JAMVI: Karata za Uhuru zinavyohatarisha Mlima Kenya kuaminiwa kisiasa

Na WANDERI KAMAU

KARATA za kisiasa za Rais Uhuru Kenyatta dhidi ya kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga, na muungano wa Okoa Kenya Alliance (OKA) zinahatarisha ukanda wa Mlima Kenya kuaminiwa kwenye mikataba ya kisiasa katika siku zijazo.

Katika siku za hivi karibuni, Rais Kenyatta amejipata kwenye njiapanda kisiasa, akijaribu kuridhisha pande hizo mbili kwamba bado anazithamini kisiasa.

Muungano wa OKA unawashirikisha kiongozi wa chama cha Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi, Kalonzo Musyoka (Wiper), Maseneta Moses Wetang’ula (Ford-Kenya) na Gideon Moi (Kanu).

Ingawa Rais Kenyatta na washirika wake wamekuwa wakisisitiza kuwa handisheki kati yake na Bw Odinga bado ni thabiti, duru zinaeleza rais anaupendelea muungano huo kuwa mrithi wake baada ya kung’atuka uongozini 2022.

Ni hali inayotajwa kuchochea baadhi ya washirika wa Bw Odinga katika ODM kumshinikiza kuanza mazungumzo kuhusu muungano wa kisiasa na Naibu Rais William Ruto.

Katika hali hiyo, wadadisi wanaonya kwamba ingawa Rais Kenyatta anacheza karata zake kama mwanasiasa, anahatarisha mustakabali wa kisiasa wa Mlima Kenya katika kuaminiwa na maeneo mengine kushirikiana kisiasa katika siku zijazo.

Wadadisi wanasema hatari iliyopo ni ukanda huo kuonekana kama “msaliti kisiasa” kwa kurejelea “usaliti” ambao baadhi ya vigogo wa wamepitia, baada ya kubuni mikataba ya kisiasa na viongozi kutoka eneo hilo.

Kando na Dkt Ruto, baadhi ya vigogo wengine ambao wamedai kusalitiwa kisiasa na ukanda huo ni Bw Odinga na Bw Musyoka.

Bw Mudavadi pia amekuwa akidai kusalitiwa na Rais Kenyatta mnamo 2012, pale rais alidai kupotoshwa na “madimoni” (nguvu za giza) kutia saini mkataba wa kisiasa kati yake na Dkt Ruto na Bw Mudavadi, ambapo yeye (Mudavadi) ndiye alitarajiwa kuwania urais.

“Ni lazima Rais Kenyatta acheze karata zake vizuri, ili kutoendeleza dhana ya wenyeji wa Mlimani kuonekana kama wabinafsi na wasioaminika kisiasa. Ni hali ambayo huenda ikazua ghadhabu miongoni mwa maeneo mengine na kubuni muungano wa kulitenga,” asema Bw Wycliffe Muga, ambaye ni mdadisi wa siasa.

Dhana ya “usaliti” dhidi ya eneo hilo ilijengeka tangu 2003, baada ya Rais Mstaafu Mwai Kibaki na washirika wake kukataa pendekezo la uwepo wa Waziri Mkuu mwenye mamlaka, nafasi ambayo ilitarajiwa kuchukuliwa na Bw Odinga.

Hili linafuatia mkataba wa kisiasa uliobuniwa kati ya Bw Kibaki na Bw Odinga, maarufu kama ‘MoU’ walipobuni muungano wa Narc mnamo 2002, ambao uliibuka mshindi kwenye uchaguzi mkuu wa urais mwaka huo.

Tangu wakati huo, Bw Odinga amekuwa akiwalaumu washirika wa Bw Kibaki kwa “kumpotosha” kwani alikiuka makubaliano hayo licha ya kumfanyia kampeni chini ya kaulimbiu ya ‘Kibaki Tosha.’

‘Usaliti’ mwingine unaohusishwa na ukanda huo ni hatua ya Bw Kibaki kudinda kumuunga mkono Bw Musyoka kuwania urais 2013, licha ya kuhudumu kama makamu wa rais wa Bw Kibaki kati ya 2008 na 2013.

Kwenye wasifu wake ‘Against All Odds’ (Dhidi ya Changamoto Zote), Bw Musyoka anadai Bw Kibaki alikuwa ameahidi kumuunga mkono kuwa mrithi wake, baada ya kuongoza kampeni kali kuirai jamii ya kimataifa kutounga mkono hatua ya Mahakama ya Kimataifa kuhusu Uhalifu (ICC) kuwafungulia mashtaka Rais Kenyatta na Dkt Ruto kutokana na ghasia zilizotokea baada ya uchaguzi tata wa 2007.

“Nilihudumu kama makamu wa rais wa Bw Kibaki kwa uaminifu mkubwa. Nilimwokoa kisiasa aliponihitaji, baada ya kukubali hatua yake kuniteua katika nafasi hiyo baada ya tandabelua iliyotokea baada ya uchaguzi mkuu wa 2007. Nilitekeleza majukumu yote aliyonipa, ikiwa ni pamoja na kuongoza harakati za kidiplomasia kuirai jamii ya kimataifa kuiunga mkono Kenya kwenye juhudi zake kujitoa katika Mkataba wa Roma, unaoiunda ICC,” akasema Bw Musyoka.

Alisema alishangazwa na Bw Kibaki, alipobadilisha uamuzi wake ghafla na kuamua kutomuunga mkono mwanaiaji yeyote.

Usaliti wa tatu unamhusisha Dkt Ruto kutengwa na Rais Kenyatta, licha yao kuchaguliwa pamoja, baada ya kuibuka washindi kwenye chaguzi za 2013 na 2017.

Dkt Ruto amekuwa akiwalaumu washirika wa karibu wa Rais Kenyatta, hasa kutoka ukanda huo kwa kuendesha njama za kumtenga kisiasa na hatimaye kumwondoa serikalini.

Kutokana na mwelekeo huo, wadadisi wanaonya kwamba kwa kuanza kuonekana “kumchezea shere” Bw Odinga kisiasa, Rais anahatarisha nafasi ya Mlima Kwenya kwenye mikataba ya kisiasa katika siku zijazo.

“Lazima Rais Kenyatta afahamu kwamba tayari, kuna dhana ambayo ishajengeka kwamba eneo hilo haliwezi kuaminika kisiasa. Anapoendelea kuandaa mchakato wa urithi wake, anapaswa kufahamu mienendo yake inafuatiliwa kwa karibu sana,” asema Bw Mark Bichachi, ambaye ni mdadisi wa siasa.

Kulingana naye, mwelekeo wa Rais Kenyatta unapaswa kufuta dhana hiyo, badala ya kuiendeleza, ili kutoa nafasi kwa wenyeji na viongozi wake kushirikishwa kwenye miungano ijayo.

Anasema kuna hatari mwenendo wake ukachochea wanasiasa wanaohisi kusalitiwa kama Dkt Ruto, Bw Odinga, Bw Mudavadi na Bw Musyoka kuungana na kubuni muungano wa kisiasa kwa lengo la “kutoa funzo” wa wale waliowasaliti.

“Chini ya mazingira hayo, wenyeji ndio watateseka. Hivyo, ni muhimu atahadhari sana,” anaonya.

Habari zinazohusiana na hii