• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 12:04 PM
Uganda yaalika Rwanda uhusiano kati yao ukidorora

Uganda yaalika Rwanda uhusiano kati yao ukidorora

Na Ivan R Mugisha, The East African

Uganda imealika Rwanda kwa mkutano wa kujadili na kuthibitisha utekelezaji wa mkataba ambao nchi hizi mbili zilitia saini 2019 kumaliza uhasama wa miaka mingi.

Barua ya mwaliko iliyotumwa na waziri wa mashauri ya kigeni wa Uganda Jenerali Jeje Odongo, ilipokelewa na mwenzake wa Rwanda, Vincent Biruta, Agosti 30, duru kutoka serikali za nchi hizo mbili zilithibitisha.

Hata hivyo, Rwanda ilikanusha kuwepo kwa mipango ya mkutano “ kwa wakati huu.” “Hakuna mkutano uliopangwa kwa sasa lakini Rwanda iko tayari kufuatilia mazungumzo kuhusu masuala yaliyotajwa. Hata hivyo, tatizo bado lipo kwa kuwa Uganda inaendelea kuteka, kukamata, kutesa na kuwafukuza raia wa Rwanda,” msemaji wa serikali ya Rwanda Yolande Makolo, aliambia The EastAfrican.

“Kama tunavyosema kila mara, hali itaimarika iwapo Uganda itakoma kusaidia makundi ya kisiasa na yenye silaha kwa Rwanda na kukoma kueneza habari za uongo kuhusu mzozo kati ya nchi zetu mbili.”

Haya yanajiri wakati ambao nchi hizi mbili zinaendelea kuzozana kuhusu madai ya ujasusi, kusaidia waasi na kutesa raia wa pande zote.

Marais wa nchi hizo hivi majuzi walirushiana lawama kwenye runinga katika kile kinachoonekana ishara kubwa ya kuvunjika tena kwa uhusiano wa kidiplomasia.

Kwenye mahojiano na runinga ya France 24 mnamo Septemba 8, Rais Yoweri Museveni wa Uganda alisema, “ Tulizungumza zamani kupitia upatanishi wa Angola. Sijaona mpaka ulifunguliwa,” alipoulizwa wakati mpaka wa nchi hizo mbili utafunguliwa.

Rais Museveni, pia alipuuza madai kwamba amekuwa akitumia mtandao wa kimataifa wa Pegasus kufanya ujasusi Rwanda.

“Sikufuatilia, lakini ni kupoteza wakati. Ujasusi wa kufanya nini? Nikitaka siri, hautajua kwa sababu siri ziko kwa akili yangu, haziko kwa vinasa sauti,” akasema.

Madai ya ujasusi yalizidi juzi wakati msomi mzaliwa wa Rwanda aliyekuwa akifunza chuo kikuu nchini Uganda alikamatwa na maafisa wa kijeshi kwa kushukiwa kufanyia Rwanda ujasusi.Mapema Septemba 5, Rais Paul Kagame alilaumu serikali ya Uganda kwa kuzoea kuteswa raua wake wanaoishi Uganda.

“Hakuna raia wa Uganda anayepata shida Rwanda lakini karibu raia wote wa Rwanda nchini Uganda wana wasiwasi. Baadhi wamejuta kutembelea Uganda huku wengine wakifanywa vilema baada ya kukamatwa na kuteswa,” alisema Kagame.

“Inaonekana vitendo hivi sasa ni sehemu ya siasa zao, sasa hawafichi ukweli huu.”Rais Kagame na Rais Museveni wamekutana mara nne tangu 2019, hasa kutatua tofauti zao chini ya upatanishi wa Angola na DRC, huku maafisa wa nchi zote mbili wakikutana mara kadhaa kutekeleza maazimio ya marais wao.

You can share this post!

Waislamu wakemea serikali kuhusu utekaji wa washukiwa wa...

Mamilioni yatakayotumiwa na serikali kwenye mbio za Kip...