• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 10:50 AM
JAMVI: Waiguru njiapanda katika kivumbi cha 2022

JAMVI: Waiguru njiapanda katika kivumbi cha 2022

Na WANDERI KAMAU

GAVANA Anne Waiguru wa Kirinyaga yupo kwenye njiapanda kuhusu mwelekeo wa kisiasa atakaofuata, uchaguzi mkuu wa 2022 unapokaribia.

Bi Waiguru amejipata akitapatapa kisiasa, asijue atakakoenda, kwani sasa anaonekana kuchanganyikiwa kabisa kuhusu mrengo atakaounga mkono ili kuokoa merikebu yake kwenye ulingo wa siasa.

Kwa sasa, guu moja la gavana huyo lipo katika Chama cha Jubilee (JP), anakodai anapigwa kisiasa, lingine kwa mrengo wa Naibu Rais William Ruto na la tatu katika chama cha ANC, chake Musalia Musalia Mudavadi.

Wadadisi wanasema huenda huu ukawa wakati mgumu sana kwa Bi Waiguru kufanya maamuzi muhimu yatakayoamua mustakabali wake kisiasa, la sivyo kuna hatari merikebu yake ikazama na kusahaulika kabisa.

Masaibu ya Bi Waiguru yalianza majuma machache yaliyopita, alipodai kuwa kuna “watu maarufu” katika Jubilee wanaompiga vita, ili kuvuruga ushawishi wake kisiasa katika Kaunti ya Kirinyaga na ukanda wa Mlima Kenya kwa jumla.

Bila kuwataja moja kwa moja, Bi Waiguru alidai walikuwa wakitumia ushawishi wao serikalini kumhangaisha kupitia Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC).

“Ni watu maarufu wanaolenga kufanya lolote wawezavyo kuhakikisha wamenivuruga kabisa kisiasa,” akasema.

Ingawa Bi Waiguru hajakuwa akiwataja watu hao, wadadisi wanaeleza uhasama wa gavana unatokana na ushindani wa kisiasa ambao umekuwepo kwa muda mrefu kati yake na Katibu wa Wizara ya Usalama wa Ndani, Dkt Karanja Kibicho.

“Ni wazi Dkt Kibicho ni miongoni mwa watu wanaopigiwa upatu kuwania ugavana katika kaunti hiyo 2022. Hivyo, si ajabu kwa uhasama huo kuwepo. Matamshi ya Bi Waiguru yanatokana na joto la kisiasa linalotokana na ushawishi wa Dkt Kibicho serikalini,” asema Bw Julius Mukuha, ambaye ni mdadisi wa siasa.

Wadadisi wanasema kuwa huenda Bi Waiguru akawa na kibarua kigumu kuhifadhi kiti chake, ikizingatiwa kuwa baadhi ya watu ambao wametangaza nia ya kuwania nafasi hiyo wanaonekana kuwa na ushawishi mkubwa kumliko.

Baadhi yao ni Mwakilishi wa Wanawake Wangui Ngirici, kiongozi wa Narc-Kenya, gavana wa zamani Joseph Ndathi kati ya wengine.

Wadadisi wanasema hali inayoashiria huenda Bi Waiguru ameingiwa na tumbojoto ni kauli aliyotoa majuzi, kwamba huenda akakosa kuhifadhi nafasi yake ikiwa angewania tena nafasi hiyo kwa tiketi ya Jubilee.

Aelekee wapi?

Kulingana na wadadisi wa siasa, Bi Waiguru ana kibarua kigumu sana, kwani ikiwa ataamua kujiunga na chama cha UDA, chake Dkt Ruto, huenda akakosa kupewa tiketi kwani tayari chama hicho kinaonekana kumpendelea Bi Ngirici kuwania ugavana kwa tiketi yake.

Alipofanya ziara katika ukanda wa Mlima Kenya wiki mbili zilizopita, Dkt Ruto aliwarai wenyeji wa Kirinyaga kumchagua Bi Ngirichi kama gavana wao kwa “kusimama nao katika kila hali.”

“Hali ilivyo, ni wazi kuwa Bi Ngirici ashapewa tiketi ya UDA. Hivyo, itakuwa vigumu sana kwa Bi Waiguru kupewa tiketi hiyo, hata ikiwa watashiriki kwenye shughuli ya mchujo,” asema Bw Kipkorir Mutai, ambaye ni mdadisi wa siasa.

Wadadisi wanasema hali hiyo pia inamyima nafasi Bi Waiguru kuteuliwa kama mgombea-mwenza wa Dkt Ruto kwenye uchaguzi wa 2022.

“Itakuwa vigumu sana kwa Bi Waiguru kukabidhiwa nafasi kubwa kama hiyo, ilhali kuna viongozi ambao wamekuwa wakiipigania kwa kumuunga mkono Dkt Ruto licha ya mahangaiko ya kisiasa ambayo wamekuwa wakipitia. Itakuwa vigumu sana kwake,” asema Bw Mutai.

Kauli hiyo inalingana na matamshi ya mbunge Rigathi Gachagua (Mathira), aliyesema majuzi kuwa “hawatawakubalia wageni kuchukua nafasi za ‘wenyeji’ katika UDA.”

Je, Bi Waiguru ana nafasi katika ANC?

Wadadisi wanasema ikiwa patazuka uwezekano wowote wa Bw Mudavadi kuungana na Bi Waiguru, basi Bw Mudavadi atakuwa ametia doa sifa yake kama mwanasiasa muungwana na mwadilifu.

Dalili za Bi Waiguru kujiunga na kambi ya Bw Mudavadi ziliibuka Alhamisi, wakati alipoandamana na baadhi ya washirika wa kiongozi huyo katika afisi za EACC, jijini Nairobi.

Bi Waiguru alikuwa amefika katika afisi hizo kujibu tuhuma za ufisadi zinazomkabili.

Kwenye kikao na wanahabari, mbunge Ayub Savula (Lugari), alisema kuwa watasimama kidete na Bi Waiguru kwa tuhuma hizo, huku wakiendelea kumrai kujiunga na kambi yao.

“Unapomtaka msichana, unamzungumzia polepole ili kumshawishi kujiunga nawe. Tutaendelea kuzungumza na Bi Waiguru hadi atakapokubali wito wetu,” akasema Bw Savula, ambaye ndiye Naibu Kiongozi wa ANC.

Jumanne, Bw Mudavadi pia alieleza uwezekano wa kumteua mgombea-mwenza kutoka Mlima Kenya.

Hata hivyo, wadadisi wanasema kuwa Bi Waiguru anaandamwa na kivuli cha sakata za ufisadi, hivyo litakuwa “kosa la kimkakati” kwa Bw Mudavadi kushirikiana naye.

“Bi Waiguru bado anaandamwa na zimwi la sakata la ufisadi katika Shirika la Kitaifa la Vijana (NYS). Sasa, ana tuhuma zingine ambazo zimechipuka upya. Huenda taswira yake isikubalike, hasa kwa viongozi wanaosisitiza watakabiliana na ufisadi,” asema Dkt Godfrey Sang’, ambaye ni mdadisi wa siasa.

Kijumla, ingawa wadadisi wanasema bado Bi Waiguru ana nafasi kujiunda upya kisiasa, kibarua alicho nacho ni kujisafisha na kuondoa zigo la tuhuma za ufisadi linalomwandama.

You can share this post!

Rais wa Tunisia atangaza mipango ya kugeuza Katiba

Nimekuwa nikiwania fursa ya kufungia Chelsea bao ugani...