• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:15 PM
AKILIMALI: Ndizi za kienyeji zinazopendwa kwa sukari yake

AKILIMALI: Ndizi za kienyeji zinazopendwa kwa sukari yake

Na CHARLES ONGADI

NI katika kijiji cha Kanamai, Kilifi ambako Joseph Katana Kenga anafanya kilimo chake cha mboga na matunda katika shamba lake la robo ekari.

Kati ya mboga zinazopatikana kwa wingi katika shamba hili ni Mkunde, Mnavu, Mchunga na Mchicha zinazoliwa kwa wingi na wakazi wa eneo hili.

Hata hivyo, kati ya matunda anayozalisha, ni ndizi ya kienyeji inayojulikana sana na wenyeji wa hapa kama ‘Mdundatsi.’

“Niliamua kupanda ndizi hii ya kienyeji kutokana na faida yake na inapendwa sana na wenyeji wa hapa na hata soko lake ni nzuri tofauti na zingine,” asema Katana Kenga.

Kulingana na Kenga, aina hii ya ndizi ina kimo kifupi sana na huzaa ndizi kwa wingi kwenye mkungu mmoja na kumfaidi mkulima.

Tofauti na ndizi aina nyingine ni kwamba mara tunda linapoiva hugeuka haraka na kuwa nyororo na wala haichukui kipindi kirefu ikiwa ingali ngumu.

“Punde inapokuwa tayari inahitajika kuliwa bila kuchukua muda mrefu na hasa kinachovutia wengi ni kwamba ni tamu kuliko ndizi za kawaida.”

Mdundatsi huchukua kipindi cha kati ya miezi minne hadi sita kukomaa na kuwa tayari kuliwa.

Kwa mujibu wa Katana, katika kuhakikisha Mdundatsi inakua vyema bila tatizo, inahitajika kunyunyiziwa maji kila wakati na pia kupaliliwa ili kuondoa wadudu wanaotatiza ukuaji wa mmea huu.

Inapokuwa tayari kwa mavuno, mkungu mmoja hutoa kati ya kilo 90-100 tofauti na ndizi zengine ambazo mkungu huwa na uzito wa kati ya kilo 60-80.

Soko

Kulingana na Katana, wafanyabiashara wa karibu huja kununua bidhaa hii shambani kila zinapokuwa tayari huku baadhi yao wakiwauzia wateja wao mitaani.

“Wengi wanapenda Mdundatsi hasa wanakijiji wanaonunua kwa bei ya rejareja na nimeona faida kubwa,” aongeza kusema.Kwa wafanyabiashara wa jumla, Katana anawauzia kilo moja kwa Sh40 na kupata kati ya Sh3,600 hadi Sh4,000 kwa mkungu mmoja.

Katika msimu wa mavuno Katana anaiambia Akilimali kwamba anavuna kati ya mikungu miwili hadi mitatu baada ya kipindi cha miezi miwili ama zaidi.

Katana anakiri kwamba ni nadra sana kwa ndizi hizi kukosa soko akishukuru kujengwa kwa soko kuu la Mtwapa linalovutia wateja wengi wa bidhaa hii.

Changamoto

Katika kila zuri halikosi changamoto zake na Katana anakiri kwamba anakuwa na kipindi kigumu msimu wa kiangazi.

“Wakati wa kipindi cha kiangazi Mdundatsi hauzai kikamilifu na mara nyingi huwa ninahesabu hasara,” asema Katana.

Ni katika kipindi hiki cha kiangazi ambapo wadudu waharibifu huwa ni wasumbufu kwa kuvamia mizizi wakisaka maji na vyakula vyao.

Mbali na pandashuka hizi, mara nyingi kisima chake cha maji hukauka na kumlazimisha kuingia mfukoni mwake kununua maji kunyinyizia mimea yake.

Anasema siri yake kuu katika kilimo hiki cha Mdundatsi ni kwamba wakati wa kiangazi anahakikisha amepanda kwa wingi mboga ili kukithi baadhi ya mahitaji yake muhimu shambani.

“Wakati wa kiangazi ninahakikisha nina mboga za kutosha zinazoniwezesha kuwa na pesa za kutosha hali inaporudia ya kawaida,” aongeza kusema.

Aidha, Katana anaiambia Akilimali kwamba anapanga kuongeza migomba zaidi katika shamba lake kutoka 50 aliyonayo kwa sasa hadi 100 akilenga kupanua zaidi kilimo chake.

Katana anawashauri wakulima wenzake Kaunti ya Kilifi kutolalia masikio bali wageukie kilimo cha ndizi hasa aina ya Mdundatsi ambayo mara nyingi wakulima hupuuza.

Anasema wakulima wengi hupanda migomba ya ndizi shambani mwao bila kuitilia maanani wakiwa na dhana kwamba haina faida.

You can share this post!

KINYUA BIN KING’ORI: Wanasiasa waovu hutumia njia za...

AKILIMALI: Alikuwa jamaa la kubeba mizigo; sasa ana...

T L