• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Ashtakiwa kwa madai ya kuwalaghai akina mama Sh9m

Ashtakiwa kwa madai ya kuwalaghai akina mama Sh9m

Na RICHARD MUNGUTI

MFANYABIASHARA mmoja ameshtakiwa kwa madai ya kuwapunja wanawake wawili zaidi ya Sh9 milioni akidai angewauzia dawa ya kuua wadudu na magugu katika viwanja vya michezo na maeneo ya kujenga barabara.

Oduru Phelix Narkiso Mbeya almaarufu Felix Oduor almaarufu Philip Ochieng almaarufu Jackson Omondi Ochieng anayeishi katika mtaa wa kifahari wa Karen alishtakiwa Jumatatu mbele ya hakimu mkazi wa mahakama ya Makadara Bi Evelyne Kanyiri.

Oduru alikanusha shtaka kwamba alipata Sh9,050,000 kutoka kwa Bi Damaris Kwamboka na Jackline Nzula akijifanya angewauzia Pramitol 25E.

Alidaiwa kupokea pesa hizo katika eneo la Westlands Nairobi kati ya Juni 26 , 2021 na Machi 18,2022.

Dawa hiyo ilikuwa inaagizwa na Oduor, aliyepia Mkurugenzi wa kampuni ya Kenland Hydro Solutions kutoka Misri.

Kwamboka na Nzula wanaowakilishwa na wakili Teddy Kaburu waliwasiliana na Oduru katika duka lake lililoko Bulbul,Ongata Rongai kisha akawatuma kuenda Tradal Holdings Limited iliyoko Westlands Nairobi ambapo walipewa cheti cha kununua (LPO) Pramitol 25 E.

Hatimaye walishika kiguu na njia hadi kampuni nyingine -Fashan Enterprises Limited walipoelekezwa kuuza mitungi 25 ya lita 20 waliyokuwa wameuziwa.

Kwa kila lita ya dawa hiyo walalamishi walikuwa wanauziwa Sh16,100. Mtungi wa lita 20 walalamishi waliununua kwa Sh322,000. Waliuza dawa hiyo kupitia kwa kampuni ya Fashan. Hawakulipwa na kampuni hiyo ya Tradal inayohusishwa na Oduru.

Mawakili Cedric Magotsi na Apollo Bwana waliomba mshtakiwa aachiliwe kwa dhamana.

Bw Magotsi alieleza mahakama kuwa haki za mshtakiwa zilikandamizwa kwa kufika kortini mara tano bila kushtakiwa.

Lakini kiongozi wa mashtaka Remyngtone Mwandawiro alipinga mshtakiwa aachiliwe kwa dhamana akidai amejaribu kuvuruga uchunguzi.

Bi Kanyiri alimwachilia kwa dhamana ya Sh4.5 milioni na kutenga kesi isikilizwe Novemba 3, 2022.

  • Tags

You can share this post!

Raila: Nimetamaushwa na mivutano ya ODM Kisii

Wanasiasa wachoma mabilioni njaa ikiuma

T L