• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 6:50 AM
‘Plan B’ ya Kenya Shujaa baada ya ziara ya Los Angeles kutibuka

‘Plan B’ ya Kenya Shujaa baada ya ziara ya Los Angeles kutibuka

NaGEOFFREY ANENE

TIMU ya taifa ya raga ya wachezaji saba kila upande ya Kenya maarufu Shujaa imejiondoa kushiriki mashindano ya mwaliko ya Quest For 7s yaliyopangiwa kufanyika Juni 25-26 mjini Los Angeles, Amerika.

Hakuna sababu maalum imetolewa na Shirikisho la Raga Kenya (KRU) kwa safari hiyo kufutiliwa mbali.

Shujaa sasa inapanga kujipima nguvu dhidi ya klabu za humu nchini.

Imevunja kambi yake ya mazoezi mnamo Juni 17 baada ya kukamilisha kipindi cha mazoezi ya asubuhi.

Kocha Innocent ‘Namcos’ Simiyu ameeleza Taifa Leo kuwa sasa vijana wake wanaelekea katika mapumziko ya juma moja.

“Tumewapa mpangilio wa mazoezi watakayoendelea nayo wakati wa likizo hiyo ambayo tutaifuatilia kama benchi ya kiufundi,” alisema Simiyu.

Alifichua kuwa mpango wao wa kwanza ulikuwa kushiriki mashindano ya Los Angeles dhidi ya Uingereza, Argentina, Korea Kusini na wenyeji Amerika. Samoa pia inatarajiwa kushiriki Quest For 7s baada ya kukamilisha kampeni yake ya kuwinda tiketi ya Olimpiki mnamo Juni 19-20 nchini Monaco.

“Katika wiki moja ama majuma mawili yajayo, tutaandaa mashindano dhidi ya klabu za humu nchini. Huu ni mpango wetu “B” kwa sababu ule wa “A” umefeli. Tumeomba klabu ziunde timu tatu ambazo zitatusaidia katika mazoezi yetu ya Olimpiki,” Simiyu alisema.

Vijana wake walishiriki mashindano ya mwaliko ya kujipiga msasa mjini Madrid nchini Uhispania mwezi Februari, mjini Dubai nchini Milki za Kiarabu mwezi Aprili na mjini Stellenbosch nchini Afrika Kusini mwezi Mei.

Timu nyingine za wanaume zilizofuzu kushiriki Olimpiki zitakazofanyika Julai 23 hadi Agosti 8 mjini Tokyo ni Japan, Fiji, Amerika, New Zealand, Afrika Kusini, Argentina, Canada, Uingereza, Australia na Korea Kusini.

Kenya Lionesses, ambayo ni ya kinadada ya Kenya, pia ilikuwa imepangiwa kusafiri hadi Los Angeles.

You can share this post!

Kipa Buffon ajiunga upya na klabu ya Parma aliyoagana nayo...

Uholanzi wacharaza Austria na kuingia 16-bora kwenye...