• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 3:25 PM
Mwaniaji kiti cha ubunge Juja kupandishwa kizimbani Aprili 26

Mwaniaji kiti cha ubunge Juja kupandishwa kizimbani Aprili 26

Na LAWRENCE ONGARO

MWANIAJI wa kiti cha ubunge Juja, Bw George Koimburi, alitoka mafichoni mnamo Alhamisi, baada ya kusakwa na maafisa wa upelelezi wa Juja kwa wiki tatu mfululizo.

Bw Koimburi ambaye anawania kiti hicho kwa tiketi ya chama cha People Empowerment Party (PEP), alisema alikuwa amezima simu akiendesha mikakati yake ya kampeni.

Maafisa wa upelelezi wamekuwa wakimtafuta ili ajibu madai kwamba alighushi vyeti vya elimu.

Bw Koimburi anakabiliwa na mashtaka matatu ya kughushi vyetu vya masomo.

Inadaiwa mwaka wa 1994 alifanya ujanja na kughushi cheti cha elimu ya Darasa la Nane KCPE, Nambari 2015684 na pia alipata cheti cha elimu ya Kidato cha Nne KCSE ambacho sio halali.

Baadaye pia mnamo Septemba 2011-12 aliwasilisha cheti bandia akidai alihitimu kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo na Sayansi cha Jomo Kenyatta ( JKUAT)/KENET/2011-12 c6.

Bw Koimburi atafikishwa katika mahakama ya Kiambu mbele ya hakimu mkuu Bi Patricia Gichohi, mnamo Aprili 26, 2021, kujibu mashtaka hayo.

Anawakilishwa na wakili wake Bw Omenke Andenje aliyetoa hakikisho kuwa mteja wake atafika mahakamani bila kuchelewa.

Kiti hicho cha Juja kimevutia wawaniaji wengine tisa huku wakipitia changamoto tele kupatana na wananchi mashinani katika kampeni zao kutokana na janga la Covid-19.

Wawaniaji wengine wa kiti hicho ni Bi Susan Njeri Waititu (Jubilee), Anthony Kirori (Maendeleo Chap Chap), na Kenneth Gichuma (National Liberal Party).

Wengine ni Eunice Wanjiru (The National Democrat), halafu kuna Chege Kariuki Zulu, Dkt Joseph Gichui, Karanja Gachu, na Muiga Rugara, ambapo wengi wao wanagombea kama wawaniaji wa kujitegemea.

You can share this post!

Real Madrid yaendelea na mpango wa kuasisi European Super...

GSU na KPA wako kikaangoni voliboli ya Afrika ya wanaume...