• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Baadhi ya wakazi wa Thika wafanya maandamano wakitaka Ruto akome kumshambulia bosi wake

Baadhi ya wakazi wa Thika wafanya maandamano wakitaka Ruto akome kumshambulia bosi wake

NA LAWRENCE ONGARO

BAADHI ya wakazi wa Thika walifanya maandamano kulaani matamshi yaliyotolewa na Naibu Rais Dkt William Ruto wikendi iliyopita kwa akimlenga moja kwa moja Rais Uhuru Kenyatta ambye amemuidhinisha kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga.

Wakazi hao wakiongozwa na mfanyabiashara Peter Mbugua walisema Dkt Ruto alimkosea heshima Rais Kenyatta kwa kumshambulia hadharani katika ngome yake ya kaunti ya Kiambu.

“Hatua iliyochukuliwa na Dkt Ruto ni ya kumkejeli Rais Kenyatta huku akidai anatafuta kura kutoka kwa wakazi wa Thika. Sisi kama wakazi wa hapa tumeudhika sana na tabia hiyo,” alisema Bw Mbugua.

Naye mkazi mwingine wa Thika Bi Lucy Mwangi alisema wakazi wa Thika wataendelea kufuata chama cha Jubilee chini ya Azimio la Umoja kwani huo ndio mwelekeo Rais Kenyatta anataka jamii ya kutoka Mlima Kenya ifuate.

“Sisi kama wakazi wa Thika na Mlima Kenya kwa ujumla hatutakubali kugawanywa kwa misingi ya vyama vya kisiasa. Kwa hivyo kiongozi yeyote anayefika Mlima Kenya aje na sera zake tuzikague badala ya kuongoza mgawanyiko miongoni mwetu,” alisema Bi Mwangi.

Naye Bw James Muroki aliyesema anawakilisha vijana wa Thika na vitongoji vyake alisema hawatakubali kupotoshwa ili kufuata kiongozi fulani “huku Rais wetu mpendwa Kenyatta akidhalilishwa.”

“Sisi tunaelewa vyema kuna viongozi wa kutoka nje ya Thika waliokuja kumlaumu rais kwa maslahi yao wenyewe. Sisi vijana tumekubaliana tutakuwa ‘rada’ ambapo hatutakubali kuchezewa shere,” alibainisha Bw Muroki.

Bi Beth Wangare mkazi wa Thika alisema wao kama wanawake watafuata mwongozo wa rais Kenyatta na hawatakubali viongozi wa kugawanya wakazi wa Thika.

“Wakazi wa Thika hawataki kupotoshwa bali wanataka kupewa mwongozo utakaowapa matumaini,” akasema Bi Wangare.

Dkt Ruto alimlaumu Rais Kenyatta kwa kile alichokiita ni usaliti.

Naibu Rais alisema alitoa mchango mkubwa sana wakati wa kampeni ili Kenyatta aweze kuwa rais lakini baadaye aliachwa kwenye mataa kwa zaidi ya miaka minne.

Pia alikosoa mwelekeo aliouchukua Rais Kenyatta wa kumuidhinisha kiongozi wa ODM Raila Odinga kama anayetaka amrithi kuwa rais wa tano wa Kenya.

 

Baadhi ya viongozi wengine walioandamana na Dkt Ruto ni Bw William Kabogo, aliyekuwa gavana Ferdinand Waititu, spika wa kaunti ya Kiambu Stephen Ndichu, seneta wa Kiambu Kimani Wamatangi, Alice Ng’ang’a, Bw Kimani Ichung’wa, mbunge wa Thika Patrick ‘Jungle’ Wainaina, na wawaniaji wengine wengi wa viti vya uongozi kupitia tiketi ya UDA.

  • Tags

You can share this post!

Kocha wa Ingwe awataka mashabiki wawe na subira

Chelsea waomba kucheza na Middlesbrough bila mashabiki...

T L