• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 10:50 AM
Kipa Jordan Pickford wa Uingereza afikia rekodi ya jagina Iker Casillas ya kutofungwa katika mechi tano mfululizo za Euro

Kipa Jordan Pickford wa Uingereza afikia rekodi ya jagina Iker Casillas ya kutofungwa katika mechi tano mfululizo za Euro

Na MASHIRIKA

KIPA matata wa Uingereza, Jordan Pickford, 27, amefikia rekodi ya aliyekuwa mlinda-lango mahiri wa Uhispania, Iker Casillas, kwenye kampeni za kuwania taji la Euro.

Hii ni baada ya Pickford ambaye huchezea Everton kuongoza Uingereza kupiga jumla ya mechi tano mfululizo bila kufungwa bao kufikia sasa kwenye kipute cha Euro mwaka huu. Casillas aliyestaafu soka mnamo Agosti 2020 akiwa na umri wa miaka 39, aliweka rekodi hiyo mnamo 2012.

Licha ya kutoshughulishwa sana na Ukraine kwenye hatua ya robo-fainali, Pickford anajivunia kipindi kizuri kwenye Euro mwaka huu huku akitegemewa zaidi kupangua makombora mazito aliyoelekezewa na Ujerumani kwenye hatua ya 16-bora.

Nguli Casillas alikuwa sehemu muhimu ya kikosi cha Uhispania kilichotwaa Kombe la Dunia mnamo 2010 nchini Afrika Kusini na mataji mawili ya Euro mnamo 2008 na 2012 akiwa nahodha.

Mnamo 2012, hakufungwa katika mechi tano mfululizo za Euro ikiwemo fainali iliyowakutanisha na Italia ambao kwa pamoja na Uingereza, wanapigiwa upatu wa kutwaa taji la mwaka huu.

Iwapo Pickford hatafungwa na Denmark kwenye nusu-fainali ya Euro mnamo Julai 7 uwanjani Wembley, basi atakuwa kipa wa kwanza kuwahi kupiga jumla ya mechi sita mfululizo kwenye kipute hicho ambacho kimekuwepo kwa miaka 61.

Rekodi ya sasa ya Pickford ni ya pili baada ya kufikia tena rekodi ya Gordon Banks ambaye pia hakufungwa katika mechi yoyote ya makundi ya fainali za Kombe la Dunia mnamo 1966. Uingereza walitawazwa wafalme wa dunia mwaka huo.

Pickford amekuwa kipa chaguo la kwanza la Uingereza tangu 2018 baada ya kocha Gareth Southgate kumpa uhakika wa kuunga kikosi cha kwanza kwenye fainali za Kombe la Dunia.

Kichapo kutoka kwa Uingereza ndicho kinono zaidi kwa Ukraine kuwahi kupokezwa katika soka ya haiba kubwa tangu wapigwe tena 4-0 na Uhispania katika hatua ya makundi ya Kombe la Dunia mnamo 2006.

Chini ya Southgate, Uingereza walifungua kampeni za Euro kwa ushindi wa 1-0 dhidi ya Croatia kabla ya kuambulia sare tasa dhidi ya Scotland katika mechi ya pili ya Kundi D. Ushindi wa 1-0 waliosajili dhidi ya Jamhuri ya Czech katika mechi ya mwisho kundini uliwapa fursa ya kupiga Ujerumani 2-0 kwenye hatua ya mwondoano.

Ushindi dhidi ya Denmark utawakatia Uingereza tiketi ya kufuzu kwa fainali ya kipute cha haiba kubwa zaidi kwa mara ya kwanza tangu 1966 walipotawazwa wafalme wa Kombe la Dunia.

Tangu Uingereza wapigwe 2-0 na Ubelgiji kwenye gozi la Uefa Nations League mnamo Novemba 15, 2020, kikosi cha pekee ambacho kimewahi kufunga Uingereza ni Poland waliopokezwa kichapo cha 2-1 kwenye mechi ya Machi 21, 2021 ya kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia za 2022.

Hadi walipofungua kampeni za Euro dhidi ya Croatia, Uingereza walikuwa wamepiga Iceland (4-0), San Marino (5-0), Albania (2-0), Austria (1-0) na Romania (1-0). Hii ni ni mara ya kwanza katika historia kwa Uingereza kutofungwa bao katika jumla ya mechi saba zilizopita.

Southgate kwa sasa ndiye kocha wa pili kuwahi kuongoza Uingereza kufuzu kwa nusu-fainali za Uingereza Kombe la Dunia na Euro baada ya Alf Ramsey kufanya hivyo mnamo 1966 na 1968.

Huku Raheem Sterling akihusika katika mabao 22 yaliyopita ya Uingereza kwa kufunga 15 na kuchangia saba kwenye mechi 21, Kane amefunga magoli 18 na kuchangia tisa mengine kutokana na michuano 26.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Mwanariadha Mkenya ajiondoa Olimpiki kwa kukosa vipimo...

Gor Mahia yazoa Sh2 milioni na tiketi ya soka ya CAF kwa...