• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 9:50 AM
Rigathi Gachagua adokeza mkataba wa Mlima Kenya kumuunga Dkt Ruto 2022 umeiva asilimia 85

Rigathi Gachagua adokeza mkataba wa Mlima Kenya kumuunga Dkt Ruto 2022 umeiva asilimia 85

Na MWANGI MUIRURI

MBUNGE wa Mathira Bw Rigathi Gachagua, Jumanne ametangaza kuwa mkataba wa ‘Tangatanga’ Mlima Kenya na Naibu Rais Dkt William Ruto kuhusu azma yake ya kuwania Urais 2022 kwa sasa umeafikia makubaliano ya asilimia 85.

Alisema kuwa kwa sasa wameelewana kupitia vinara wateule wa Kaunti 11 kuhusu masuala muhimu ya kiuchumi ambayo yanafaa kupewa kipaumbele iwapo Dkt Ruto ataibuka mshindi katika uchaguzi mkuu na awe rais wa tano wa nchi hii.

Alisema kuwa vinara hao ni Seneta Mithika Linturi (Meru), Seneta Kithure Kindiki (Tharaka Nithi), Mbunge Mwakilishi wa Wanawake wa Meru katika Bunge la Kitaifa Bi Beatrice Nkatha ambaye atasaidiana na Bw Linturi kisha mbunge maalum Bi Cecily Mbarire (Embu).

Wengine ni mbunge wa Kandara Bi Alice Wahome (Murang’a), Mbunge Mwakilishi wa Wanawake wa Nyandarua katika Bunge Faith Gitau akiwa sauti upande huo, mbunge wa Bahati Kimani Ngunjiri (Nakuru), Gachagua mwenyewe (Nyeri) na Seneta wa Laikipia Joseph Kinyua akiwa ndiye kusema upande huo na Mbunge wa Embakasi Kusini James Gakuya (Nairobi) huku Purity Ngirici akiwakilisha Kirinyaga. Kiambu kuna Moses Kuria ambaye ni mbunge wa Gatundu Kusini.

Bw Rigathi akiwa katika runinga ya Inooro asubuhi alisema kuwa wameafikiana kuhusu kufufua sekta za kiuchumi eneo la Mlima Kenya na kile kimebakia sasa ni kuibuka na jarida litakalojumuisha masuala hayo yote kabla ya kuwasilishwa kwa Dkt Ruto na baadaye masharti ya kupambana na janga la Covid 19 yatakapolegezwa, yawasilishwe kwa umma kupitia mikutano mikubwa ya hadhara.

“Jarida hilo litaandaliwa na jopo la wawakilishi sita wa Mlima Kenya na ambao kazi yao ni ya kukutana na wadau wote katika sekta za kiuchumi ili yale yatakayotangazwa katika mikutano hiyo yawe na uwiano wa mashauriano,” akasema.

Bw Rigathi alisema kuwa ile asilimia 15 inayobakia ni kuhusu nyadhifa ambazo Mlima Kenya watapata katika serikali inayopendekezwa ya Dkt Ruto.

“Kwa sasa hatuwezi tukajadiliana kuhusu nyadhifa kwa kuwa kuna mchakato wa BBI ambao unaendelea na ambao unapendekeza kuundwa kwa nafasi zaidi kama za Waziri Mkuu na manaibu wake wawili. Kuna pia pendekezo kuwa baadhi ya mawaziri wawe wakiteuliwa kutoka kwa safu ya wabunge waliochaguliwa hivyo basi kutushinikiza tuahirishe harakati hizo hadi tuone mwelekeo wa BBI,” akasema.

Alisema kuwa Mlima Kenya kwa sasa kumejaa mirengo ya kisiasa “ambapo kuna sisi Tangatanga, kuna Kieleweke ambao humpendekeza kiongozi wa ODM Raila Odinga awe rais wa tano, kuna wanaomsaka Seneta wa Baringo Bw Gideon Moi kuwa mwaniaji wao wa Urais na pia kukiwa na baadhi wanaopendekeza kiongozi wa ANC Bw Musalia Mudavadi.”

Bw Rigathi aliitaka mirengo hiyo yote ya kisiasa “ifanye kampeni zao kwa Amani bila ya kurushiana cheche za maneno na kujaribu kusambaratisha wengine.”

Alisema kuwa “sisi tukikutana na Dkt Ruto, wao wakutane na wanaopendekeza kisha mwishowe tutaenda kwa kura ya 2022 na wapigakura wataamua ni wapi imani yao ya kisiasa iko.”

Aliwasuta, mbunge wa Kieni Bw Kanini Kega na mwenzake wa Nyeri Mjini Bw Ngunjiri Wambugu, kwa kile alichokitaja kuwa “kujihusisha na harakati za kupinga mikutano ya ‘Tangatanga’ ilihali wao huwa wanakutana na Bw Odinga na huwa hatuwaulizi” akiwataka “wakome kuwashwa na pilipili wasiyoila.”

You can share this post!

Wakazi wa Thika kunufaika na umeme mitaani

Utafiti wakosa kutoa picha kamili ya ushirikiano kati ya...