• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 1:12 PM
Wanasiasa wachoma mabilioni njaa ikiuma

Wanasiasa wachoma mabilioni njaa ikiuma

NA LEONARD ONYANGO

WANASIASA wanazidi kumwaga mabilioni ya fedha katika kampeni za uchaguzi wa Agosti 9 huku mamilioni ya wapigakura wakihangaika kutokana na makali ya njaa na bei za juu za bidhaa.

Shirika la Chakula Duniani (WFP) limeonya kuwa idadi ya watu ambao wanahitaji chakula kwa dharura inaongezeka kila uchao, haswa katika maeneo ya Kaskazini Mashariki, Pwani na Bonde la Ufa.

Shirika hilo linasema kuwa hali ni mbaya zaidi katika kaunti za Lamu, kilifi, Taita Taveta, Tana River, Turkana, Samburu, Pokot Magharibi, Baringo, Kajiado, Narok, Laikipia, Nyeri, Embu, Meru, Isiolo, Wajir, Garissa na Mandera.

Baa hilo la njaa limesababishwa na mavuno duni kutokana na ukame wa muda mrefu, kupanda kwa bei ya mbolea na kemikali za kuua wadudu wanaoharibu mazao.

Gharama ya juu ya mahindi imelazimu familia nyingi kula mlo mmoja kwa siku katika sehemu mbalimbali nchini, ikiwemo mijini haswa mitaa ya mabanda.

Kwa sasa pakiti ya kilo mbili ya unga wa mahindi inauzwa kwa Sh220 madukani. Bei ya bidhaa nyinginezo imeongezeka maradufu ikilinganishwa na mwaka jana.

Mwananchi anapoendelea kuumia, wanasiasa nao wamekuwa wakilaumiana kuhusu bei ya juu ya vyakula, ambapo wale wa Kenya Kwanza wanadai kuwa Bw Odinga na Rais Uhuru Kenyatta wameshirikiana kupandisha bei ya bidhaa nchini, ukiwemo unga.

Nao wanasiasa wa Azimio, wanalaumu Dkt Ruto kwa kushindwa kuchukua hatua kupunguza bei ya bidhaa kwani angali serikalini.

Kwa upande wake Rais Kenyatta amekuwa akijitetea kuhusiana na bei ya juu ya bidhaa akidai kuwa hali hiyo imesababishwa kwa kiasi kikubwa na vita nchini Ukraine.

Hata hivyo, wataalamu wanalaumu sera za utawala wa Jubilee kwa kushindwa kuimarisha kilimo kwa miaka 10 ambayo umekuwa uongozini pamoja na ukopaji madeni kiholela.

Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki jimbo la Nairobi Philip Anyolo mnamo Jumapili alikosoa wanasiasa wanaowania viti kwa kupuuza mamilioni ya Wakenya wanaohangaishwa kwa njaa, akisema wamesalia kimya huku Wakenya wakiumia.

AHADI ZA KUDANGANYA

Wakenya wanapoumia njaa, wanasiasa wanamwaga mabilioni kwenye kampeni kuzurura kote nchini wakitoa ahadi hewa.

Ijumaa, wanasiasa wa muungano wa Azimio la Umoja One Kenya wakiongozwa na mwaniaji wa urais Raila Odinga, mgombea mwenza wake Martha Karua na Waziri wa Usalama Fred Matiang’i, walikuwa na helikopta saba walipozuru Kaunti ya Nyamira.

Juni 13, 2022, viongozi wa Azimio walizuru Kaunti ya Kisii wakiwa na helikopta 11.

Wanasiasa wa muungano wa Kenya Kwanza nao wanapohudhuria mkutano mmoja wa kisiasa, wakiongozwa na kinara wao Naibu wa Rais William Ruto hutumia helikopta zisizopungua tano.

Helikopta zinawezesha wanasiasa kuhutubia mikutano mingi ya kampeni au kufanya kampeni katika kaunti zaidi ya moja kwa siku.

Kwa mfano, Bi Karua jana Jumatatu aliandaa kampeni katika Kaunti ya Narok na baadaye katika eneo la Njoro, Kaunti ya Nakuru.

HELIKOPTA NA MABANGO

Inagharimu Sh170,000 kukodisha helikopta kwa saa. Hivyo kukodisha helikopta kwa siku inagharimu kuanzia Sh1 milioni kwa kuzingatia idadi ya viti.

Mwaka jana pekee, wanasiasa waliagiza helikopta 41 kutoka ng’ambo wakijiandaa kwa ajili ya kampeni.

Kulingana Mamlaka ya Safari za Ndege nchini (KCAA), helikopta mpya 325, nyingi zikiwa za wanasiasa, zilinunuliwa kati ya 2020 na 2021.

Helikopta hununuliwa kwa zaidi ya Sh202 milioni ughaibuni lakini gharama huongezeka hadi zaidi ya Sh350 nchini.

Mbali na helikopta, wanasiasa wanatumia mamilioni katika kuweka mabango mijini na barabarani na kuandaa mikutano ya kisiasa.

Bango moja jijini Nairobi hugharimu kati ya Sh150,000 na Sh200,000 kwa mwezi kwa kutegemea eneo na ukubwa wake.

Wawaniaji wa ugavana wameweka mabango katika kila kona katika kaunti zote. Wawaniaji wa urais wameweka mamia ya mabango kote nchini katika juhudi za kujipigia debe.

Baadhi ya wanasiasa wameripotiwa kuishi katika hoteli za kifahari kukwepa wapigakura ambao wamekita kambi katika makazi yao wakitaka kupewa hela za chakula, karo na mahitaji mengineyo.

  • Tags

You can share this post!

Ashtakiwa kwa madai ya kuwalaghai akina mama Sh9m

Mapasta, mapadri na mashemasi kulipwa na serikali –...

T L