• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 6:55 PM
Nimekuwa nikiwania fursa ya kufungia Chelsea bao ugani Stamford Bridge tangu nikiwa na umri wa miaka 11 – Lukaku

Nimekuwa nikiwania fursa ya kufungia Chelsea bao ugani Stamford Bridge tangu nikiwa na umri wa miaka 11 – Lukaku

Na MASHIRIKA

MSHAMBULIAJI Romelu Lukaku amesema kufungia Chelsea bao uwanjani Stamford Bridge ni jambo alilokuwa akiotea tangu akiwa mtoto mdogo.

Hii ni baada ya nyota huyo raia wa Ubelgiji kutikisa nyavu za Aston Villa mara mbili na kuongoza Chelsea kusajili ushindi wa 3-0 katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Jumamosi.

Mabao hayo yalikuwa ya kwanza kwa Lukaku kuwahi kupachika wavuni akichezea Chelsea katika uwanja wao wa nyumbani. Chini ya kocha Thomas Tuchel, goli jingine la Chelsea ambao kwa sasa hawajapoteza mechi yoyote hadi sasa msimu huu, lilifumwa wavuni na Mateo Kovacic.

“Imekuwa ndoto yangu tangu nikiwa na umri wa miaka 11. Nimejituma sana kwa ajili ya ufanisi huu,” akasema Lukaku.

“Mwanzo wangu kitaaluma kambini mwa Chelsea ulikabiliwa na panda-shuka tele. Hata hivyo, nimekuwa nikiimarika kadri muda unavyosonga na kufunga kwangu kumekuwa kukibashirika kirahisi katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita. Haya yote ni kwa sababu ya tajriba na bidii,” akaongeza.

“Ingawa huu ni mwanzo bora kwetu, inatulazimu kujitahidi hata zaidi. Sote tunafahamu kwamba msimu huu utashuhudia ushidani mkali zaidi kwa kuwa vikosi vingi vitakuwa vikipigania nafasi ya kutawazwa mabingwa wa EPL,” akaeleza Lukaku.

Mchuano dhidi ya Villa ulikuwa wa 15 kwa ujumla kwa Lukaku kutandaza ugani Stamford Bridge. Ushindi huo uliwapaisha Chelsea hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa jedwali la EPL kwa alama 10 sawa na viongozi Manchester United.

Chelsea kwa sasa ndicho kikosi cha pili katika historia ya EPL kuwahi kushinda jumla ya mechi 600 kwenye kipute hicho. Man-United wameshinda michuano 690.

Maandalizi ya Villa kwa ajili ya gozi hilo dhidi ya Chelsea yalivurugwa na kutokuwepo kwa kipa chaguo la kwanza Emiliano Martinez pamoja na fowadi Emi Buendia. Wawili hao waliachwa nje ya kikosi kutokana na kanuni za karantini baada ya kuongoza Argentina kwenye michuano ya kimataifa kufuzu kwa fainali zijazo za Kombe la Dunia.

Wavamizi wa Chelsea walimshughulisha vilivyo kipa Jed Steer huku wakilazimisha kona tatu chini ya dakika 10 za kwanza za mchezo.

Licha ya Villa kumkaba zaidi Lukaku aliyegusa mpira mara chache zaidi kuliko mchezaji yeyote mwingine aliyepangwa katika kikosi cha kwanza (mara 23 chini ya kipindi cha dakika 93), Lukaku, 28, alifaulu kuweka rekodi ya kufunga Villa mabao manane kutokana na mechi sita zilizopita za EPL.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO 

You can share this post!

JAMVI: Waiguru njiapanda katika kivumbi cha 2022

Haaland afunga mabao matatu na kuongoza Dortmund...