• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 8:55 PM
TAHARIRI: IEBC iwezeshwe kuwasajili wengi

TAHARIRI: IEBC iwezeshwe kuwasajili wengi

KITENGO CHA UHARIRI

PENDEKEZO la Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kwamba huenda ikapunguza muda wa kusajili wapigakura wapya kutoka siku 30 hadi 15 kutokana na ukosefu wa fedha, halifai.

Kulingana na mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati, tume hiyo inahitaji jumla ya Sh40.9 bilioni ili kuiwezesha kuendesha Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9, 2022 bila kutatizika.

Bw Chebukati aliambia wahariri jijini Mombasa, Jumatatu kwamba tume hiyo inahitaji Sh14.6 bilioni zaidi kuendesha shughuli zake vyema.

Uhaba huo, kwa mujibu wa Bw Chebukati, utalazimu tume hiyo kupunguza kwa asilimia 50 idadi ya siku za kusajili wapigakura kwa wingi mwanzoni mwa mwaka 2022.

Takwimu za Sensa ya 2019 zinaonyesha kuwa vijana milioni tano waliokuwa na umri wa kati ya miaka 13 na 17 mnamo 2017, watakuwa wamehitimu kupiga kura mwaka 2022.

Jumla ya Wakenya 19.6 milioni wamesajiliwa kuwa wapigakura, kwa mujibu wa sajili iliyotumiwa katika uchaguzi wa 2017.

Katiba inaruhusu kila Mkenya aliyehitimu umri wa miaka 18 kutekeleza haki yake ya kikatiba ya kuchagua viongozi anaowapenda au kuwania wadhifa wowote.

Ilitarajiwa kwamba IEBC ingeongeza muda wa kusajili wapigakura kwa wingi kutoka siku 30 hadi siku 60 kutokana na janga la corona.

Kuongezwa kwa muda wa usajili wa wapigakura hadi siku 60 kungesaidia kupunguza misongamano katika vituo vya kujiandikisha kuwa wapigia kura.

Lakini kupunguza muda huo kunamaanisha kuwa kutakuwa na misongamano katika vituo vya usajili, hivyo kusababisha kuongezeka kwa visa vya corona humu nchini.

Aidha, kupunguzwa kwa siku za usajili kutafungia nje mamilioni ya Wakenya, haswa vijana, ambao wangependa kujisajili ili kutekeleza haki yao ya kikatiba.

IEBC itafute njia za kubana matumizi ili kupata fedha za kutosha kuendesha shughuli ya usajili wa wapigakura.

Vilevile, Bunge halina budi kuingilia kati na kuwezesha IEBC kupata Sh14.6 bilioni zinazohitajika, ili kuiwezesha kuendesha shughuli zake.

Uchaguzi unaotiliwa shaka ndicho chanzo kikuu cha vurugu ambazo zimekuwa zikishuhudiwa kila baada ya uchaguzi mkuu.

Bunge litafute mikakati ya kuhakikisha kuwa fedha hizo zinazohitajika zinapatikana.

You can share this post!

Wakili adai urafiki wa Aydin na Ruto ulifanya afurushwe

Kibarua kwa Rais Suluhu joto la kudai katiba mpya...