• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 4:40 PM
Kisa cha Covid-19 chatishia kampeni ya wanaraga wa Afrika Kusini watakaovaana na Kenya Olimpiki

Kisa cha Covid-19 chatishia kampeni ya wanaraga wa Afrika Kusini watakaovaana na Kenya Olimpiki

Na GEOFFREY ANENE

WAPINZANI wa Kenya Shujaa katika mechi za makundi za Olimpiki 2020, Afrika Kusini wanakodolea macho kubanduliwa bila kucheza mechi baada ya kusukumwa karantini kufuatia kisa cha maambukizi ya virusi vya corona katika ndege waliyosafiria hadi Japan.

Ingawa wachezaji wote 14 na maafisa wanne wa timu hiyo maarufu kama Blitzboks, hawajapatikana na virusi hivyo baada ya kuwasili Julai 14, kugunduliwa kwa abiria aliye navyo kumesababisha wote waliokuwa kwenye ndege hiyo kulazimishwa kujitenga.

Gazeti la Daily Mail linadai kuwa karantini hiyo inaweza kuendelea hadi Julai 26 na kuvuruga kabisa maandalizi ya Afrika Kusini. Kila mtu anayewasili Japan lazima awasilishe nambari ya ndege aliyotumia kusafiria na pia nambari ya kiti chake halafu anapimwa ugonjwa wa Covid-19 akiwa bado katika uwanja wa ndege.

Kiongozi wa msafara wa timu ya Afrika Kusini, hata hivyo, ametaka utulivu kambini mwa timu hiyo. “Ni hali isiyo nzuri, lakini hakuna sababu ya kuingiwa na kiwewe,” Patience Shikwambana amenukuliwa na vyombo vya habari nchini Afrika Kusini akisema.

Afrika Kusini wako Kundi C pamoja na Amerika ya kocha Mike Friday, Shujaa inayotiwa makali na Innocent Simiyu na Jamhuri ya Ireland.

Shujaa imeratibiwa kuanza kampeni yake ya Olimpiki dhidi ya Amerika kisha Afrika Kusini katika siku ya kwanza mnamo Julai 26 halafu ivaane na Ireland mnamo Julai 27. Mechi za kuorodheshwa kutoka nambari moja hadi 12 (mwisho) zitaandaliwa Julai 28.

You can share this post!

AKILIMALI: Mfumaji vikapu hodari, mtunzaji mazingira...

Wakazi wa Lamu walia makali ya njaa, kiu