• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 6:50 AM
Jumbe za msamaha, hisani zatawala Idd

Jumbe za msamaha, hisani zatawala Idd

Na WACHIRA MWANGI

MAELFU ya Waislamu kote nchini walijumuika jana kuadhimisha sherehe ya Idd al-Fitr – kukamilisha mfungo wa Ramadhan.

Jijini Mombasa, Waislamu waliongozwa na aliyekuwa Kadhi Mkuu, Sheikh Hammed Mohamed Kassim, katika uwanja wa Ronald Ngala kuadhimisha kukamilika kwa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan.

Sherehe hizo za Idd al-Fitr zilifanyika kote nchini ikiwemo Masjid Ummu Kulthum Kizingo huku Waislamu wakijumuika pamoja kufungua baada ya kufunga kwa siku 30.

Katika sherehe hizo, Waislamu hujumuika kufanya suala za pamoja, kula pamoja na kuwasaidia wasiojiweza katika jamii.Sheikh Kassim aliwahimiza Waisalam kusamehe, kuomba msamaha na hata kutafakari kuhusu matendo yao huku wakiendelea kusherehekea.

“Ninafurahia tumeweza kufika mwisho wa safari hii. Tulifunga kwa siku 30 na Allah ayajibu maombi yetu. Tunafahamu wengine tulioanzisha safari hii pamoja hawajaweza kufika mwisho,” alisema Sheikh Kassim.

Sheikh Kassim pia aliwahimiza waumini waendelee kuwasaidia kwa moyo wa upendo wale wasiojiweza katika jamii hata wanapoendelea na serehe hizo za siku tatu.

“Tuwe wenye shukrani si tu katika maneno bali pia katika matendo kwa yale yote Allah ametutendea. Tusherehekee pamoja na wasiojiweza katika jamii (Zakat al-Fitr),” alisema Sheikh Kassim.

Kadhi huyo pia aliwahimiza viongozi wa kisiasa waendelee kudumisha amani na umoja miongoni mwa Wakenya ili kujenga uchumi wa nchi badala ya kueneza chuki.

Katika hafla hiyo ya sherehe, aliwahimiza watu waombeane na kuheshimiana hasa wakati ambapo dunia inapitia hali ngumu kutokana na ugonjwa wa corona.

“Tumeshaona madhara ya ugonjwa wa corona katika uchumi wetu, maisha yetu pamoja na biashara zetu. Tunajua kuwa Allah ni mkuu na kupitia maombi, tutaliangamiza janga hili la corona,” alisema Sheikh Kassim.

Sherehe hiyo ya maombi pia ilihudhuriwa na viongozi kama vile Mbunge wa Mvita, Bw Abdulswamad Nassir na Mbunge wa Jomvu, Bw Badi Twalib ambao pia walisisitiza udumishaji wa amani na msamaha.

Mfanyabiashara wa Kaunti ya Mombasa, Bw Mohamed Said Abdalla ‘Saido’ alisema kuwa sherehe ya Idd ni kuleta watu pamoja na kusameheana.

Alisisitiza kuwa hakuna mgawanyiko kati ya Waislamu waliosherehekea Idd Fitr siku ya Alhamisi na wanaosherehekea Ijumaa.

“Wengine walimaliza Ramadhan Alhamisi na kuna wengine waliomaliza Ijumaa, hatuna chochote dhidi yao kwa kuwa sisi sote ni sawa mbele zake Allah,” alisema Bw Abdallah.

You can share this post!

Serikali yapandisha bei ya mafuta baada ya majaji kurarua...

Chama cha UGM chataka Uhuru atimuliwe kwa kukiuka katiba