• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 10:50 AM
Azimio sasa yatishia kuvuruga maridhiano

Azimio sasa yatishia kuvuruga maridhiano

NA JUSTUS OCHIENG

MUUNGANO wa Azimio la Umoja-One Kenya umetishia kutohudhuria mkutano wa Kamati ya Kitaifa ya Mazungumzo (NADCO) ulioratibiwa kufanyika kesho Nakuru ikiwa Bunge la Kitaifa halitaidhinisha mabadiliko yao ya uongozi katika bunge hilo. Mkutano huo umepangwa kuanza kesho hadi Jumamosi Oktoba 28.

Bw Jeremiah Kioni, ambaye ni moja wa viongozi katika mchakato huo wa mazungumzo, alimshutumu Spika Moses Wetang’ula kwa kutatiza juhudi zao za kutekeleza mabadiliko ya uongozi wa muungano huo bungeni.

Azimio imepitisha kuondolewa kwa mbunge maalum Sabina Chege kama naibu Kinara wa Wachache.

Muungano huo ulikuwa umeamua Mbunge wa Embakasi Magharibi Mark Mwenje kuchukua nafasi ya Bi Chege, lakini uamuzi huo bado haujatekelezwa.

Bw Kioni ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Jubilee aliambia Taifa Leo kwamba mojawapo ya majukumu ya kamati ya mazungumzo ni kuhakikisha vyama vinafuata kanuni zote.

“Hatutahudhuria mkutano huo ikiwa hawatatekeleza uamuzi wa kumng’oa Sabina Chege katika wadhifa huo,” akasema Bw Kioni.

Kadhalika, Bw Kioni alimshutumu Bw Wetang’ula kwa kuegemea upande wa Bi Sabina.

“Kufikia sasa hawajafaulu kubatilisha uamuzi huo. Tunasema kwamba hatutashiriki tena mazungumzo hayo ikiwa mabadiliko haya hayatatekelezwa,” Bw Kioni alidai.

Kulingana na mpango wa kuendeleza kwa harakati ya kamati ya mazungumzo, kikosi husika kinatarajiwa kufika katika hoteli ya Sarova Woodlands jijini Nakuru Jumapili Oktoba 22 kwa mikutano ya wiki itakayokamilika Jumamosi Oktoba 28.

Kikosi hicho kitajadili muhtasari wa mawasilisho ya umma na kupitia upya memoranda na mawasilisho ya wadau miongoni mwa masuala mengine.

Tayari kamati ya mazungumzo inayoongozwa na kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka na mbunge wa Kikuyu Kimani Ichung’wah imetoa wito kamati hiyo iongezewe muda.

“Pia tunaomba kuongezwa muda. Kama mnavyofahamu, kipindi kilichotengwa kinakaribia kufika tamati na kwa kuzingatia kazi inayotusubiri, tunaliomba Bunge la Kitaifa na Seneti kuongeza muda kwa siku 30,” akasema Bi Cecily Mbarire, mwanachama wa kamati hiyo.

Lakini Bw Kioni alisisitiza kuwa kikosi chake hakitashiriki mkutano huo ikiwa matakwa yake hayatatekelezwa.

Mnamo Jumanne, Kiongozi wa Wachache katika Bunge la Kitaifa Opiyo Wandayi, alimwandikia Bw Wetang’ula kuhusu suala hilo ambalo lilikuwa na utata, akimtaka aharakishe mabadiliko hayo.

Hata hivyo, kamati hiyo tayari imeafikiana kuhusu masuala muhimu ikiwa ni pamoja na kuunda kikosi kipya kwa ajili ya uteuzi wa mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) na makamishna sita.

  • Tags

You can share this post!

Mwanamume azuiliwa kwa kukiri wivu ulimfanya amchape mpenzi...

Demu aliwahi kuniambia anapenda ufyekaji mzuri, sasa anadai...

T L