• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 10:50 AM
Rais wa Tunisia atangaza mipango ya kugeuza Katiba

Rais wa Tunisia atangaza mipango ya kugeuza Katiba

Na AFP

TUNIS, Tunisia

RAIS wa Tunisia Kais Saied ametangaza mipango ya mageuzi ya Katiba na kuundwa kwa serikali mpya miezi michache baada yake kufuta kazi waziri mkuu na kusimamisha bunge.

Lakini wakosoaji wake wamefananisha hatua hiyo na mapinduzi ya serikali na ambayo sio halali.

Akiongea katika vituo viwili vya runinga baada ya kufanya matembezi ya jioni katika barabara za jiji kuu, Tunis, Rais Saied alisema ataunda serikali mpya “haraka iwezekanavyo”.

Alisema atafanya hivyo, baada ya kuteua watu wenye maadili na ambao wanaweza kumsaidia kuendesha masuala ya nchi hiyo kwa weledi mkubwa.

Hata hivyo, Rais Saied hakutangaza ni lini atabuni serikali hiyo japo alisisitiza kuwa “ni muhimu kubadilisha Katiba”.

Rais huyo aliyechanguliwa mnamo mwaka wa 2019, amekuwa akijinadi kama shupavu katika ufasiri wa katiba na mamlaka iliyompa.

Saied alitumia mamlaka hayo mnamo Julai 25, alipomfuta kazi Waziri Mkuu, kuzima bunge na kutwaa mamlaka yote makuu ya nchini.

Hatua hiyo ilijiri baada ya mivutano kukithiri katika bunge na hivyo kuathiri utawala.

Rais huyo pia amekuwa mstari wa mbele kuendeleza vita dhidi ya ufisadi huku akiendeleza utawala ambao wandani wake wamefasiri kuwa wa kidikteta.

Hii ni kwa sababu serikali yake imekuwa ikiwazuilia wakosoaji wake, bila kuwafungulia mashtaka.

Wengine ambao wametiwa korokoroni ni wafanyabiashara na maafisa wa idara ya mahakama.

Hatua za Rais Saied pia zimepingwa na chama cha upinzani cha Ennahdha, chenye miegemeo ya Kiislamu na ambacho kina idadi kubwa ya wabunge bungeni.

Tafsiri: CHARLES WASONGA

You can share this post!

Watoto na vijana waanza kupewa chanjo ya corona

JAMVI: Waiguru njiapanda katika kivumbi cha 2022