• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 10:50 AM
Raila: Nimetamaushwa na mivutano ya ODM Kisii

Raila: Nimetamaushwa na mivutano ya ODM Kisii

NA RUTH MBULA

KIONGOZI wa ODM, Bw Raila Odinga, amefichua kwamba juhudi zake za kusuluhisha mivutano ya kisiasa inayokumba chama hicho na muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya katika Kaunti ya Kisii, zimekosa kuzaa matunda.

Bw Odinga aliye pia mwaniaji urais wa muungano huo, alisema amejaribu kuzungumza na viongozi katika eneo hilo mara kadhaa.

Kwa mara kadhaa, mikutano ya muungano huo imekuwa ikikumbwa na ghasia za kisiasa.

Bw Odinga alisema amewarai viongozi kuweka kando tofauti zao za kisiasa ili kuuwezesha muungano huo kushinda viti vingi zaidi kwenye uchaguzi wa Agosti 9.

“Nimekuwa nikilaani ghasia hizo. Hapo awali, nimefanya vikao kadhaa na viongozi kutoka Kisii na kuwashauri kuwa hakupaswi kuwa na chuki baina yao, hasa wanapokabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa wapinzani wetu. Niliwaambia kuwa wote ni wa familia moja katika Azimio, licha ya kuwa katika vyama vya ODM, Jubilee, UPA, DAP-K kati ya vingine,” akasema.

“Nitawaita tena na kufanya kikao nao. Tutakubaliana kuwa wanafaa kuendesha kampeni zao bila kuchukiana au kudharauliana,” akasema Bw Odinga.

Wadadisi wanasema kuwa ikizingatiwa umebaki mwezi mmoja pekee uchaguzi mkuu kufanyika, kauli ya Bw Odinga imekuja wakati ufaao.

Bw Odinga alisema angetaka kuona kampeni za muungano huo zikiendeshwa kwa njia ya amani ili kutowapa wapinzani nafasi kupenya kisiasa katika eneo hilo.

Bw Odinga alitoa kauli hiyo wikendi, kwenye mahojiano ya pamoja na vyombo vya habari kutoka eneo la Nyanza. Alikuwa akijibu swali kutoka kwa mwanahabari mmoja kuhusu uhusiano mbaya uliopo baina ya Gavana James Ongwae na mwaniaji ugavana katika kaunti hiyo kwa tiketi ya ODM, Simba Arati.

Mivutano kati ya mirengo hiyo miwili ndiyo inatajwa kuchangia kuvurugika kwa mkutano wa kisiasa uliohutubiwa na mgombea-mwenza wa Bw Odinga, Bi Martha Karua, wiki iliyopita.

Polisi mmoja alikamatwa baada ya kudaiwa kulipua kifaa cha gesi ya kutoa machozi mara tu baada ya Bi Karua kuanza kuhutubu.

Bw Odinga alikashifu kisa hicho, akikitaja kuwa cha kusikitisha.

Akaeleza: “Kwanza, ninakashifu vikali tukio lililotokea katika Uwanja wa Gusii wakati Bi Karua alikuwa akikutana na akina mama. Ni jambo la kusikitisha na ambalo lazima tulikashifu kwa njia zote. Ninafahamu kuwa polisi mmoja alikamatwa. Hata hivyo, kuna uwezekano mkubwa alifadhiliwa na mtu.”

  • Tags

You can share this post!

Wezi wavamia kanisa na kuiba mali yenye thamani ya Sh250,000

Ashtakiwa kwa madai ya kuwalaghai akina mama Sh9m

T L