• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
TAHARIRI: TSC sasa iheshimu uongozi wa KNUT

TAHARIRI: TSC sasa iheshimu uongozi wa KNUT

KITENGO CHA UHARIRI

SIKU ya Jumamosi hafla muhimu sana katika tasnia ya wafanyakazi humu nchini iliandaliwa. Chama cha Kitaifa cha Walimu (Knut) kiliandaa uchaguzi.

Uchaguzi huu ulifanyika baada ya shughuli hii kukumbwa na vikwazo vingi. Awali Katibu Mkuu anayeondoka alitishia kupinga mchakato huu kortini kwani alidai ulikuwa haramu.

Hata hivyo, mnamo Ijumaa, Bw Wilson Sossion alijiuzulu na kuunga mkono kufanyika kwa uchaguzi huo.

Hatua hii ilikuwa muhimu sana kwani iliepushia chama hiki aibu ya makabiliano.

Katika uchaguzi wa Jumamosi, Collins Oyuu alichaguliwa bila kupingwa kumrithi Sossion katika nafasi ya Katibu Mkuu wa chama. Oyuu anakuwa Katibu Mkuu wa saba katika historia ya chama hiki.

Katika hotuba yake, Oyuu aliahidi kushirikiana na Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC) pamoja na serikali ili kufungua ukurasa mpya kwa walimu.

Inasikitisha kwamba chama cha Knut kilianza kupata mwingilio wa nje kuanzia mwaka wa 2019 na shughuli zake kuvurugwa iwapo si kulemazwa.

Katika kipindi hiki, uanachama wake ulipungua kutoka walimu zaidi ya laki mbili hadi walimu elfu kumi na tano pekee.

Mapato ya Knut ambayo hutokana na michango ya wanachama yaliathiriwa pakubwa. Kwa sasa Knut inapokea Sh15 milioni pekee kutoka kwa kiasi cha Sh141 milioni kila mwezi. Kulemazwa huku kwa Knut kulichangiwa na TSC kutaka kudhibiti chama hiki chenye usemi mkubwa.

Haikuwa haki kwa TSC kuingilia shughuli za Knut. Haikuwa haki kwa zaidi ya laki mbili ya walimu kuadhibiwa na kudhulumiwa na idara ya serikali kwa sababu ya msimamo mkali wa Sossion.

Vyama vya wafanyakazi vipo kuwatetea wanachama. Hatua hii ya TSC lazima ilaaniwe vikali kwani ni ukiukaji wa sheria.

Maadamu sasa Sossion hayuko madarakani, tunatumai zaidi ya laki mbili ya walimu watatendewa haki.

Nyongeza ya mishahara waliyonyimwa kama sehemu ya adhabu wapewe tena katika malimbikizi yake yote.

Serikali inapasa iheshimu haki ya wafanyakazi kuwakilishwa. Aidha, inapasa ikubali kukosolewa palipo na haja. Si haki kwa serikali kuwa katika mstari wa mbele kukiuka sheria. Hebu basi na tuwe na mwanzo mpya wa TSC.

You can share this post!

NI OGIER! Mfaransa Ogier atwaa ubingwa wa WRC Safari Rally

KAMAU: Ni kosa kuwabagua wananchi kwa misingi ya tabaka