• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 5:50 AM
Ukweli kuhusu chanjo za corona zilizoruhusiwa nchini

Ukweli kuhusu chanjo za corona zilizoruhusiwa nchini

NA LEONARD ONYANGO

KIASI kikubwa cha chanjo za corona huenda kikatupwa iwapo watu watakosa kujitokeza kuchanjwa ndani ya miezi mitatu ijayo.

Nyingi ya dozi za chanjo za corona zilizo humu nchini zinatarajiwa kuharibika baada ya siku 100 zijazo.Tayari Kenya imepokea jumla ya dozi 5,404,780 za chanjo za AstraZeneca, Moderna na Johnson & Johnson.

Kenya inatarajia dozi milioni 1.76 za Pfizer kutoka nchini Amerika mwezi huu, na msaada wa dozi milioni 2 wa Sinopharm kutoka China pia utafika mwanzoni mwa Oktoba.

Kufikia sasa, serikali imeidhinisha aina tano za chanjo; AstraZeneca, Pfizer, Moderna, Sinopharm na Johnson and Johnson, kutumika humu nchini kupambana na makali ya corona.Mwenyekiti wa Jopokazi la Kusimamia chanjo nchini, Dkt Willis Akhwale, anasema kuwa chanjo hizo zimesambazwa katika maeneo yote nchini na zinatolewa bila malipo.

Serikali inalenga kuongeza idadi ya wahudumu wa afya wanaotoa chanjo kutoka 800 hadi 3,000 katika juhudi za kuhakikisha kuwa Wakenya milioni 10 wanachanjwa kufikia mwishoni mwa mwaka huu.Kulingana na Katibu wa wizara ya Afya Susan Mochache, chanjo zote ni sawa hivyo hakuna haja ya watu kuchagua.

“Nawahimiza Wakenya wasichague kwani chanjo zote ni muhimu na zina uwezo wa kupunguza makali ya virusi vya corona, haswa aina ya Delta ambayo inasababisha idadi kubwa ya vifo nchini Kenya,” akasema Dkt Mochache.

Anasema, aina zote za chanjo zimeidhinishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) hivyo hakuna haja ya watu kuwa na wasiwasi.

Takwimu za wizara ya Afya zinaonyesha kuwa Nairobi inaongoza kwa asilimia 8.7 ya waliochanjwa angalau dozi ya kwanza ikifuatiwa na Nyeri (asilimia 6.3) na Uasin Gishu (asilimia 5).Kaunti ya Marsabit ndiyo ina idadi ndogo zaidi ya watu waliochanjwa angalau dozi ya kwanza kwa asilimia 0.3 ikifuatiwa na Wajir (asilimia 0.5) na Tana River (0.5).

Moderna

Chanjo ya Moderna inaweza kuhifadhiwa ndani ya jokofu kwa miezi sita kabla ya kuharibika na haifai kumulikwa na jua ili kuepuka kupoteza makali.Kenya imepokea dozi 880,000 za chanjo ya Moderna kutoka Amerika.

Chanjo hii inapoingia mwilini inasisimua kingamwili (immune system) kuzuia virusi vya corona.Moderna ni miongoni mwa chanjo kuu ambazo zimetumika kuchanja idadi kubwa zaidi ya watu nchini Amerika.

Chanjo zingine zinazotumika kwa wingi nchini humo ni Pfizer na Johnson & Johnson.Chanjo ya Moderna ina uwezo wa kupunguza makali ya virusi vya corona kwa asilimia 94, kwa mujibu wa WHO.

Matatizo ya muda mfupi unayoweza kuyapata baada ya kudungwa chanjo hiyo ni uchovu, maumivu ya kichwa na misuli, kuhisi baridi na kichefuchefu.Kulingana na Taasisi ya Kudhibiti Maradhi (CDC), idadi ya watu ambao wamethibitishwa kuhisi maumivu kwa muda mrefu baada ya kuchanjwa Moderna, ni chini ya asilimia 1.

“Wengi wa waliopata matatizo hayo, walibainika kuwa na matatizo mengineyo ya kiafya,” ikasema ripoti ya CDC iliyotoewa mwezi uliopita.

Taasisi hiyo inashauri kuwa kabla ya kuchanjwa, mtu anafaa kufichua ikiwa ana ugonjwa wa mwasho wa moyo, mimba au mpango wa kupata ujauzito, ananyonyesha au amedungwa chanjo nyingine.

“Kabla ya kuchanjwa Moderna, eleza mhudumu wa afya ikiwa una historia ya kuzimia baada ya kudungwa sindano,” inashauri ya CDC.

Ili mtu kuchukuliwa kwamba amepata chanjo ya Moderna kikamilifu ni sharti apate dozi mbili ambazo hutolewa umbali wa mwezi mmoja.Utafiti uliofanywa nchini Ubelgiji na matokeo yake kuchapishwa katika jarida la Journal of the American Medical Association (JAMA) ulibaini kuwa chanjo ya Moderna hulinda mwili kwa kipindi kirefu kuliko chanjo zingine ambazo huanza kuishiwa makali baada ya muda fulani.

AstraZeneca

Kulingana na WHO, chanjo ya AstraZeneca ina uwezo wa kukabiliana na makali kwa asilimia 63.Chanjo hii ilianza kutolewa humu nchini mnamo Machi mwaka huu.Chanjo hii huharibika baada ya miezi sita. Hiyo inamaanisha kuwa chanjo za msaada zinazoletwa humu nchini kutoka mataifa ya kigeni zimesalia na chini ya mwezi mmoja pekee ziharibike.

Athari ambazo hujitokeza muda mfupi baada ya kudungwa chanjo ya AstraZeneca ni sawa na za Moderna.Lakini mapigo ya moyo huongezeka ndani ya kipindi cha saa moja na masaa mawili kwa mtu mmoja kati ya 10 wanaopata chanjo hii.

“Baadhi ya watu pia hutapika na kuhisi maumivu katika miguu na mikono,” inasema WHO.Dozi ya pili ya chanjo hii inaweza kutolewa kati ya wiki nne na 12 baada ya dozi ya kwanza.AstraZeneca ndiyo chanjo ambayo imetolewa kwa idadi kubwa zaidi ya watu duniani, ikiwemo nchini Kenya.

Taasisi ya Kuhakiki Dawa ya Ulaya (EMA), wiki iliyopita ilisema kuwa chanjo ya AstraZeneca inaweza kusababisha tatizo ambapo kingamwili zinaanza kushambulia na kuharibu neva (nerve) za mwili (Guillain-Barre).EMA hata hivyo, ilisema kuwa tatizo hilo ni adimu mno.Kati ya chanjo milioni 592 zilizotolewa katika mataifa ya Ulaya ni visa 833 vya ‘Guillain-Barre’ vimegunduliwa.

Johnson & Johnson

Kenya ina dozi 141,600 za chanjo ya Johnson & Johnson. Kulingana na Dkt Akhwale, dozi nyingi za Johnson & Johnson zitapelekwa katika maeneo ambayo ni vigumu kuyafikia. Hii ni kwa sababu chanjo hii hutolewa mara moja tu tofauti na Moderna, AstraZeneca na nyinginezo.

Ina uwezo wa kupunguza makali ya corona kwa kati ya asilimia 52 na 82.Chanjo hii inapoingia mwilini inawezesha kingamwili kupigana na virusi vya corona.Awali, chanjo hii ilikuwa ikiharibika baada ya miezi mitatu lakini muda wake umeongezwa hadi miezi sita.Kulingana na CDC, mtu anapodungwa chanjo hii, hupatwa na maumivu ya kichwa, misuli na kichefuchefu – matatizo ambayo hudumu kwa hadi siku mbili.

Pfizer

Chanjo hii ina uwezo wa kukabili corona kwa asilimia 95. Tofauti na chanjo zinginezo ambazo zinapendekezwa kutumika kwa watu wa miaka 18 na zaidi, Pfizer inaweza kutolewa hata kwa watoto wa miaka 12.Mtu hupata ulinzi dhidi ya corona siku 12 baada ya kudungwa.

Shirika la WHO linapendekeza kuwa dozi ya pili itolewe kati ya siku 21 na 28 baada ya ile ya kwanza.Sawa na chanjo zingine, Pfizer pia ina athari za kiafya za muda mfupi baada ya kudungwa kama vile kichefuchefu, maumivu ya kichwa, kuhisi baridi kati ya mengineyo. Matatizo hayo yanaweza kudumu kwa hadi siku saba baada ya kuchanjwa.

Sinopharm

Chanjo hii ni ya dozi mbili. Dozi ya pili inatolewa baada ya siku 21. Ina uwezo wa kuzuia makali ya corona kwa asilimia 79.WHO inapendekeza kuwa mtu aliye na joto la sentigredi 38 na zaidi asidungwe chanjo hii hadi pale litakapopungua.Chanjo hii imetengenezwa nchini China.

Mataifa ya Ulaya ambayo yameidhinisha matumizi ya chanjo hii ni Austria, Cyprus, Finland, Ugiriki, Iceland, Uswisi, Uhispania, Uholanzi na Sweden.Sawa na chanjo zinginezo, Sinopharm pia ina athari ambazo hutokea baada ya kuchanjwa kama vile maumivu ya kichwa.

You can share this post!

Avokado husaidia hasa wanawake kuyeyusha mafuta tumboni...

MARY WANGARI: Kongamano la UN litumiwe kuimarisha mifumo ya...