• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 12:04 PM
Maelfu bado wapigania kuenda Saudia

Maelfu bado wapigania kuenda Saudia

Na MARY WAMBUI

LICHA ya simulizi za kuatua moyo kuhusu madhila wanayopitia Saudi Arabia, maelfu ya Wakenya wamekwama Nairobi wakilalamikia kuchelewa kupata tiketi ya ndege kwenda kufanyia kazi Uarabuni.

Muungano wa Kupigania Maslahi ya Wafanyakazi Wahamiaji Nchini (ASMAK) inakadiria kuwa idadi hiyo ni karibu watu 10,000 ambao walifuzu kutoka Mamlaka ya Kitaifa ya Mafunzo ya Kuhusu Kozi Fupi (NITA) Nairobi.

Mafunzo hayo yaliyoanzishwa mnamo 2018 hutolewa kwa wahamiaji ambao wamepata kazi Uarabuni na wako tayari kuondoka kuelekea huko.

Ingawa vyombo vya habari vimekuwa vikiripoti kuhusu ukatili ambao wafanyakazi wahamiaji hutendewa nchi za Uarabuni hasa Saudia na Lebanon, mawakala wa wafanyakazi wanaosaka ajira katika nchi hizo wamelalamika kuwa hakuna ndege za kuwawezesha wasafiri Uarabuni kwa muda wa mwezi mmoja uliopita.

Hasa, Wakenya wengi wamekuwa wakifika Uarabuni kufanya kazi za nyumba, ujakazi au nyingine za mkono. Mara nyingi wanawake huajiriwa kwa mikataba ya miaka miwili kama wajakazi huku wanaume wakihudumu kama wafanyakazi wa hoteli na wanaowaelekeza wateja au kusafisha maduka makuu.

Hata hivyo, baadhi wameishia kuuawa na kuzamisha jamaa zao kwenye lindi la ukiwa huku wengine wakiteswa na kuokolewa, wakirejea nchini mikono mitupu licha ya kuwa na matumaini ya kupata utajiri mwanzoni.

“Kuna makundi matatu ya wafanyakazi ambao wamehitimu ila bado hakuna tiketi za ndege na usafiri wao hadi Uarabuni haujafanikiwa. Tayari tulikuwa tumefanikiwa kupata vyeti vyao vya kusafiri (visa) na pia wameandaliwa kandarasi zao lakini bado hawajaripoti kazini. Hatujapata tiketi zetu za ndege na hakuna anayetueleza sababu ni nini. Kwa sasa kuna msongamano wa wafanyakazi waliofuzu na wameandaliwa mikataba ila waajiri wao wameingiwa na wasiwasi kwa sababu hakuna ndege ya kuwapeleka Saudi Arabia,” akasema Francis Nduhiu, ambaye ni mwenyekiti wa ASMAK.

Aidha Wakenya wengine ambao wamefanya kazi na kumaliza kandarasi zao nao pia wamekwama Saudia na hawawezi kurejea nchini kutokana na ukosefu wa ndege. Hii ni kwa sababu ndege ambazo zilikuwa zikiwapeleka Saudia hazijakuwa zikiendeleza safari hizo tangu Agosti.

“Tiketi za wafanyakazi hawa hununuliwa kwa nusu ya bei ya ile ya kawaida kwa sababu hizi ni ndege ambazo hutengwa kwa usafiri huo. Hata hivyo, kwa sasa tiketi zinauzwa kwa bei ya juu ambapo wafanyakazi hao wahamiaji hawawezi kumudu.”

Kila mwezi, Kenya huwatuma wafanyakazi 3,000 au zaidi ili waajiriwe kwa mikataba Saudi Arabia.

Baada ya kufuzu kwa kumaliza kozi fupi wanazofundishwa, maajenti wao huhakikisha kuwa wamepokea chanjo ya virusi vya corona na huwapa hifadhi katika vyumba vya muda ambako wao hujitenga wakisubiri safari zao.

“Kutokana na ukosefu wa tiketi za ndege na maajenti wao wanaishi nao katika vyumba vya muda, idadi yao katika vyumba hivyo inazidi kuongezeka huku polisi nao pia wakiwahangaisha. Kampuni zilizowaajiri na waajiri wengine nao wameanza kulalamika,” akasema Katibu wa ASMAK Monica Muema.

Waziri wa Leba Simon Chelugui hakupokea simu za Taifa Leo ila wiki jana alifichua kuwa Kenya imeanza mazungumzo na mataifa ya Uarabani ambako Wakenya wengi wameajiriwa kama njia ya kuhakikisha maslahi ya raia wake yanazingatiwa.

You can share this post!

Laikipia: Wabunge wawili ndani

KINYUA BIN KING’ORI: Ruto afikirie upya kuhusu kubuni...