• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 8:55 PM
BENSON MATHEKA: Viongozi waungane, ndio, lakini wasigawanye raia

BENSON MATHEKA: Viongozi waungane, ndio, lakini wasigawanye raia

Na BENSON MATHEKA

Ikiwa umesalia mwaka mmoja kabla ya uchaguzi mkuu ambao Wakenya watachagua rais wa tano, wanasiasa wako mbioni kuunganisha vyama vyao huku baadhi wakitumia jamii na maeneo yao kujipigia debe.

Kufikia sasa, makundi kadha yameibuka. La kwanza linaongozwa na Naibu Rais William Ruto ambaye ametambua chama cha United Democratic Alliance (UDA) anachodai kinaungwa mkono na Wakenya wa matabaka ya chini.

Kundi la pili linajumuisha viongozi wa vyama Wiper ( Kalonzo Musyoka), Amani National Congress (Musalia Mudavadi), Kanu (Gideon Moi) na Ford Kenya( Moses Wetangula) chini ya muungano wa One Kenya Alliance (OKA).

Kundi la tatu linashirikisha chama cha ODM cha aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga na Jubilee cha Rais Uhuru Kenyatta ambaye anatarajiwa kustaafu siasa baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka ujao.

Kuna kundi la nne linalohusisha vyama vya kisiasa vyenye mizizi eneo la Mlima Kenya ambalo linaongozwa na kiongozi wa chama cha Narc Kenya, Martha Karua, Moses Kuria wa Chama cha Kazi na Mwangi Kiunjuri wa The Service Party of Kenya (TSP).

Mnamo Jumanne, Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi, Gavana wa Makueni Kivutha Kibwana na mwaniaji urais Mukhisa Kituyi waliashiria kuwa huenda wakaungana kabla ya uchaguzi mkuu ujao.Muturi na Kibwana pia wameeleza kuwa wanamezea mate urais kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Rais Uhuru Kenya naye yuko mbioni kuunganisha ODM na OKA ili waweze kumshinda Dkt Ruto ambaye wametofautiana kwa kipindi cha miaka minne sasa.

Ingawa ni haki ya wanasiasa kuunganisha vyama vyao, itakuwa makosa kutumia miungano yao kugawanya Wakenya kwa misingi ya kikabila au kimaeneo.

Baadhi yao wamenukuliwa wakisema, wanaungana kuhakikisha maslahi ya maeneo yao yatawakilishwa kwenye serikali ijayo. Hii ni kasumba ambayo wamekuwa wakiendeleza kila wakati uchaguzi mkuu unakaribia ili kulinda maslahi yao binafsi.

Kwa kufanya hivi huwa wanachochea chuki za kijamii, kisiasa na kieneo na kusababisha ghasia kila baada ya uchaguzi mkuu. Ni kweli kila eneo linafaa kuwakilishwa kwenye serikali lakini sio kila mwanasiasa anafaa kuwa ndani ya serikali.

Kuna njia nyingi za kuhakikisha hitaji hili limetimizwa bila kugawanya na kuchochea Wakenya kupigana. Wanasiasa wanaounda miungano wanafaa kufahamu kuwa Wakenya wana haki ya kutangamana na kuishi kwa amani kama vile wanasiasa walio na haki ya kuunda miungano lakini si kwenye jukwaa la kupalilia chuki na uhasama baina ya jamii.

You can share this post!

Raila sasa tayari kukubali reggae ikizimwa kabisa

CHARLES WASONGA: Darubini kwa Chebukati uchaguzi wa 2022...