FLORA alikataa kwenda kupata chanjo ya corona kufuatia ripoti kwamba inasababisha mgando wa damu miongoni mwa matatizo mengine ya kiafya.

“Nasikia watu wanapata mgando wa damu baada ya kudungwa chanjo hiyo, mimi sitaki,” asema.

Ni hofu ambayo imekumba watu wengi ulimwenguni huku nchi kadhaa zikisitisha chanjo ya Oxford/AstraZeneca baada ya visa vya damu kuganda kuripotiwa miongoni mwa watu walio na umri wa chini ya miaka 55.

Kwa Flora, ripoti za watu kufariki baada ya damu kuganda walipodungwa chanjo ya corona zimemfanya kuogopa ikizingatiwa kuwa wataalamu wanasema kuchanjwa hakukingi mtu kikamilifu dhidi ya maambukizi.

Kile ambacho Flora na watu wengine hawafahamu ni kwamba mtu anaweza kupata mgando wa damu hata bila chanjo ya corona.

Wataalamu wa afya wanasema kwamba kuganda kwa damu sio jambo geni katika masuala ya afya na kuna njia za kuepuka hali hii huku wakisisitiza kuwa chanjo hiyo ni salama na manufaa yake yanazidi athari zake.

Wanasema kwamba tatizo la kuganda kwa damu mwilini halikuanza na chanjo ya corona. Kulingana na shirika la dawa la Muungano wa Ulaya (EMA) kati ya mamilioni ya watu waliopata chanjo hiyo ni wachache tu walioripotiwa kupata tatizo la kuganda kwa damu ambako pia hakukuhusishwa moja kwa moja na chanjo yenyewe.

Kulingana na kituo cha kuthibiti maradhi cha Amerika, kati ya watu 145 milioni ambao wamechanjwa nchini humo kuanzia Desemba 14 2020 hadi Machi 29 2021 vifo 2,509 viliripotiwa ikiwa ni asilimia 0.0017 ya watu waliopokea chanjo ya corona. Nchi hiyo inatumia chanjo za kampuni tofauti na CDC ilisema baada ya mili ya waliokufa kufanyiwa uchunguzi hakuna ushahidi uliopatikana kwamba vifo vilisababishwa na chanjo.

Kote ulimwenguni watu 649 milioni walikuwa wamepata chanjo ya corona kufikia Jumapili na idadi ya vifo ni chini ya asilimia moja.

Japo tafiti zinasema kwamba kuganda kwa damu kunaweza kusababisha madhara makubwa ikiwemo kupatwa na kiharusi na kifo, wanasisitiza kwamba kuna sababu zinazochangia hali hii kwa wanaodungwa chanjo ya corona na sio chanjo yenyewe.

Kulingana na Dkt Hamida Suleiman wa hospitali ya Pendo jijini Nairobi, kuna makundi ya watu yaliyo katika hatari ya kupata tatizo la kuganda kwa damu hata bila kudungwa chanjo ya corona ya Oxford/AstraZeneca.

“Unaweza kupata mgando wa damu ukilazwa hospitali. Baadhi ya watu walio na corona wanaogunduliwa kuwa na mgando wa damu ni wale waliolazwa hospitalini,” asema Hamida na kuongeza kuwa hakuna kisa cha kuganda damu kilichoripotiwa nchini tangu zoezi hilo lilipoanza wiki tatu zilizopita.

Anasema watu wanaoketi kwa muda mrefu wako katika hatari ya kupata tatizo la kuganda kwa damu sawa na walio na miili minene.

“Tafiti zimeonyesha kuwa watu walio na miili minene, walio na matatizo ya moyo na kisukari wanakabiliwa na hatari ya kuganda damu hasa wasipofanya mazoezi ya kuimarisha hali yao ya afya,” aeleza.

Kulingana na wataalamu wa shirika la afya la Healthline, mtu anaweza kupunguza hatari ya kuganda kwa damu kwa kufanya mazoezi.

Kufanya mazoezi

Kutofanya mazoezi, waeleza wataalamu, kunaongeza hatari ya kupata mgando wa damu kwa hivyo mtu anafaa kuhakikisha anafanya mazoezi mara kwa mara. Ikiwa unaketi kwa muda mrefu ukifanya kazi au kusafiri, tenga wakati wa kusimama na kutembea kwa miguu angalau kwa dakika thelathini.

Kupunguza uzani

Ili kujiepusha na hatari ya kupata tatizo la mgando wa damu mtu anafaa kupunguza uzani.

Kulingana na wataalamu, kupunguza unene wa mwili kunapunguza kwa kiwango kikubwa hatari ya kuganda kwa damu mwilini.

Uvutaji wa sigara

Uvutaji wa sigara unaweza kuharibu mishipa ya damu na kusababisha damu kuganda.

Dawa za kupanga uzazi

Baadhi ya dawa zikiwemo za kupanda uzazi na kuthibiti kiwango cha homoni mwilini zinaweza kusababisha mgando wa damu.

Kulingana na Healthline, njia bora ya kuzuia mgando wa damu unaohusishwa na corona ni mtu kujikinga asiambukizwe virusi hivyo. Hii inaashiria kuwa huenda wale wanaopata tatizo hili baada ya kupata chanjo huwa wanajiweka katika hatari ya kuambukizwa tena kwa kulegeza kanuni za kujikinga.

Dkt Hamida anaonya kwamba watu walio na virusi, dalili za virusi au walioambukizwa virusi hawafai kupata chanjo kabla ya kuthibitishwa wamepona kabisa.

“Ukipata chanjo ya corona ukiwa na virusi unajiweka katika hatari zaidi. Ni muhimu kufuata ushauri na masharti ya watalaamu wa afya. Muhimu ni kufahamu kuwa chanjo ya corona haikuzuii kuambukizwa virusi hivyo. Inachofanya ni kuimarisha kinga ya mwili wako,” asema.

Watalaamu wanasema kwamba njia ya pekee ya kuepuka kuambukizwa corona ni kudumisha umbali kutoka kwa mtu hadi mwingine, kudumisha usafi kwa kunawa mikono kila wakati kwa maji yanayotiririka na sabuni, kuepuka kushika uso, mdomo, pua na macho kwa mikono michafu na kuvaa barakoa.

Watalaamu wanashauri watu wanaohisi kwamba wako katika hatari ya kupata mgando wa damu baada ya kuambukizwa corona kumuona daktari.

“Ukiambukizwa corona na uko na wasiwasi kwamba unaweza kuwa katika hatari ya kupata mgando wa damu, usisite kumuona daktari,” asema Dkt Eric Kimani wa hospitali ya Global health, Nairobi.

Mgando wa damu unaweza kutibiwa kwa dawa mradi tu daktari amethibitisha ni salama mgonjwa kuzitumia.

Kulingana na Dkt Robert Brodsky, ambaye ni mtaalamu wa damu, baadhi ya watu walioambukizwa corona wanaweza kupata mgando wa damu.

“Kwa baadhi ya watu walio na corona, tunaona ongezeko la mgando wa damu katika mapafu, miguu na kwingine,” asema na kusisitizia watu umuhimu wa kinga na mazoezi.

Hata hivyo, Brodsky anasema kwamba kuna maradhi mengine yanayohusishwa na mgando wa damu.

“Utafiti unaendelea kubaini iwapo mgando wa damu unaohusishwa na watu wanaoambukizwa corona ni wa kipekee,” asema.

Dkt Hamida asema kwamba chanjo ya corona ambayo EMA imesema inaendelea kufanyiwa utafiti zaidi inaimarisha kinga ya mwili dhidi ya virusi hivyo na hivyo ni muhimu.

You can share this post!

Mwalimu mkuu akamatwa Machakos kwa kusambaza mtihani wa...

DALILI NZURI: Maumivu na uchovu ni ishara chanjo inafanya...