• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 8:50 AM
Uvundo tele Nairobi huku NMS ikizembea

Uvundo tele Nairobi huku NMS ikizembea

Na BENSON MATHEKA

MNAMO Machi 2021 Idara ya Huduma la Jiji la Nairobi (NMS) ilisema kwamba imeweka mikakati ya kuimarisha usafi katika kaunti ndogo zote 17 za Nairobi.

Hii ni moja ya majukumu ambayo idara hiyo ilitwikwa baada ya aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Sonko kuhamisha majukumu muhimu kwa serikali kuu ikiwemo uzoaji wa taka na uimarishaji wa miundo misingi.

NMS chini ya usimamizi wa Mkurugenzi Mkuu Meja Jenerali Mohammed Badi ilianza vyema na kuahidi mnamo Januari kutumia malori 210 zaidi ya kuzoa taka kote katika jiji kuu la nchi na kitovu cha uchumi Afrika Mashariki.

Lakini juhudi ambazo shirika hilo lilianza lilipobuniwa mwaka jana na kulifanya lisifiwe zimetoweka na mitaa ya jiji imejaa rundo za taka zinazooza.

Kuanzia barabara zilizo kati kati ya jiji hadi mitaa ya makazi, taka zimetapakaa huku zikichukua zaidi ya mwezi kabla ya kuzolewa.

“Hali hapa ni mbaya sana. Sijui mara ya mwisho kuona lori au wafanyakazi wa NMS wakizoa taka ilikuwa lini,” asema Jared Onyango, mkazi wa mtaa wa Umoja, mashariki mwa jiji.

Katika barabara za jiji, wafanyabiashara na wageni wanakerwa na uvundo unaotoka kwa jaa za taka ambazo zinachukua zaidi ya wiki moja bila kuzolewa.

“Sioni haja ya kulipa kodi kwa mamlaka ikiwa hawazoi taka. Hakuna wafanyakazi wa kuziondoa au kufagia ilivyokuwa ikifanyika kabla ya NMS kutwaa usimamizi wa jiji,” asema Abel Kamau anayemiliki duka katika barabara ya Dubois jijini Nairobi.

Wakazi wanahofia kuwa huenda wakaambukizwa magonjwa kufuatia hatua ya NMS ya kuchelewa kuzoa taka.

Chini ya utawala wa Bw Sonko na mtangulizi wake, Evans Kidero, kulikuwa na mpango wa kudumisha usafi kati kati ya jiji huku wafanya kazi wakifagia barabara za kati kati ya jiji kuanzia saa tatu usiku.

“Siku hizi sioni wafanyakazi wa kaunti jinsi ilivyokuwa zamani walipokuwa wakifagia na kuzoa taka usiku,” asema mlinzi mmoja kwenye barabara ya Moi Avenue katikati ya jiji akiketi kando ya pipa lililofurika rundo la taka.

Baadhi ya barabara zimekuwa majaa ya kurundika taka zinazooza na kusababisha uvundo mkali. Mnamo Machi mwaka huu, NMS ilisema kwamba ingeongeza malori zaidi ili kufanikisha uzoaji wa taka na kuimarisha usafi katika jiji lakini kulingana na hali ilivyo kwa wakati huu, hiyo ilikuwa ahadi hewa tu.

Kwa miaka mingi uzoaji wa taka umekuwa biashara inayotumiwa kupora pesa katika serikali ya jiji la Nairobi kupitia zabuni za mamilioni ya pesa.

Alipobuni NMS mwaka jana, Rais Kenyatta alisema tatizo kubwa la Nairobi ni ufisadi na mitandao ya walaghai na kumuagiza Meja Jenerali Badi kuivunja.

“Tunashuhudia taka zisizozolewa katika baadhi ya barabara kati kati mwa jiji,” aliongeza.

Walaghai hawa husimamia usambazaji wa maji na utoaji wa leseni na kufanya utoaji wa huduma kutowezekana,” alisema Rais Kenyatta.

Licha ya jukumu la uzoaji taka kuhamishiwa NMS, hali imekuwa mbaya zaidi huku taka zikirudikana na kutapakaa kote.

Ikiwa na bajeti ya zaidi ya Sh25 bilioni na ikiwa kaunti inayokusanya kiwango cha juu cha ushuru na kwamba ilibuniwa kwa lengo la kumaliza mitandao ya wafanyabiashara wanaothibiti shughuli katika jiji, ilitarajiwa NMS ingedumisha usafi Nairobi.

Wakazi zaidi ya 4 milioni wa Nairobi hutoa zaidi ya tani 3000 za taka. Hii inamaanisha kuwa zikikosa kuzolewa kwa wiki moja, zaidi ya tani 21,000 hurundikana na kuozeana mitaani, barabarani na kuziba mitaro ya maji taka hali ambayo huwa inasababisha mafuriko wakati wa mvua.

Kulingana na NMS, lengo la kununua malori zaidi lilikuwa ni kuimarisha uzoaji wa taka kwa kuwezesha wanakandarasi kuwa wakizichukua maeneo yaliyoidhinishwa katika wadi 85 za Nairobi.

“Baadhi ya wadi ziko na idadi kubwa ya watu kuliko nyingine na kwa hivyo zinatoa taka kwa wingi na kwa hivyo zitakuwa na maeneo zaidi,” alieleza naibu mkurugenzi wa mazingira katika NMS, Maureen Njeri.

Hata hivyo, kulingana na hali ilivyo, mpango huu haukufaulu kutekelezwa.

NMS inalaumu wakazi wa kutupa taka maeneo yasiyoruhusiwa na kusababisha mirundiko inayoshuhudiwa kote katika jiji.

“Watu wanatupa taka maeneo yasiyoidhinishwa na hii imekuwa changamoto kwetu,” asema afisa mmoja wa idara ya mazingira katika NMS ambaye aliomba tusitaje jina.

“Kuna vita pia katika tenda za uzoaji taka ambayo imekuwa ikitumiwa kufyonza pesa,” asema.

Mnamo Januari, Meja Jenerali Badi alitangaza kuwa idara yake ilialika kampuni za kibinafsi kusaidia NMS katika uzoaji taka na ilikuwa ikishughulikia tenda hizo.

You can share this post!

Serikali yaonya dhidi ya fujo katika uchaguzi wa Bonchari

TAHARIRI: Serikali iwasaidie waliokwama India