• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 5:50 AM
Miaka 10 tangu auawe na Amerika, Osama bado ana ufuasi mkubwa

Miaka 10 tangu auawe na Amerika, Osama bado ana ufuasi mkubwa

Na AFP

MWONGO mmoja tangu alipowindwa na kuuawa nchini Pakistan na vikosi maalum vya Amerika, mwasisi wa Al-Qaeda, Osama bin Laden, bado ana ushawishi mkubwa kwa wanamgambo wa kiislamu hata katika maeneo yenye michafuko ya wapiganaji wa kiislamu, ambayo imebadilika mno katika miaka kadhaa iliyopita.

Mwili wa Bin Laden ulirushwa katika Ziwa la Arabian kutoka kwenye ndege ya Amerika saa kadhaa baada ya kifo chake, ili kuzuia kuundwa kwa kituo cha hija ardhini.Hata hivyo, amesalia kuwa kielelezo na ishara kwa wanamgambo wengi wa kiislamu.

Raia huyo wa Saudi, alielewa umuhimu wa propaganda ambazo zimesaidia kudumisha taswira yake ya ukakamavu hata baada ya kifo chake.Katika video alizokuwa akirekodi, alikuwa akijitokeza na bunduki ubavuni mwake, licha ya kwamba, ilikuwa nadra kumwona akipigana moja kwa moja vitani.

‘Osama bin Laden alikuza kwa makini taswira yake kwa umma ili kuvutia wafuasi wa dhati. ‘Taswira yake – ya muumini wa dhati wa Kiislamu katika mavazi ya kitamaduni zaidi, lakini aliyekuwa na bunduki yake ya AK-47 karibu kila wakati na koti lake maalum – iliundwa kujitokeza kama kiongozi wa kiislamu wa kiroho na kijeshi,” anasema Katherine Zimmerman, mshauri wa Mradi wa Vitisho Hatari katika Taasisi ya Amerika.

Hatua hii ya kutoa taswira maalum ilifanikiwa hasa katika kuwateua makurutu wapiganaji, anasema Colin Clarke, mkurugenzi wa utafiti katika kituo cha Soufan Centre, Amerika.’

Ingawa alikosolewa wakati mwingine kwa kupenda mno vyombo vya habari, alikuwa na maarifa ya kutosha kuelewa umuhimu wa kuendeleza ujumbe wa Al-Qaeda, katika mitandao mikuu,” anasema Clarke.

Baada ya mashambulizi ya Septemba 11, 2001, dhidi ya Amerika, yaliyotekelezwa na wanamgambo wa Al-Qaeda kwa amri ya bin Laden, Magharibi ilitumia mabilioni ya pesa ikijaribu kuangamiza wanamgambo wa Kiislamu wenye itikadi kali.Lakini wanamgambo wa Kiislamu kwa sasa ni wengi zaidi kote duniani kushinda walivyokuwa miongo miwili iliyopita.

Habari za jana

Rais Joe Biden, anayepanga maadhimisho ya miaka 20 ya 9/11, kwa kutoa vikosi vya Amerika Afghanistan kufikia Septemba, hataweza kudai ushindi wowote kamili katika operesheni hiyo.

Bin Laden aliweza kubadilisha maeneo ya vita kuwa nyanja za mafunzo kwa wapiganaji wa kiislamu.Michafuko kutoka Bosnia, Chechnya hadi Somalia ilitoa nafasi nzuri kwa wanamgambo wenye itikadi kali ambao walisababisha balaa nje ya mataifa yao.

“Hakutishia tu kushambulia Magharibi, lakini alifanikiwa na aliweza kuivuta Amerika katika vita vikali vya ulipizaji kisasi nchini Afghanistan, jinsi tu alivyopanga,” anasema Clarke.

Wanamgambo wa Kiislamu walibadilika kufuatia kifo cha bin Laden, huku Al-Qaeda ikipoteza hadhi yake kama mtandao mkuu zaidi duniani wa wanamgambo wa Kiislamu, iliyotwaliwa na kundi la Islamic State , ambalo lilidhibiti maeneo ya Iraq na Syria.

Makundi hayo mawili yalishiriki falsafa ya ukatili na itikadi kali, hayakuwahi kuungana na badala yake yamegeuka kuwa mahasimu wakuu huku yakipigana nchini Syria na eneo kuu la Sahel, Afrika.

Bin Laden alifariki kabla ya mgawanyiko huo kutokea kumaanisha kuwa utawala wake miongoni mwa wanamgambo wa kiislamu, hautiwi doa na utengano uliofuata.

‘Maadamu aliuawa kabla ya 2014 utengano kati ya IS na AQ, bado anachukuliwa vyema na kundi la IS,’ anasema Aaron Zelin, mtafiti anayeendesha tovuti ya masuala ya wanamgambo wa kiislamu, inayotathmini video za wanamgambo wenye itikadi kali na matini nyinginezo. ‘Kwa njia fulani, IS inajiona kama warithi wa kweli wa njia ya Bin Laden,’ anasema Zelin, kinyume na mtangulizi wake Ayman al-Zawahiri, raia wa Misri ambaye hakufahamika mno ulimwenguni.

Kadri muda ulivyosonga, Bin Laden aligeuka kuwa simulizi tu iliyobaki na wanamgambo wachache ambao pengine walikutana naye ana kwa ana.’Kwa wengi, yeye ni habari za jana na hana maana yoyote kwa masuala ya leo,” anasema Glenn Robinson, mwandishi wa kitabu kipya kwa jina ‘Global Jihad: A Brief History.’

‘Alisawiriwa kama simba katika vyombo vya habariLakini miongoni mwa wanamgambo wa kiislamu, mikakati yake ina utata, hasa uamuzi wake wa kushambulia Amerika, ambao kwa baadhi ya wanamgambo, ulikuwa na madhara makuu.’

“Unachukuliwa pakubwa kama kosa kuu la mikakati. Mojawapo wa ushahidi huu ni kwamba ni wanamgambo wachache mno wa Kiislamu wanaofuata mikakati hiyo siku hizi na wengi hata hawajawahi kujihusisha nayo,” anafafanua Robinson.

Isitoshe, Al-Qaeda sasa ni nembo na kundi tu badala ya shirika thabiti lenye kituo cha kufanyia maamuzi.Makundi yake yanaendeleza mashambulizi katika maeneo ya Sahel, Somalia, Yemen na Syria na kwa kiasi kidogo mno Magharibi.

Uso wa Bin Laden bado huwekwa katika T-shirt, jina lake huandikwa nyuma ya magari na vinyago vyake hutumiwa wakati wa maandamano.

‘Osama bin Laden amesawiriwa kama simba katika vyombo vya habari vya kiislamu na bado hujitokeza katika propaganda,’ anasema Zimmerman.Aliashiria video ya wapiganaji wa Al-Shabaab, Somalia baada ya shambulizi Disemba iliyopita, iliyowaonyesha wakitazama video ya Bin Laden.Hii ilikuwa ‘kuweka picha iliyolenga kuonyesha uhusiano wao na uongozi wake,” anasema.

You can share this post!

IG aunda kikosi kuchunguza mauaji ya wanne

Uhuru aondoa amri ya kutoingia na kutoka kaunti tano...