WANDERI KAMAU: Uchaguzi ujao utumiwe kulainisha siasa zetu

Na WANDERI KAMAU

KILA uchaguzi mkuu unapokaribia nchini, imekuwa kawaida kwa wanasiasa kubuni miungano ya kisiasa huku wakitoa ahadi za kila aina kwa wananchi.

Ni mtindo ambao umekuwa ukishuhudiwa nchini tangu miaka ya tisini, wakati mfumo wa vyama vingi vya kisiasa ulipoanza.

Wanasiasa hujigeuza malaika. Waliokuwa wasaliti hugeuka kuwa watetezi wa wananchi, waliotorokea mijini hurejea mashinani huku wengine wakianza ‘miradi’ ya ‘kuwasaidia’ wananchi kama vile barabara, mashindano ya michezo kwa vijana, michango kwa vyama vya akina mama, kufadhili ujenzi wa madarasa kati ya mikakati mingine.

Kijumla, kampeni za uchaguzi huwa kama mikutano ya mahubiri; mapasta wakiwahubiria washirika wao kuhusu namna Mungu atawafanyia miujiza na kugeuza maisha yao.

Hata hivyo, mkasa wa mtindo huu ni kuwa umeendelea kuwageuza wananchi mateka wa wanasiasa.

Wanasiasa hutumia ushawishi wao kuwafanya wananchi maskini kimakusudi, ili kuhakikisha wanazingatia kila kauli wanazotoa nyakati za uchaguzi zinapokaribia.

Chini ya upofu huo, wananchi huwa hawaoni maovu yoyote yanayoendelea.

Wachochezi husifiwa kama wakombozi, wauaji kama mashujaa, wezi kama wakarimu na wadanganyifu kama wasema kweli.

Mwelekeo huo umefuta msingi wa kisiasa uliowekwa mnamo 1992, baada ya marehemu Daniel Moi kubadilisha Kipengele 2 (a) cha Katiba, ambacho awali kiliruhusu Kanu pekee kuwa chama kisiasa nchini.

Baada ya mageuzi hayo, ilitarajiwa kwamba vyama vya kisiasa vilivyobuniwa vingekuwa vyenye falsafa na misimamo pevu.

Matarajio mengine ni kuwa mazingira ya kisiasa nchini yangegeuka na kufanana na yale yaliyo katika mataifa ya Amerika ama Uingereza, ambapo vyama hushindana kwa misingi ya sera na ajenda za kuwasaidia wananchi.

Nchini Amerika, ushindani mkuu huwa kati ya vyama vya Republican na Democratic, hali ambayo imeweka uthabiti mkubwa nchini humo tangu lilipojipatia uhuru mnamo 1776 kutoka kwa Uingereza.

Katika mazingira hayo, huwa ni rahisi sana kutabiri mwelekeo wa kisiasa nchini humo kila baada ya miaka minne, uchaguzi mkuu unapofanyika. Nchini Uingereza, ushindani mkuu huwa kati ya vyama vya Labour na Conservative.

Kama Amerika, ushindani huo hukitwa kwenye falsafa za chama, manifesto zake, uboreshaji wa sera zilizopo na mikakati ya kuwasaidia raia.

Chini ya taswira hizo, huwa ni rahisi sana kwa raia kufanya maamuzi ambayo yatawafaa bila kuzingatia misukumo ya wanasiasa binafsi.

Mazingira hayo huwapa wananchi nafasi ya kutathmini manifesto za vyama na misimamo yake kuhusu masuala mbalimbali yanayowaathiri kama vile ufufuzi wa uchumi, mahusiano kati ya mataifa hayo na nchi zingine ulimwenguni kati ya mengine.

Uwepo wa nidhamu kwenye siasa umezijengea nchi hizo mazingira mazuri na yanayotabirika kwa urahisi. Hili ni kinyume na Kenya!

Badala ya kujenga nidhamu, tumeruhusu mfumo wetu wa siasa kutekwa na kila aina ya waovu.

Matokeo yamekuwa ukosefu wa falfasa maalum inayoamua mwelekeo wa siasa zetu, kama ilivyo nchini Tanzania ama Afrika Kusini.

Vyama vipya hubuniwa kila baada ya uchaguzi na baadaye hutoweka. Je, ni lini tutalainisha siasa zetu? Huu ndio wakati mwafaka kuhakikisha tumejikomboa kisiasa.

akamau@ke.nationmedia.com

Habari zinazohusiana na hii

Mradi wa Uhuru 2022

Vigogo wapimana akili