• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 3:25 PM
Wakazi wa Lamu walia makali ya njaa, kiu

Wakazi wa Lamu walia makali ya njaa, kiu

Na KALUME KAZUNGU

ZAIDI ya wakazi 2,000 wa vijiji vya Pandanguo, Jima na Madina katika Kaunti ya Lamu wanakabiliwa na baa la njaa na uhaba wa maji.

Mzee wa kijiji cha Pandanguo, Bw Adan Golja alisema wakazi wa kijiji chake na kile jirani cha Jima wamekuwa wakitegemea kisima kimoja kupata maji kwa matumizi ya nyumbani na kimekaribia kukauka.

“Huu ni msimu wetu wa pili kupanda mahindi, pojo, maharagwe na mtama na kuondoka bila mavuno yoyote mashambani kutokana na kiangazi. Uhaba wa maji pia unakumba vijiji vyetu. Watu na mifugo wanahangaika hapa,” akasema Bw Golja.

Bi Makka Bulo alisema kina mama na watoto wamekuwa wakilazimika kusafiri mwendo mrefu kutafuta maji safi ya kunywa.

“Chakula na maji, vyote ni taabu. Serikali na wahisani wajitokeze kutusaidia. Tumechoka kusafiri zaidi ya kilomita 20 kutafuta maji na chakula,” akasema Bi Bulo.

Wakati serikali kuu ilipozindua operesheni ya usalama ya Linda Boni iliyolenga kuwafirusha magaidi wa al-Shabaab wanaoaminika kujificha ndani ya msitu wa Boni mnamo 2015, iliwaamuru Waboni kutoingia msituni ili kuvuna matunda na kurina asali mwituni.

Badala yake, serikali iliahidi kwamba ingesambazia wananchi chakula na mahitaji mengine hadi pale operesheni hiyo ingekamilika. Hadi sasa operesheni bado ipo lakini mpango huo kusambazia chakula Waboni ulisitishwa kitambo.

Msemaji wa jamii ya Waboni kijijini Pandanguo, Ali Sharuti aliiomba serikali ya kaunti kusambaza maji vijijini kupitia malori ili kusaidia wakazi kukabiliana na hali mbaya ya ukame inayokumba maeneo yao.

Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Irungu Macharia alisema serikali ya kitaifa kwa ushirikiano na kaunti na wahisani inafanya juu chini kuhakikisha wakazi wanaokumbwa na changamoto ya chakula na maji wanasaidiwa.

You can share this post!

Kisa cha Covid-19 chatishia kampeni ya wanaraga wa Afrika...

Maafisa wa polisi wako katika mazingira duni, yaboreshwe...