• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 1:13 PM
Gor Mahia yazoa Sh2 milioni na tiketi ya soka ya CAF kwa kuzima mashemeji Ingwe

Gor Mahia yazoa Sh2 milioni na tiketi ya soka ya CAF kwa kuzima mashemeji Ingwe

Na GEOFFREY ANENE

GOR Mahia wamemaliza ukame wa miaka tisa bila taji la Kombe la Rais wa Shirikisho la Soka Kenya maarufu kama Betway Cup baada ya kuzima mahasimu wa tangu jadi AFC Leopards kwa njia ya penalti 4-1 ugani Nyayo, Jumapili.

Vijana wa kocha Vaz Pinto, ambao kufuatia ushindi huo wamefuzu kushiriki Kombe la Mashirikisho la Afrika msimu 2021-2022, walionekana kidogo kuwa chini kimchezo katika muda wa kawaida wa dakika 90, lakini walionyesha ustadi katika upigaji wa penalti.

Sydney Wahongo, Kenneth Muguna, Clifton Miheso na Samuel Onyango walimwaga kipa Ezekiel Owade aliingizwa uwanjani dakika ya mwisho na kocha Patrick Aussems katika nafasi ya John Oyemba akiaminiwa kuwa anaweza kupangua penalti.

Kipa Gad Mathews alikuwa shujaa wa Gor baada ya kupangua penalti kutoka kwa nahodha wa Leopards Isaac Kipyegon pamoja na Said Tsuma, huku Peter Thiong’o akifunga penalti hiyo moja ya Ingwe. Itakumbukwa kuwa mshambuliaji wa Ingwe, Elvis Rupia alikuwa amegonga mwamba katika muda wa kawaida.

“Wakati mwingine, soka huwa katili. Tulicheza vizuri sana, lakini tukapoteza nafasi nyingi. Hatukuwa katili mbele ya goli. Hata hivyo, hakuna haja ya kutoa vijisababu kwa sababu tulicheza vizuri. Tutapumzika siku mbili ama tatu kabla ya kurejelea mazoezi ya kujiandaa kwa mechi zilizosalia za Ligi Kuu,” Mbelgiji Aussems alisema.

Pinto alisema amefurahia kuwa wamepiga Ingwe licha ya kuwa mechi hiyo ilikuwa ngumu sana. “Tulistahili kushinda, ingawa ilikuwa mechi ngumu. Sasa nafurahi kuwa tumefuzu kushiriki soka ya Afrika itakayotuwezesha kupata fedha zitakazotuwezesha kuwapa wachezaji motisha zaidi,” alisema kocha huyo Mreno kabla ya kuongeza kuwa K’Ogalo watapigania kuhifadhi ubingwa wao wa ligi.

Gor, ambayo mara ya mwisho ilikuwa imeshinda kombe ni mwaka 2012 kupitia penalti 3-0 dhidi ya Sofapaka, ilipokea tiketi ya soka ya CAF pamoja na zawadi ya Sh2 milioni. Leopards iliridhika na tuzo ya Sh1 milioni. Bidco United iliyobwaga Equity Bank 1-0 katika mechi ya kutafuta nambari tatu, ilitia mfukoni Sh750,000 nayo Equity ikaridhika na Sh500,000.

  • Tags

You can share this post!

Kipa Jordan Pickford wa Uingereza afikia rekodi ya jagina...

Mat Ryan hatua moja kutua Real Sociedad