• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 1:20 PM
Mnataka kukaa msituni hadi 2032? Gachagua akejeli jamii ya Wakamba akiwarai kumuunga Ruto

Mnataka kukaa msituni hadi 2032? Gachagua akejeli jamii ya Wakamba akiwarai kumuunga Ruto

NA LABAAN SHABAAN

RAIS William Ruto na Naibu Rais Rigathi Gachagua waligeuza jukwaa la uzinduzi wa shughuli ya upanzi wa miti nchini kuwa uwanja wa siasa ambapo waliwarai wakazi wa Kaunti ya Makueni kuunga serikali mkono ufikapo uchaguzi mkuu wa 2027.

Dkt Ruto alikiri kuwa eneo la Makueni si ngome yake ya kisiasa kwa jinsi Kiongozi wa Upinzani Raila Odinga alivyo na ushawishi huko.

“Unajua hii Makueni ni pahali pagumu (yeye kupenya kisiasa). Tulijaribu na Rais Uhuru Kenyatta 2013 tukapata asilimia 4, tukajaribu tena 2017 tukapata asilimia 9. Juzi (2022) nimeng’ang’ana mpaka nimefikisha asilimia 20,” alisema.

“Mimi ninaona hapa mbele mambo yako sawa,” Rais aliongeza akijipigia debe kabla ya uchaguzi mkuu wa 2027.

Naibu Rais alikariri kauli ya Rais akidai serikali ya mrengo wa Kenya Kwanza itatawala kwa mihula miwili Dkt Ruto akiwa kiongozi wa taifa.

Bw Gachagua aliwaambia wakazi wa Makueni wamuunge Rais mkono ili wafaidi maendeleo kutoka kwa serikali.

“Unajua ukitaka moto unaomba mahali moto uko. Sasa hivi  mpaka mwaka wa 2032 mwenye maneno ni huyu (Rais William Ruto)… Sasa miaka tisa mtakaa msituni?…Si muingie hapa hiyo miaka imebaki tisa kama mnataka kutoka baadaye mtoke halafu mpate maendeleo,” alisema Naibu Rais akirejelea matakwa ya viongozi wa Makueni kuhusu maendeleo kutoka kwa serikali.

Rais na Naibu wake walijumuika na Gavana wa Makueni Mutula Kilonzo Jnr na viongozi wengine huko Kiu Wetland eneobunge la Kibwezi Magharibi kuadhimisha siku ya kupanda miti.

Hapa, Rais alizindua sikukuu ya upanzi wa miti kote nchini kulenga kukabili changamoto za mabadiliko ya hali ya anga kwa kupanda miti 15 bilioni.

  • Tags

You can share this post!

Arati alipukia kamishna akidai bodaboda ‘wafuasi wake’...

Justina Syokau asema anatafuta kijana barobaro bilionea...

T L