• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 9:48 PM
Scotland na Uholanzi nguvu sawa kirafiki

Scotland na Uholanzi nguvu sawa kirafiki

Na MASHIRIKA

BAO la dakika za mwisho kutoka kwa Memphis Depay anayewaniwa pakubwa na Barcelona kutoka Olympique Lyon, lilisaidia Uholanzi kusajili sare ya 2-2 dhidi ya Scotland katika mchuano wa kirafiki mnamo Jumatano usiku nchini Ureno.

Bila huduma za wanasoka saba tegemeo waliaombukizwa virusi vya corona, Scotland wanaotiwa makali na kocha Steve Clarke walitangulia kuona lango la Uholanzi kupitia Jack Hendry katika dakika ya 10 kabla ya Depay kusawazisha mambo dakika saba baadaye.

Hata hivyo, Kevin Nisbet aliwarejesha Scotland uongozini katika dakika ya 63 kabla ya matumaini yao ya kuzamisha chombo cha Uholanzi kudidimizwa na Depay dakika moja kabla ya kipenga cha kuashiria mwisho wa mchezo kupulizwa.

Scotland walikuwa bila wanasoka John Fleck, David Marshall, Stephen O’Donnell, Nathan Patterson, Grant Hanley, John McGinn na Che Adams ambao kwa sasa wamejitenga katika kambi yao ya mazoezi nchini Uhispania kwa sababu ya corona.

Scotland kwa sasa wanajiandaa kupimana nguvu na Luxembourg mnamo Juni 6 ugenini huku Uholanzi wakichuana na Georgia.

Sare dhidi ya Uholanzi ilikomesha rekodi mbovu ya Scotland kushindwa na Uholanzi mara nne mfululizo katika mechi za awali.

Scotland wameshinda mechi moja pekee kati ya 11 zilizopita za kirafiki huku wakipoteza nane na kuambulia sare mara mbili. Kikosi hicho hakijashinda mchuano wowote kati ya mitano iliyopita ambapo kimesajili sare mara moja na kuchabangwa mara nne.

Depay amehusika moja kwa moja katika mabao 29 ambayo yamefungwa na Uholanzi katika mechi 25 zilizopita huku akifunga mara 16 na kuchangia magoli mengine 13.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Uingereza wakomoa Austria na kujiweka sawa kwa kampeni za...

LISHE: Rosti ya maini