• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 8:55 PM
DALILI NZURI: Maumivu na uchovu ni ishara chanjo inafanya kazi vizuri – Wataalamu

DALILI NZURI: Maumivu na uchovu ni ishara chanjo inafanya kazi vizuri – Wataalamu

Na BENSON MATHEKA

SHIRIKA la Afya Ulimwenguni (WHO) linasema kuwa chanjo ya Covid-19 ni salama na athari zake sio tofauti na chanjo nyinginezo.

Wataalamu wa shirika hilo wanasema kwamba chanjo inanuiwa kukinga mtu dhidi ya afya yake kudorora na kufariki akiambukizwa virusi hivyo.

“Unaweza kupata mabadiliko mwilini baada ya kuchanjwa ambayo ni ishara kwamba chanjo inafanya kazi mwilini na unajenga kinga,” WHO inaeleza kwenye tovuti yake.

Mabadiliko ya mwili baada ya mtu kupata chanjo, yanafanya mtu kuhisi joto na maumivu ya misuli miongoni mwa hisia nyingine.

“Hizi ni hisia za kawaida, ni ishara kwamba mwili unapokea chanjo na unajiandaa kupigana na virusi,” wanaeleza wataalamu wa WHO.

Wanasema kwamba mabadiliko hayo huondoka baada ya siku chache na yanaonyesha kuwa chanjo inafanya kazi.

Kulingana na Dkt Swami Das, mtaalamu wa maradhi ya kuambukizwa, athari za chanjo hazimaanishi kwamba haifanyi kazi au inadhuru mtu.

Kabla ya kudungwa chanjo, matabibu wanafaa kuelezea mtu mabadiliko ya mwili ambayo anaweza kupata.

Kwa chanjo ya corona, mtu huwa anapata joto, kuhisi mchovu, kuumwa na kichwa, maumivu ya misuli, kuhisi baridi na kuhara.

Ni muhimu kukumbuka kuwa mabadiliko haya huwa ya siku chache na hayawezi kumlemea mtu.

Kulingana na WHO, chanjo ya corona hutoa kinga dhidi ya virusi hivyo pekee na kwa hivyo mtu anafaa kuhakikisha anadumisha hali nzuri ya afya.

Baada ya kupatiwa chanjo, mtu anafaa kukaa katika eneo la kuchanjiwa kwa kati ya dakika 15 na 30 ili wahudumu wa afya waweze kumhudumia iwapo inaweza kumuathiri haraka.

Wataalamu wanashauri watu kuwafahamisha wahudumu wa afya wakipata matatizo ya kiafya au athari za chanjo zikidumu kwa zaidi ya siku tatu.

WHO inaondoa hofu kwamba chanjo ya corona inaweza kusababisha watu kuambukizwa virusi ikisema chanjo zote ilizoidhinisha haziwezi kufanya hivyo.

“Kumekuwa na wasiwasi kuhusu chanjo za corona zinaweza kuambukizwa watu virusi vya corona. Hakuna chanjo yoyote iliyoidhinishwa iko na virusi hai vinavyosababisha corona, hivyo, chanjo za corona haziwezi kufanya mtu kuambukizwa virusi hivyo,” WHO inasisitiza.

Baada ya kuchanjwa, linaeleza shirika hilo, mwili huchukua wiki mbili kujenga kinga thabiti dhidi ya SARS-CoV-2, virusi vinavyosababisha corona. Kwa hivyo, mtu anaweza kuambukizwa muda mfupi kabla na baada ya kuchanjwa. Hii ni kwa sababu chanjo huwa haijapata muda wa kutoa kinga.

  • Tags

You can share this post!

SHINA LA UHAI: Chanjo: Hatari ya mgando wa damu ipo ila ni...

PATA USHAURI WA DKT FLO: Nitakabili vipi ‘allergy’ ya...