• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Uingereza wakomoa Austria na kujiweka sawa kwa kampeni za Euro

Uingereza wakomoa Austria na kujiweka sawa kwa kampeni za Euro

Na MASHIRIKA

UINGEREZA waliwapiga Austria 1-0 katika mechi ya kupimana nguvu iliyowakutanisha uwanjani Riverside mnamo Juni 2, 2021.

Hata hivyo, pigo zaidi kwa kikosi hicho cha kocha Gareth Southgate ni jeraha la paja lililomweka beki Trent Alexandre-Arnold wa Liverpool katika ulazima wa kuondolewa uwanjani katika kipindi cha pili.

Uingereza walifunga bao la pekee na la ushindi katika mchuano huo kupitia fowadi chipukizi wa Arsenal, Bukayo Saka katika dakika ya 56.

Southgate aliyefichua kikosi cha wanasoka 26 atakaowategemea kwenye fainali zijazo za Euro alipanga kikosi chenye mabadiliko mengu dhidi ya Austria huku wachezaji wote waliowajibikia Manchester United, Chelsea na Manchester City kwenye fainali za Europa League na Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo 2020-21 wakiachwa nje.

Mabadiliko hayo yalichangia motisha zaidi ya Austria ambao nusura wapate mabao mawili ya mapema kupitia kwa beki wa Everton, Ben Godfrey aliyekuwa karibu kujifunga mara mbili kwa kukosa kuwasiliana vilivyo na kipa Jordan Pickford ambaye ni mwenzake kambini mwa Everton.

Hata hivyo, ushindi kwa Uingereza una maana kwamba masogora wa Southgate wameangusha wapinzani wao katika jumla ya mechi saba zilizopita za kirafiki, hii ikiwa rekodi nzuri zaidi kuwahi kujivuniwa na kikosi hicho tangu Mei 1985 na Mei 1986 chini ya kocha Sir Bobby Robson.

Alexander-Arnold, 22, ni miongoni mwa mabeki wanne wa kulia waliojumuishwa na Southgate kwenye kikosi chake cha wanasoka 26. Wengine ni Reece James wa Chelsea, Kieran Trippier wa Atletico Madrid na Kyle Walker wa Manchester City.

Austria kwa sasa wamepoteza mechi mbili mfululizo kwa mara ya kwanza tangu wazidiwe maarifa na Poland na Israel mnamo Machi 2019.

Akiwa na umri wa miaka 19, Saka kwa sasa ndiye tineja wa tatu baada ya Theo Walcott na Alex Oxlade-Chamberlain kuwahi kufungia Uingereza bao wakati akiwa mchezaji wa Arsenal.

Kiungo mvamizi Jude Bellingham naye aliweka rekodi ya kuwa mchezaji mchanga zaidi kuwahi kuvalia jezi za Uingereza akiwa na umri wa miaka 17 na siku 338 tangu Wayne Rooney afanye hivyo alipowajibishwa dhidi ya Liechtenstein mnamo Septemba 2003 akiwa na umri wa miaka 17 na siku 321.

Uingereza wanakamilisha maandalizi yao kwa ajili ya fainali za Euro mnamo Juni 6 kwa mechi ya kirafiki dhidi ya Romania kabla ya kushuka dimbani kupepetana na Croatia katika mchuano wa kwanza wa Euro mnamo Juni 13, 2021 ugani Wembley, London.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Ufaransa wapepeta Wales 3-0 kirafiki

Scotland na Uholanzi nguvu sawa kirafiki