• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 9:01 PM
Aling’oa mtoto macho?

Aling’oa mtoto macho?

NA WYCLIFFE NYABERI

BAADHI ya wakazi wa Kisii wanakisia kuwa huenda mtoto Sagini aling’olewa macho kwa minajili ya ushirikina.

Kijijini kwao majirani waliokataa kutajwa, walieleza Taifa Leo kuwa kitendo hicho kilitokea eneo ambako Oktoba 2021, wanawake wanne walichomwa kwa kudaiwa kumroga mtahiniwa.

Lakini jana Jumatatu polisi walisema wanafuatilia kesi ya uhalifu, ambapo mwanaume wa miaka 28 aliwaeleza kuwa mama yake mzazi aliyetorokea Nairobi huenda ndiye mshukiwa mkuu wa kisa hicho.

Kiongozi wa mashtaka wa kesi hiyo, Bw Hilary Kaino, mnamo Jumatatu alimweleza Hakimu Mkuu Mkazi wa Kisii, Bi Christine Ogweno, kuwa Alex Maina Ochogo, ambaye ni binamu wa Sagini, alimsindikiza mshukiwa mkuu alipokuwa akitoroka.

Jumatatu, Ochogo alifikishwa kortini ambapo polisi walipewa siku tano kumzuilia katika kituo cha polisi cha Rioma ambapo kesi yake itatajwa.

“Ochogo alikamatwa na polisi kwani yadaiwa alimsaidia mshukiwa huyo kupanga safari ya kuenda Nairobi. Alimsaidia kufika katika kituo cha basi kabla ya kutoweka,” Bw Kaino akamwambia Hakimu.

Kwa kuwa washukiwa wengine bado hawajapatikana, kiongozi huyo wa mashtaka aliomba siku tano hadi polisi wamalize uchunguzi wao. Ombi hilo lilikubaliwa.

Kisa cha kumng’oa mtoto huyo macho kimeibua hisia kali kutoka kwa Wakenya huku watu wengi wakiamini kuwa huenda waliomdhulumu walikuwa na sababu za kishirikina.

Lakini familia ya mtoto huyo imejitenga na kauli hizo, ikisema haina ufahamu wowote na wala haikujihusisha kivyovyote katika kitendo hicho cha kikatili.

“Mimi ni mkongwe na siwezi nikafanyia mjukuu wangu unyama huo. Watu wamesema mengi na kutuhukumu lakini tunaomba serikali ifanye kila juhudi ili ukweli ujulikane,” alisema nyanya yake Sagini, Rael Mayieka.

Kulingana na baba wa mtoto huyo, Thomas Ongaga, bibi yake aliondoka nyumbani Mei 2022.

“Alinieleza kuwa amepata kibarua katika boma la mtu na aliondoka na kuniachia watoto. Amekuwa akitutumia Sh200 na siku aliyotoweka mtoto wetu, nilikuwa nimeondoka kwenda kutoa hela zilizokuwa kwenye simu yangu ili ninunue chajio. Niliporudi, nilielezwa mtoto hayuko na baada ya kutafuta usiku kucha, hakupatikana hadi siku iliyofuatia akiwa amedhulumiwa,” Bw Ongaga akasema.

Mamaye mtoto kwa jina Maureen Nyaboke, alirejea nyumbani juzi baada ya kusikia habari kuhusu mateso aliyoyapitia mwanawe.

Alibubujikwa na machozi ya uchungu mbele ya Gavana wa Kisii, Simba Arati katika hospitali ya macho ya Kisii.

Mtoto Sagini alitoweka nyumbani Desemba 13 na kupatikana katika shamba la mahindi lililo karibu na nyumbani kwao siku iliyofuatia mwendo wa adhuhuri.

Bi Mayieka alisema mjukuu wake alitoweka baada ya kumtuma amletee maji kutoka kijito kimoja kilicho karibu ili atumie maji hayo kumfulia nguo zake.

Baada ya kupatikana kondeni, Sagini alikimbizwa katika Hospitali Ndogo ya Kaunti ya Marani ambako alipata huduma ya kwanza kabla ya kupelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kisii na baadaye Hospitali ya Macho ya Kisii kwa matibabu maalum.

Madaktari katika hospitali ya macho ya Kisii walifahamisha kuwa kijana Sagini ataendelea kuwa kipofu maisha yake yote.

Mkurugenzi wa Matibabu katika Hospitali ya Macho ya Kisii, Dkt Dan Kiage alisema kwamba walimpokea mvulana huyo Jumatano jioni na ilibidi kwanza kumsafisha majeraha yake.

“Ingawa anapata nafuu, hakuna njia ambayo ataona tena. Macho yake yote yametobolewa na kitu chenye ncha kali kama kisu. Pia tulibaini kuwa washambuliaji walijeruhi kope na kuacha uchafu hapo. Tulichofanya ni kusafisha uchafu na kutibu mifuniko na kutoa dawa za kuzuia maambukizi,” alisema Dkt Kiage.

Serikali ya Kisii inapanga kumpeleka Sagini katika kituo maalum kumhifadhi wakiwa na dada yake.

Gavana Arati alisema katika kituo hicho, mtoto huyo ataangaliwa na kupewa usaidizi wa kisaikolojia.

“Hilo ni jukumu letu. Hakuna mtu mwingine wa kufanya hilo na kwa hivyo nitalazimika kwa sababu sina chaguo lingine,” Bw Arati alisema.

Gavana huyo alitangaza kulipa bili ya hospitali ya mvulana huyo na gharama nyinginezo.

Aliishukuru Hospitali ya Macho ya Kisii kwa kumlaza mgonjwa huyo na kusema ana matumaini kuwa polisi watafanya kazi yao na kuwafichua wahusika wa kitendo hicho kiovu.

Polisi pia wamemhoji baba ya mtoto huyo wakitafuta njia za kutegua kitendawili hicho.

  • Tags

You can share this post!

Rai raia wapate chanjo ya Covid kabla ya 2023

Wandani wa Ruto waunga pendekezo afisi ya kiongozi wa...

T L