• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 3:25 PM
Lissu ampa Suluhu masharti sita makali kabla kurejea TZ

Lissu ampa Suluhu masharti sita makali kabla kurejea TZ

Na THE CITIZEN

DODOMA, TANZANIA

ALIYEKUWA mwaniaji wa Urais na kiongozi wa upinzani Tanzania, Tundu Lissu ametoa masharti sita makali kwa serikali ya Rais Samia Suluhu yanayohusiana na usalama wa maisha yake kabla ya kurejea kutoka Ubelgiji anakoishi uhamishoni.

Lissu aliwania Urais mnamo Novemba 2020 na kubwagwa na marehemu Rais John Pombe Magufuli aliyefariki mwezi uliopita. Alitorokea usalama wake Ubelgiji, akidai alikuwa akiandamwa na vyombo vya usalama baada ya kupinga matokeo ya uchaguzi huo.

Alhamisi, Lissu ambaye ni Naibu Mwenyekiti wa Chadema alisema atarejea Tanzania iwapo serikali itamhakikishia usalama wake, kuwasamehe wafungwa wa kisiasa na pia akabidhiwe gari ambalo alinusurukia kifo baada ya kumiminiwa risasi 16 jijini Dodoma mnamo Januari 2018.

Mbunge huyo wa zamani wa Singida Mashariki pia ameitaka serikali imrejeshe fedha zote alizotumia kama gharama ya matibabu, alipwe pensheni yake kama mbunge wa zamani na kuondoa kesi zote dhidi yake mahakamani.

Hata hivyo, Msemaji wa polisi Tanzania David Misime alisema uchunguzi kuhusu kushambuliwa kwa Lissu ulikwama baada ya mwanasiasa huyo kukataa kushirikiana na polisi wala kuitikia mialiko ya kutoa mwanga zaidi kuhusu suala hilo.

“Hatuwezi kumkamata kwa sababu ndiye alikataa kushirikiana nasi. Hata hivyo, yupo huru kufika kwetu na kutoa maelezo zaidi wakati wowote utakaomfaa,” akasema Misime.

Mkuu huyo wa polisi pia alisema idara hiyo haimpendelei kiongozi yeyote na wao wanatekeleza jukumu lao la kuhakikisha kuwa amani inadumishwa Tanzania wala hawatambagua Lissu.

“Iwapo anapanga kurejea, basi anakaribishwa nchini kwa sababu idara yetu haihusiki na siasa ila sisi tunawajibikia tu amani ya raia wa Tanzania,” akaongeza.

Mwanasiasa huyo pia alishangaa kwa nini serikali iliwaondoa walinzi waliokuwa wamempa wakati wa kuwania Urais mwaka jana, akisema kuondolewa kwao kunaweka maisha yake hatarini.

“Nilikamatwa kisha nikawaachiliwa kabla ya kukimbilia usalama wangu huku Ubelgiji. Nataka nihakikishiwe usalama kwa sababu Rais Samia Suluhu anajua vyema niliyoyapitia aliponitembelea katika hospitali ya Nairobi 2018. Nataka kuwajua waliojaribu kuniua na mikakati ya kiusalama iliyowekwa kunikaribisha nyumbani. Kesi zote dhidi yangu zitaendelea? Na nitaruhusiwa kushiriki katika siasa?’’ akahoji Lissu.

Spika wa Bunge la Kitaifa Job Ndugai naye hakupatikana ili atoe kauli yake kuhusu suala hilo japo amewahi kunukuliwa hadharani akisema kuwa Lissu alikuwa ameshalipwa fedha zake zote kama mbunge wa zamani.

You can share this post!

Mombasa iko katika hatari ya kufungwa, aonya Joho

KIKOLEZO: Mwaka mbichi ila mgumu ajabu