• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 5:50 AM
Serikali yakiri kudaiwa Sh16m za usalama wa baharini

Serikali yakiri kudaiwa Sh16m za usalama wa baharini

Na WINNIE ATIENO

SERIKALI imeungama kudaiwa Sh16 milioni na kampuni ya Ufaransa ambayo hutoa huduma za usalama wa baharini.

Waziri wa Kilimo, Ufugaji na Uvuvi, Bw Peter Munya Jumatano alisema Kenya imeanza kulipa deni hilo kwa kampuni hiyo ambayo hufuatilia shughuli za baharini kwa njia ya setilaiti.

Taifa Leo ilikuwa imebainisha kuwa, ukosefu wa huduma hizo ni mojawapo ya changamoto zinazoweza kutoa mwanya kwa wavuvi haramu kutoka nchi za kigeni kutumia meli kubwa kuvua samaki katika maji makuu Bahari Hindi.

Hii huwanyima riziki wavuvi wa humu nchini maeneo ya Pwani.

Kwa miezi minane sasa, serikali ilishindwa kuzuia meli haramu katika maji makuu ya Bahari Hindi kwa kukosa kulipa ada kwa kampuni hiyo.

“Hilo deni litalipwa na tutarejea kulinda bahari yetu dhidi ya uvamizi. Kuna meli zilizopewa leseni ya kuvua bahari yetu lakini kuna zengine ambazo wamekuwa wakituibia na hao ni wahalifu. Tukiwa na uwezo wa kulinda bahari yetu wavamizi hao watakoma wizi huo,” akasema.

Kando na hayo, waziri aliungama kuhusu kuwepo kwa meli za makampuni ya kigeni yaliyopewa leseni kuvua samaki katika Bahari Hindi.

Alisisitiza kuwa zilipewa leseni na vibali vyote vinavyohitajika ingawa tatizo lililopo ni malalamishi ya wavuvi wanaopata ushindani usio wa haki.

“Msijali sana kuhusu meli hizo, tunafaa kuwa na wasiwasi na meli zisizokuwa na vibali zinazoiba raslimali yetu na hawalipi kodi,” akasema akiwa Mombasa jana.

Uchunguzi wa Taifa Leo ulikuwa umebainisha kuwa, serikali iliruhusu makampuni ya kigeni kutumia meli kubwa kuvua samaki katika maji makuu baharini na hivyo basi kufanya wavuvi wanaotegemea mashua kwa kazi zao kukosa samaki.

Alikiri kumekuwa na changamoto ya kulinda bahari lakini akaahidi serikali itachukua hatua.

You can share this post!

Fowadi Erik Lamela ayoyomea Sevilla

Reggea ilizma Ajenda Nne Kuu za Rais – Ruto