• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
Afisi ya Rais yatuma kikosi kufufua ujenzi wa mabwawa ya Arror na Kimwarer

Afisi ya Rais yatuma kikosi kufufua ujenzi wa mabwawa ya Arror na Kimwarer

FRED KIBOR na RICHARD MUNGUTI
Serikali imeonyesha nia ya kutimiza ahadi yake ya kufufua mradi uliokwama wa mabwawa ya Arror na Kimwarer baada ya Afisi ya Rais kutuma kikosi cha maafisa wa kiufundi kutembelea maeneo yanayopendekezwa kujengwa Kaunti ya Elgeyo Marakwet.

Jumapili, Septemba 10, 2023, serikali ilituma timu ya maafisa wakuu ikiongozwa na Katibu wa Idara ya Ustawi wa Maeneo Kame Idris Salim Dakota, mwenzake wa maji Paul Rono, Wakili Mkuu wa serikali Shadrack Mose kutembelea maeneo ya ujenzi wa mabwawa hayo.

Waliandamana na usimamizi wa Mamlaka ya Maendeleo ya Bonde la Kerio na kaunti ya Elegyo Marakwet akiwemo Gavana Wisley Rotich katika ziara hiyo.

“Tulipokea maafisa wa kiufundi waliotumwa kutoka kwa Ofisi ya Rais kwa dhamira ya kutafuta ukweli kwenye maeneo ya mabwawa ya Arror na Kimwarer. Walitembelea maeneo hayo na baadaye wakajumuika na umma huko Kipsaya Marakwet Magharibi na HZ huko Keiyo Kusini. Ningependa kumshukuru Rais William Ruto kwa ishara yake nzuri ya kuanzisha tena mchakato huo baada ya kukwama kwa muda mrefu,” alisema Gavana Rotich kwenye taarifa.

Ujenzi wa mabwawa hayo mawili ya mabilioni ulisitishwa mnamo 2019 baada ya madai ya ufisadi kuibuka huku aliyekuwa Waziri wa Fedha Henry Rotich miongoni mwa wengine akishtakiwa kwa kula njama ya kulaghai serikali Sh63 bilioni.

Haya yakijiri, Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma Jumatatu Septemba 11, 2023 aliwasilisha ombi akitaka hakimu Eunice Nyuttu anayesikiza kesi dhidi ya aliyekuwa Waziri wa Fedha Henry Rotich ya ubadhirifu wa Sh63 bilioni za ujenzi wa mabwawa hayo ya Arrow na Kimwarer, ajiondoe katika kesi hiyo akidai hatendi haki.

Hata hivyo, hakimu huyo alimwamuru kiongozi wa mashtaka Geoffrey Obiri awasilishe ombi rasmi ndipo mawakili wa washtakiwa wajibu.

Kumekuwa na maswali kuhusu mwelekeo wa kesi hiyo haswa katika uitaji wa mashahidi ambao baadhi yao wamelazimika kushurutishwa kujitokeza kiasi cha kupewa ilani ya kukamatwa iwapo watakataa kufika mahakamani.

Kisa cha punde zaidi kilikuwa wiki chache zilizopita ambapo aliyekuwa Waziri wa Kilimo Peter Munya aliamriwa kufika kutoa ushahidi kama mmoja wa wafichuzi wa wizi wa pesa hizo za mabwawa, kama inavyodaiwa.

Na alipowasilishwa kortini, wala hakuulizwa maswali na ikabidi kurejea nyumbani.

Jumatatu, Septemba 11, 2023, mahakama ililazimika kutoa ilani ya kukamatwa kwa wafanyakazi wanne wa umma ambao wameorodheshwa kama mashahidi, wakitakiwa kufika mahakamani kuulizwa maswali.

 

  • Tags

You can share this post!

Matumaini kwa wakulima serikali ikiahidi kulipa fidia baada...

Huenda nyama ya pundamilia inauzwa madukani kupitia mlango...

T L