• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 8:55 PM
Akiri kuua mkewe ‘kwenye fumanizi akizini’

Akiri kuua mkewe ‘kwenye fumanizi akizini’

NA BRIAN OCHARO

MWANAMUME amekiri kosa la mauaji ya mkewe, akidai alifanya hivyo alipomfumania akizini na mwanamume mwingine nyumbani kwao.

Mnamo Februari 26, Evans Katuti, alirudi nyumbani Chaani, Changamwe, Kaunti ya Mombasa, baada ya kutazama mechi ya fainali ya Kombe la Carabao kati ya Manchester United na Newcastle United.

Alipofika mwendo wa saa nne unusu usiku, inadaiwa alimkuta mwanamume akiwa na mkewe Anna Kambui, wakiwa nusu uchi.

Mahakama iliambiwa, Bw Katuti alipomuuliza mkewe kuhusu mwanamume huyo, mke alimjibu ni mpenzi wake.

Walibishana kisha wakaanza kupigana na katika harakati hizo, mwanamke huyo anadaiwa kumfinya mumewe sehemu zake za siri.

Mshukiwa anadaiwa kuchukua kisu na kumdunga mkewe huyo mara mbili tumboni.

Mwanamume ‘mgeni’ ambaye alikuwa akitazama makabiliano ya wawili hao, alitoroka, Katuti aliposhika kisu.

Iliripotiwa kuwa mshukiwa alifunga nyumba yake na kuabiri gari kuelekea kijijini kwao Magharibi mwa Kenya.

Hata hivyo, akiwa njiani, aliarifu ndugu zake kuhusu kilichotokea nao wakamshauri ajisalimishe kwa polisi.

Bw Katuti alijisalimisha katika kituo cha polisi cha Mtito Andei ambapo alimwarifu mkuu wa polisi kuhusu kilichotokea.
Maafisa waliwasiliana na wenzao wa Chaani ambao walienda eneo la tukio na kukakusanya ushahidi na kuondoa mwili wa marehemu.

Bw Katuti alifikishwa mbele ya Hakimu Mkuu wa Mombasa Martha Mutuku mnamo Jumatatu, ambapo alikiri kosa la kuua bila kukusudia.

Hati za mahakamani zinaonyesha mshtakiwa aliungama mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Rita Orora, akisimulia matukio ya siku hiyo.

Hakimu alimpa mshukiwa muda wa kufikiria kuhusu ombi lake kabla ya ahukumiwe.

Wakili wa serikali, Bw Alex Gituma, alikubaliana na hakimu, akisema kuwa iwapo mshtakiwa atadumisha kuwa ana hatia, atasomewa maungamo yake kabla kuhukumiwa ipasavyo. Kesi hiyo imetajwa leo, Aprili 5.

  • Tags

You can share this post!

Mama mjamzito, wanawe watatu wasombwa na mafuriko

TAHARIRI: Hujuma hii kwa ugatuzi hakika haifai

T L