• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 8:50 AM
MAKALA MAALUM: Mahangaiko tele ya kupata tiba yalazimu wanawake wa hapa kuwaendea waganga

MAKALA MAALUM: Mahangaiko tele ya kupata tiba yalazimu wanawake wa hapa kuwaendea waganga

Na MAUREEN ONGALA

KATIKA kijiji cha Balagha, Kaunti ya Kilifi, tunawakuta wanawake wameketi kwenye kikundi chini ya mwembe wakiwa wanapumzika kutokana na uchovu kwa shughuli zao za kila siku shambani mwao.

Kila mmoja alikuwa ameweka jembe na upanga wake kando yake huku wakiwa wamejaa mchanga katika sehemu tofauti za mwili, dalili kuwa walikuwa wamechoka kutokana na kazi walizokuwa wamefanya.

Huo ndio mti pekee ambao una kivuli na hewa safi shambani.

Wanawake hao wanaendelea kudondoa mboga za mchunga huku wakipiga gumzo.

Tuligundua kuwa gumzo lao lilihusu sana mashaka wanayopitia katika harakati za kutafuta matibabu katika eneo hilo. Miili yao imenyong’onyea na nyuso zao kuonekana kuchoka na kushamiri huzuni wasijue la kufanya.

Wanawake hao kutoka kijiji cha Balagha katika eneobunge ya Magarini, wanaeleza kwa uchungu kuwa hawana kituo cha afya killicho karibu na wao hulazimika kwenda kwa mwendo mrefu kutafuta huduma za kimatibabu.

Kulingana nao, zahanati ya Matolani ndicho kituo cha afya cha pekee kilicho karibu, lakini kiko umbali wa zaidi ya kilomita 15.

Akizungumza na Taifa Leo, Bi Kajeni Menza alisema kuwa kutokuwepo kwa hospitali kumewalazimu wakazi wengi wa eneo hilo kwenda kwa waganga wa kienyeji kutafuta matibabu.

“Shida yetu ni kuwa hatuna hospitali. Tunateseka sana tukiwa wagonjwa na mara nyingi inakuwa shida kwetu kusafiri zaidi ya kilomita 15 kutafuta matibabu. Kwa sababu ya tatizo hilo wengine wetu huamua kwenda kwa waganga,” akasema.

Bi Menza alisema kuwa kutoka kijiji cha Balagha hadi katika zahanati ya Matolani kunagharimu Sh500 kwa bodaboda kwa mwendo mmoja. Anaendelea kuwa wanawake wajawazito wameathirika pakubwa wanapotaka kujifungua hali inayowalazimu kutegemea wakunga wa kienyeji ambao pia hawapatikani kwa urahisi hasa wakati wa usiku. Anaeleza kuwa kuna wakunga watatu pekee ambao wanatambulika kuwahudumia wanawake katika eneo hilo.

“Wakati mwingine utampigia mkunga simu na hatakuja wakati unapojifungua, lakini atakuja asubuhi kumchukua mtoto ili kwenda kumsajili katika zahanati ya Matolani,” akasema.

Wanawake hao humlipa mkunga Sh1,000 kwa huduma zake. Watoto pia wanazidi kupitia hali ngumu hasa wanaposhikwa na ugonjwa wa ghafla.

Bi Margret Jacob, ambaye ni mmoja wa wakazi anasema kuwa idadi kubwa ya wanawake kutoka Balagha hutegemea kazi za vibarua ili kupata pesa za matumizi ikiwemo ya matibabu.

Bi Margret Jacobs akizungumza na wanahabari. Picha/ Maureen Ongala

Anasema mara kwa mara wao hulazimika kuwaomba bodaboda kuwabeba kwa deni hadi hospitalini kwa sababu ya ukosefu wa pesa.

“Wakati mwingine mtoto anakuwa mgonjwa wakati huna pesa na kwa sababu ni dharura inakubidi umrai bodaboda akupeleke hospitalini kisha utamlipa ukishalipwa baada ya kulima mashamba ya watu,” akasema.

Anaendelea kuwa wakati mwingine wagonjwa hukosa matibabu katika zahanati ya Matolani hivyo basi huwalazimu kusafiri hadi katika kituo cha afya cha Baolala ambacho kiko umbali wa takribani kilomita 35.

Wao hulipa Sh1,000 kutoka Balagha hadi Baolala. Bi Jacob anaendelea kuwa iwapo hawatapa huduma katika kituo cha afya cha Baolala, huwa wanalazimika kwenda katika hospitali ya Baricho ambayo iko mbali sana na huwalazimu kutumia zaidi ya Sh2,000 kwa usafiri.

Wakati mwingine kinamama wajawazito hupoteza uhai pamoja na mtoto wao tumboni kufuatia matatizo yanayosababishwa na uchungu wa uzazi.

Bi Elina Nyevu anaeleza masikitiko yake kuwa mbali na kuwa wanawake wajawazito na watoto wanapitia changamoto za kutafuta matibabu, wakazi wanaougua magonjwa mengine pia wanazidi kuteseka.

Anaswema wakati mwingine wauguzi hukosa kuwashughulikia na badala yake kuwaambia warudi nyumbani wasubiri kupigiwa simu.

Baada ya kukosa matibabu katika zahanati ya Matolani, Bi Nyevu hufunga safari hadi zahanati ya Baolala ambapo wauguzi humpeleka katika hospitali ya Malindi katika gari la wagonjwa.

Bw Samuel Kithi ambaye pia ni mkazi, anasema hali ya kukosa huduma bora za afya kwa wanawake na watoto inazidi kuwakera wanaume wengi katika sehemu hiyo.

“Tunapata changamoto nyingi kwa bibi zetu pamoja na jamii kwa jumla kutokana na ukosefu wa usafiri na pia mwendo mrefu ambao wanawake wajawazito hulazimishwa kwenda ili kupata huduma za afya na pia kiwango cha huduma ambazo zinatolewa katika zahanati yetu ya Matolani,” akasema.

Anaongeza kuwa wanaume hulazimishwa kupiga simu mara tu bibi zao wanapoanza kuhisi utungu wa kuzaa ili kumtayarisha daktari awe katika zahanati na kumsubiri.

“Ukienda ghafla katika zahanati waweza ukamkosa daktari wa kumhudumia bibi yako,” akasema.

Bi Josphine Ngala anaeleza kuwa hali mbovu ya barabara iliyojaa mabonde na miteremko imekuwa tatizo lignine kubwa kwa wakazi hao.

Bi Josphine Ngala asema wanawake hupata changamoto tele hasa zinazohusu huduma za afya ya uzazi. Picha/ Maureen Ongala

“Kuna ugonjwa mwingine ambao haufai mgonjwa kusafirishwa kwa pikipiki, kwa mfano mwanamke mjamzito anayeumwa na uchungu wa kuzaa na anastahili kufika hospitali kwa haraka. Ni shida wao kukaa kwenye pikipiki pia inakuwa tatizo kubwa wakati anarushwarushwa kwenye mabonde kila mara,” akasema na kuongeza kuwa hali hii huchangia matatizo zaidi.

“Inahuzunisha kwetu wazazi tukiona jinsi jamii inavyoteseka. Wanawake wengi huwa katika hatari ya kupoteza maisha wanapoenda hospitalini, wengi wao huanza kuvuja damu nyingi,” akasema.

Anaeleza kuwa mambo huendelea kuwa magumu kwa wanawake ambao hupata matatizo na kuwalazimu kwenda kujifungua katika hospitali ya Malindi, hasa kutokana na shida ya usafiri.

“Mwanamke mjamzito anapokuwa katika zahanati na awe na matatizo, itabidi asubiri kwa zaidi ya masaa matano kabla ya gari la wagonjwa kufika huku anaendelea kuteseka hapo,” akasema.

Bi Ngala alisema kuna gari moja tu la uchukuzi wa umma ambalo hutoka Balagha kuelekea mjini Malindi na matatu hiyo hutoka mapema asubuhi na kurudi jioni.

Wanapojifungua wakiwa katika hospitali, wanawake hao hulazimishwa kukesha kwenye viti wakisubiri hadi masaa ambapo matatu hiyo itatoka Mjini Malindi na kuelekea nyumbani.

“Baada ya kujifungua na kuruhusiwa kwenda nyumbani, wanawake hukosa mahali pa kulala na kuwalazimisha kukesha kwenye viti katika baridi hadi asubuhi, na pia mchana wakisubiri wakati gari litakaokuwa linarudi kijijini Balagha,” akasema.

Hata hivyo, anasema, baadhi ya wauguzi huwa na roho ya imani na kuwapa kinamama hao vitanda vya kulalia lakini watalazimika kutoka pindi tu mama mwingine atakapojifungua.

“Kwa kuwa hakuna gari, mama aliyejifungua atatalazimika kushinda tena pale hospitalini kwa sababu hawezi kutumia pikipiki,” akasema.

Kulingana na Bi Ngala, hali hiyo imewavunja moyo kinamama wengi ambao wameamua kutoenda hospitalini wanapkuwa wajawazito na hata baada ya kujifungua hawapeleki watoto wao kupata chanjo.

Anasema watu wanaoumwa na nyoka pia hupitia changamoto za kupata matibabu kwani hakuna dawa ya kuzuia sumu ya nyoka mwilini katika vituo vya afya nyanjani na wao hulazimika kusafiri hadi katika hospitali kuu ya Kilifi kupata matibabu.

  • Tags

You can share this post!

Familia yaahirisha mazishi ya Kangogo

WARUI: Walimu wakuu wanaokaidi agizo la karo wachukuliwe...